Freeman Mbowe,Mwenyekiti wa Chadema. PICHA|MAKTABA.
Dar es Salaam. Wakati
wenyeviti wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
pamoja na kamati zake za kitaalamu wanakutana Zanzibar kutafuta suluhu
kuhusu mgawanyo nafasi za kugombea katika uchaguzi mkuu ujao, kuna
uwezekano mkubwa vyama hivyo kuteua mgombea urais kutoka Chadema.
Tovuti hii
inaweza kuripoti kwa uhakika kuwa uwezekano huo unatokana na vigezo
vinavyotumiwa na vyama hivyo kusimamisha mgombea mmoja kwa kila jimbo na
kwenye nafasi ya urais ambavyo vinaipa Chadema nafasi hiyo dhidi ya
vyama vingine katika umoja huo ambavyo ni CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Vigezo
hivyo ni matokeo ya uchaguzi 2010, idadi ya madiwani kwa kila chama,
matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Desemba mwaka jana, mtandao
wa chama nchini na nguvu ya mgombea iwapo Chadema kitamsimamisha katibu
mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kwa mara ya pili.
Taarifa
zilizolifikia Mwananchi kutoka ndani ya kamati ya ufundi ya Ukawa
zinasema pamoja na kuwapo mvutano katika baadhi majimbo Tanzania Bara,
kwa upande wa Zanzibar hakuna tatizo hilo, jambo linaloipa CUF nafasi ya
moja kwa moja kwenye ubunge, uwakilishi na hata urais wa visiwa hivyo.
Kwa
mujibu wa habari hizo, nafasi nzuri ya CUF kupita moja kwa moja
Zanzibar bila ushindani ndani ya Ukawa, inatoa fursa kwa upande wa Bara,
kwa vyama vilivyosalia kupitishwa kuwania urais wa Muungano.
Hata
hivyo, kwa vigezo vilivyotajwa hapo juu, Chadema ndiyo inakuwa na
nafasi isiyo na kipingamizi kutokana na rekodi vyama vilivyosalia Bara.
Katika
Uchaguzi Mkuu wa 2010, Chadema kilimsimamisha Dk Slaa na aliibuka wa
pili baada ya Rais Jakaya Kikwete akiwa na kura 2,271,941 (asilimia
26.34) akifuatiwa na Profesa Ibrahim Lipumba aliyepata kura 695,667
(asilimia 8.06) na Hashim Rungwe wa NCCR-Mageuzi aliyepata kura 26,388
(asilimia 0.31). NLD haikusimamisha mgombea urais.
Kwa
upande wa majimbo yaliyotokana na uchaguzi wa 2010, Chadema kiliongoza
kikiwa na wabunge 24 (wote kutoka Bara), CUF 23 (wawili kutoka Bara, 21
Zanzibar) na NCCR-Mageuzi wanne (wote wa Bara).
Katika
rekodi za uchaguzi wa mitaa zilitolewa na Tamisemi kabla ya chaguzi za
marudio, Chadema ilipata mitaa 980, ikifuatiwa na CUF (mitaa 266), NCCR
Mageuzi (28) na NLD mtaa mmoja. Kwa upande wa vijiji, Chadema
kilishinda vijiji 1,754, CUF (516), NCCR-Mageuzi (67) na NLD vijiji
viwili.
Hata kwa upande wa vitongoji Chadema kiliviongoza
vyama hivyo kwa kupata vijiji 9,145 kikifuatiwa na CUF (2,561),
NCCR-Mageuzi (339) na NLD vitongoji viwili.
Tayari
NCCR-Mageuzi kimeonyesha nia ya kumteua Dk George Kahangwa kuwania urais
wakati Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikaririwa na gazeti
hili hivi karibuni akisema kuwa chama chake kimekwishamteua kuwania
urais, hivyo jina lake litapelekwa Ukawa kushindanishwa.
Hali
ikiwa hivyo, wajumbe wa Ukawa leo watakumbana na wakati mgumu wa
kufikia maridhiano ya kugawana majimbo 19 kutokana na taarifa za kuwapo
mvutano mkali wa pande zote za vyama husika.
Wanaokutana leo ni wenyeviti wa vyama, makamu wenyeviti, makatibu na wajumbe wa sekretarieti kutoka vyama hivyo.
Kabla
ya kuanza kikao cha jana asubuhi wajumbe 16 wa Kamati ya Ufundi
walikutana na baadaye jioni wenyeviti wa umoja huo wakawa na kikao cha
awali, ikiwa ni sehemu ya vikao vya hatua za kugawana maeneo ya kuwania
ili kutoa ushindani na hatimaye ushindi dhidi ya CCM.
Chanzo cha habari kutoka ndani kimelieleza Mwananchi kuwa NLD nayo imeongeza mvutano ikihitaji majimbo matano.
Wiki
iliyopita, gazeti hili liliandika kuwa Ukawa ilikuwa imekamilisha kazi
ya ugawaji wa majimbo 170 lakini ukawapo mvutano katika majimbo 19
ambayo vyama zaidi ya kimoja vilikuwa vinayataka.
Majimbo
hayo ni Segerea, Kinondoni, Kigamboni na Ukonga ya Dar es Salaam,
Morogoro Mjini na mengine ya mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera.
“Mvutano
ni kwamba, kuna vyama vinavyotaka uwakilishi tu wa majimbo hayo lakini
kiukweli yanaweza kupotea bure tu endapo vitakabidhiwa. Wengine wanataka
kuangalia zaidi ushawishi wa chama ndani ya jimbo husika ila wengine
wanapinga, wakisema umoja huo hautakuwa na sababu kama watakosa
uwakilishi,” kilieleza chanzo hicho.
“NLD wanahitaji majimbo
matano, CUF na Chadema wanavutana zaidi, ila NCCR-Mageuzi wameonekana
kushtushwa sana na hali hiyo,” kilisema chanzo kingine kutoka
NCCR-Mageuzi.
Chanzo kingine kilieleza kuwa kamati ya
wataalamu ilishakamilisha kazi yake ya uchambuzi wa majimbo hayo na
kuwasilisha taarifa zake lakini kuna upinzani mkali ambao umeendelea
kuibuliwa na wajumbe wa umoja huo.
“Kikao cha leo
kinaashiria kuwa na mvutano, ninaamini kuna uwezekano wa kufikia mwafaka
lakini ikishindikana kabisa kwa leo lazima vitaandaliwa vikao vingine,”
kilieleza chanzo kingine.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati
ya Wataalamu, Benson Kigaila (Chadema) alisita kuweka wazi juu ya
mvutano uliopo huku akibainisha kuwa maridhiano yatapatikana.
Kigaila alisema kikao cha leo kina nafasi kubwa ya kumaliza mvutano huo na kueleza Watanzania juu ya mwelekeo wa safari yao.
Mvutano mkali
Kigaila
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni ya Mafunzo na Usimamizi wa
Kanda wa Chadema, alisema: “Kwa sasa siwezi kueleza chochote kwani vikao
ndiyo vinafanyika kwa sasa, lakini naomba vikao vikishamalizika
viongozi wetu watazunguza tu,” alisema.
Alipoulizwa juu ya
NLD kuhitaji majimbo matano, Kigaila alikiri kuwa kweli wanataka mgawo
wa majimbo lakini alikataa kutaja idadi yake.
“NLD wanayo
haki kama vyama vingine, kwa nini wasipate? Watapata, lakini kuna
taarifa sahihi zitakazoelezwa baada ya kikao cha leo.”
Jumanne
wiki hii, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bara, Magdalena Sakaya alilieleza
gazeti hili kuwa kikao hicho kitakuwa na ajenda ya kukusanya maoni na
mapendekezo ya wanachama, kujadiliana kwa pamoja ili kufikia muafaka wa
majimbo hayo.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema katika hatua za kutafuta maridhiano ya majimbo hayo, vyama vyote
vinapaswa kutambua kila nafasi ya chama kilichoshiriki kwenye
makubaliano ya Ukawa.
“Tukifuata kanuni, nadhani kuna vyama
ambavyo havitakuwa na nafasi Ukawa na haitakuwa na maana ya kuungana,
kwa hivyo lazima busara itumike zaidi. Haiwezekani chama fulani
kilazimishe kuchukua majimbo mengi kuliko kingine,” alisema Nyambabe.
Alipoulizwa
kuhusu utata katika mgawanyo wa majimbo, Dk Slaa alisisitiza kumalizika
kwa mvutano kutokana na busara za viongozi wa vyama hivyo.MWANANCHI
No comments:
Post a Comment