WAZIRI WA NISHATI NA MADINI AZINDUA AWAMU YA PILI YA USAMBAZAJI UMEME VIJIJINI


Waziri wa Nishati na Madini,George Simbachawene(katikati)akizindua mradi wa usambazaji Umeme vijijini(Rea)awamu ya pili katika Kijiji cha Upper Kitete wilayani Karatu mkoa wa Arusha unatekelezwa na mkandarasi wa kampuni ya Angelique International Ltd ya India kwa thamani ya Sh.11 bilioni .

Waziri wa Nishati na Madini,George Simbachawene akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua mradi wa usambazaji Umeme vijijini(Rea)awamu ya pili katika Kijiji cha Upper Kitete wilayani Karatu mkoa wa Arusha unatekelezwa na mkandarasi wa kampuni ya Angelique International Ltd ya India kwa thamani ya Sh.11 bilioni juzi,kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Karatu,Omari Kwaangw' na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya,Lazaro Maasay.     
 
 
Filbert Rweyemamu
Arusha.Hatimaye Kijiji cha kwanza kuanzishwa  katika mfumo wa Vijiji vya Ujamaa wakati wa awamu ya kwanza  ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere cha Upper Kitete,Kata ya Mbulumbulu wilayani Karatu kimepata  umeme  kupitia mradi wa Usambazaji  umeme vijijini (Rea).

Akizindua mradi huo Waziri wa Nishati na Madini,George Simbachawene alisema katika awamu ya pili ya usambazaji umeme vijijini kiasi cha Sh 43 bilioni zitatumika kwajili hiyo mkoani hapa, wakati wilaya ya Karatu itatumia Sh 11 bilioni .

Aliiagiza Shirika la Umeme nchini Tanesco kuwaelimisha wananchi kuona umuhimu  wa matumizi ya    umeme kwenye nyumba na maeneo ya  shughuli za kiuchumi  kwani bila hivyo fedha zilizotumika kwenye mradi huo hazitakua na tija iliyokusudiwa .

“Umeme utakua na tija kwa wilaya hii iwapo utatumika ipasavyo  katika huduma za kijamii katika vituo vya afya,shule,shughuli za kiuchumi zinazohitaji matumizi ya umeme na majumbani,”alisema Simbachawene.

Awali Mkuu wa wilaya ya Karatu Omari Kwaangw’ alisema usambazaji umeme vijijini utafungua fursa za ajira kwa vijana kujiajiri katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na kuwafanya waishi maisha ya kisasa kama wananchi wengine nchini.

“Kijiji chetu kina historia ya muda mrefu,kilikua ni kwanza kuanzishwa wakati wa vijiji vya ujamaa miaka ya 60 tujipongeze kupata umeme ambao gharama yake naamini kila mwananchi anaimudu ya Sh 27,000 tu baada ya mwezi  Juni itapanda hadi 127,000 hivyo tumieni fursa hii ipasavyo,”alisema Kwaangw’

Alisema amekua akipokea barua za wananchi wanaotaka kuunganishwa na umeme hasa kwenye maeneo ya kijamii kikiwemo Kituo cha afya katika Kata ya Baray ili kuwezesha huduma za afya kupatikana muda wote.

Meneja wa Tanesco Kanda ya Kaskazini,Ngerere Makoye akitoa taarifa ya mradi huo,alisema zaidi ya wananchi 3,294 wanatarajiwa kuunganishiwa umeme katika vijiji mbalimbali wilayani humo.

Hata hivyo alisema moja ya changamoto ilikua ni gharama kuwa kubwa kutokana na umbali kutoka Kijiji kimoja hadi kingine na mwitikio mdogo wa wananchi  kuchangia gharama ya kiasi cha Sh 27,000 za kuwekewa umeme majumbani mwao.

Mkazi wa  Kijiji hicho,Stephano Ngaida  alisema walikua wakitumia fedha zaidi kwaajili ya kusaga nafaka kwa kutumia mashine zinazotumia Dizeli lakini wamepata unafuu baada ya umeme wa gridi kufika Kijijini kwao huku Mwalimu Julius Sarwat anayefundisha katika Chuo cha Ufundi Mbulumbulu alisema Chuo chao kitanufaika kwa kuanzisha masomo ya Komputa na kufunga mashine za uchomeleaji.


Post a Comment

Previous Post Next Post