Na Ferdinand Shayo,Simanjiro.
Jamii ya Wafugaji imeshauriwa
kutilia mkazo suala la kuwasomesha watoto wa kike badala ya kuwabagua na
kuwaozesha katika mdogo jambo linalozototesha maendeleo ya jamii
hizo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Simanjiro Grace Mbarouk amesema kuwa endapo jamii hizo zitahamasika na
kuwapeleka watoto wa kike shuleni jamii itapata ukombozi ikiwa ni pamoja
na kuondokana na umasikini.
Akizungumza katika Uzinduzi wa
Miradi ya Ujenzi wa Bwalo la Wanafunzi,Nyumba za walimu na madarasa katika
shule ya sekondari Emboreet uliodhaminiwa na ECLAT Foundation,Grace
ameitaka jamii ya wafugaji kuacha kasumba ya kuwabagua watoto hao na badala
yake kuwapatia haki yao ya msingi ya kupata elimu ili wawe chachu ya maendeleo
ya jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera
amewataka wazazi wote kuhakikisha kuwa wanawapeleka shule watoto waliofaulu
kwenda kidato cha kwanza na iwapo watakaidi agizo hilo watachukuliwa hatua ,pia
ameipongeza ECLAT Foundation kwa juhudi zao za kuisaidia jamii ya wafugaji
iweze kupata elimu bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa ECLAT
Foundation ,Peter Toima amesema kuwa taasisi yake imedhamiria kusaidia jamii ya
wafugaji katika masuala ya elimu na pia kusaidia vikundi vya kinamama ili
waweze kukua kiuchumi.
Beatrice Elias Mwanafunzi wa kidato
cha pili katika Shule ya Sekondari Emboreet anaeleza changamoto
zinazowakabili katika jamii yake ikiwemo kupangiwa zamu ya kuchunga
ng’ombe na kufanya kazi nyingine kiasi cha kukosa muda wa kujisomea na kurudi
nyuma kitaaluma.
Mabadiliko ya teknolojia pamoja na
hali ya hewa yanaisukuma jamii ya wafugaji kubadilika ili kuendana na wakati na
mahitaji .Jamii za wafugaji hazina budi kujiendeleza kielimu na kupata maarifa
yatakayowaletea maendeleo ya kijamii,kiuchumi na kisiasa.
No comments:
Post a Comment