Pages

May 30, 2015

ASILIMIA 42% YA WATOTO WAMEDUMAA TANZANIA

Profesa Joyce Kinabo wa Chuo Kikuu cha Sokoine kilichopo mkoani Morogoro akizungumzia masuala ya lishe kwa waandishi wa habari hawapo pichani,jana katika mkutano wa wa masuala ya Lishe uliondaliwa na taasisi ya kimataifa ya chakula na lishe (FANUS), uliofanyika jijini Arusha.Picha na Ferdinand Shayo

Asilimia 42 ya watoto wamedumaa nchini Tanzania hali inayosababishwa na kukosekana kwa lishe bora yenye virutubisho hivyo hivyo kusababisha udumavu na kuathiri afya ya akili.



Profesa Joyce Kinabo wa Chuo Kikuu cha Sokoine kilichopo mkoani Morogoro amesema kuwa kukosekana kwa lishe bora kumekua kukiathiri maendeleo ya taaluma kwa watoto na kuzorotesha maendeleo ya jamii kwa ujumla.



Joyce akizungumza katika mkutano wa wa masuala ya Lishe uliondaliwa na taasisi ya kimataifa ya chakula na lishe (FANUS), uliofanyika jijini Arusha amesema kuwa kati ya watoto 100 watoto 42 wanakabiliwa na tatizo la udumavu hivyo ameitaka jamii na serikali kutilia mkazo suala la lishe bora na virutubisho ili kuondokana na tatizo hilo.



“Serikali na watunga sera wanapaswa kutambua uhusiano ulioko kati ya lishe bora na maendeleo ya taifa,elimu ya lishe na virutubisho itolewe kuanzia ngazi ya familia,jamii hadi kitaifa na pia mashuleni somo la lishe lirudishwe ili kuchochea ustawi bora wa jamii na taifa” Alisema Joyce



Amesema kuwa jamii ya wafugaji hususani wamasai wanakabiliwa na tatizo la udumavu ,ukondefu na upungufu wa damu mwilini kwa kukosa kutumia mboga mboga na matunda na vyakula vingine  kwani jamii hiyo hupendelea maziwa na nyama.



“Asilimia 16% wana kimo kisicholingana na umri wao yote haya yanasababishwa na lishe duni kwa baadhi ya watu” Alisema Profesa



Profesa Tola Atinmo wa chuo kikuu cha Ibadan nchini Nigeria kitengo cha Virutubisho vya binadamu amesema kuwa haki ya kupata lishe na virutubisho ni haki ya msingi ya kila binadamu kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wa haki za binadamu wa kimataifa wa mwaka 1948.



Ameishauri serikali kuhakikisha kuwa inaboresha masuala ya lishe,afya na usalama wa chakula kwa raia wake .



Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,Daudi Felix Ntibenda amesema kuwa mkutano huo unatoa fursa kwa wataalamu wa masuala ya lishe nchini na viongozi kujifunza masuala hayo muhimu katika maendeleo ya jamii.
 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...