Pages

May 28, 2015

BUNGE LA BAJETI KUONGEZEWA SIKU 10 KUJADILI MISWADA!!


Bunge la Bajeti lililokuwa livunjwe Juni 27, mwaka huu litaongezwa siku 10 ili kutoa nafasi ya kujadiliwa kwa miswada takriban 10 kinyume na historia yake.
Mkutano huo wa 20 wa Bunge la 10 ni wa mwisho katika uhai wa chombo hicho cha kutunga sheria kabla ya kuvunjwa, kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Taarifa zilizotufikia na kuthibitishwa na Ofisi ya Bunge na Rais Jakaya Kikwete, zilieleza kuwa tayari makubaliano yamefikiwa baina ya Bunge na Serikali ili kuwezeshwa kufikishwa miswada hiyo katika kipindi hiki cha Bunge la Bajeti.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Tano wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), juzi usiku, Rais Kikwete alisema makubaliano hayo yamekwishafanyika na miswada itakayojadiliwa mmojawapo ni wa kuanzishwa tume ya utumishi ya walimu, ambayo inawezesha walimu nchini kuwa na chombo kimoja cha kuwasimamia.
“Tayari tumezungumza na Spika wa Bunge na tumekubaliana katika kikao kinachoendelea kitaongezwa siku 10 ili kuwezesha kumaliza shughuli za serikali ikiwamo miswada,” alisema.
Chanzo kingine cha habari ndani ya Serikali kilieleza kuwa moja kati ya miswada itakayowasilishwa na Serikali ni pamoja na marekebisho ya sheria ya uchaguzi pamoja na muswada wa sheria ya vyombo vya habari.
 Sababu nyingine inayotajwa kuhusu kuongezwa muda kwa Bunge hilo ni Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ambao ndiyo wenye jukumu la kuchagua mgombea urais wa chama hicho, ambao utafanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 11 hadi 12.
Wabunge wote wa CCM ni wajumbe wa mkutano huo, hivyo kama Bunge litavunjwa Juni 27, 2015 watapoteza sifa za kuwa wajumbe wa mkutano huo.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu chama hicho tawala kuhusishwa na nyongeza ya siku za Bunge hilo alisema, “Huo ni upuuzi mwingine sasa. Vikao vya CCM vimepanga ratiba kabla hata ya huo uamuzi wa Bunge unaousema. Hakuna ukweli katika hilo.”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama alipoulizwa kuhusu suala hilo alishindwa kukubali wala kukataa na kutaka atafutwe Katibu wa Bunge.Tayari Chama cha Wamiliki wa vyombo vya Habari Tanzania (Moat), kimeunda timu maalumu itakayokwenda bungeni kuwashawishi wabunge wasiupitishe muswada wa sheria wa vyombo vya habari baada ya kubaini umejaa kasoro.
Muswada huo ulioandaliwa na Serikali ulitakiwa kuwasilishwa katika mkutano wa 19 wa Bunge kwa hati ya dharura bila mafanikio na tayari Rais Kikwete amesema atausaini kabla hajaondoka madarakani.
Naibu Spika, Job Ndugai alipoulizwa alisema: “Hilo jambo bado hatujakaa katika kamati ya uongozi kulijadili vizuri. Bado hatujajua Serikali inaleta miswada gani. Ila pamoja na hayo, hicho kitu (kuongeza muda) kitakuwapo.”
Aliongeza, “Unajua mikutano ya Bunge huwa ni 20 tu, bado hatujajua hicho kikao kitakachokuja kitaitwaje. Jambo hili bado ni bichi sana na huko nyuma hatujawahi kuwa na kitu kama hiki.

“Tutakaa katika kamati za uongozi kujadili. Miswada inayoletwa ni muhimu sana kwa nchi. Mfano lazima kutakuwa na masuala ya uchaguzi, yaani kuiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) masuala fulanifulani hivi,” alisema.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Hiyo barua (ya Serikali) sijaiona na wala sijajua hilo jambo. Kama miswada itakuwapo basi muda utaongezwa.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Juma Mtanda akizungumzia muswada wa habari alisema,
 “Siujui na sijawahi kuuona ila nasikia tu kwamba kuna mpango wa kuuleta bungeni. 
Ninachokisubiri sasa ni muswada husika kuletwa katika kamati yangu na hapo ndipo nitakuwa na maoni mazuri zaidi.” Hata hivyo, Mtanda alisema wakiupata, kamati hiyo haitakuwa tayari kuburuzwa na watahitaji maoni ya wadau wa habari.
Waziri Kivuli wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi alisema: “Hata sisi tunakisikia kitu kama hicho. Tunachokifanya sasa ni kujipanga tu na kuungana na wadau wa habari kupinga muswada huu bungeni.”

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...