Mkurugenzi
wa Mipango wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Jason Rwiza,
akielezea namna TANROADS inavyofanya kazi za ujenzi wa barabara hapa
nchini kwa ujumbe wa viongozi kutoka Sudan Kusini katika ofisi za Wakala
hao jijini Dar es salaam jana.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Barabara wa Sudan Kusini Eng. Kenyata Warille,
akifafanua namna Mamlaka yake inavyofanya kazi za ujenzi wa barabara
nchini kwao. (Nyuma wa kwanza kulia) ni Mwakilishi wa JICA wa Sudan
Kusini Tomoki Kobayashi, akifatilia kwa makini.
Naibu
Waziri wa Usafirishaji, Barabara na Madaraja wa Sudan Kusini Mh. Simon
Mijok (Wa kwanza kulia), akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi wa
Sudan Kusini Eng. Gabriel Makur, baadhi ya vitabu walivyopewa na Wakala
wa Barabara nchini (TANROADS) kwa ajili ya kuwasaidia kuboresha taasisi
zao za ujenzi.
Ujumbe
wa viongozi kutoka Sudani Kusini wakiangalia namna magari yanavyopimwa
uzito kwa kutumia njia ya kigitali yenye uwezo wa kurekodi taarifa zote
za vipimo na kupatikana katika mtandao wa TANROADS. Mzani huo unapima
gari moja kwa muda wa sekunde 30 tofauti na wa zamani.
Gari
lililozidisha uzito likipimwa katika mzani mpya wa kisasa wa Vigwaza
mkoani Pwani. Magari kama haya yanayozidisha uzito huharibu miundombinu
ya barabara nchini.
Ujumbe
wa viongozi wa sekta ya ujenzi na mazingira toka Sudan Kusini
umepongeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), kwa namna
unavyofanyakazi na kuahidi kushirikiana nao ili kuimarisha sekta ya
barabara na madaraja nchini mwao.
Akizungumza
katika ziara ya mafunzo inayoendelea hapa nchini Naibu Waziri wa
Usafirishaji,Barabara na Madaraja wa Sudan Kusini Mhe. Simon Mijok
amesema mfumo wa uendeshaji wa TANROADS ni mzuri na unaofaa kuigwa na
nchi yake kwani unatoa uhuru kwa wakala kuwa na mtandao wa utendaji nchi
nzima.
“Kutokana
na miaka mingi ya vita nchini kwetu miundombinu mingi ya barabara na
madaraja imeharibika hivyo njia nzuri ya kuifufua kwa haraka ni kuwa na
taasisi yenye mfumo wa utendaji kama TANROADS na Mfuko wa Barabara”,
amesisitiza Naibu Waziri Mijok.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Barabara ya Sudan Kusini (SSRA)
Eng.Kenyata Warille amesema mafunzo wanayoyapata hapa nchini
yatawawezesha kufanya mabadiliko muhimu katika taasisi zao za ujenzi na
watawatumia watanzania kuwashauri ili watumie muda mfupi kuboresha
miundombinu ya nchi yao na kwenda na kasi ya maendeleo ya nchi za Afrika
Mashariki na Kati.
Amesema
Sudan Kusini licha ya kuwa nchi kubwa kwa eneo bado ina mtandao wa
barabara wa Km 19,073 zinazounganisha majimbo kumi ya nchi hiyo yenye
watu takriban milioni 12.
Aidha
ujumbe huo umepata nafasi ya kujionea namna mizani ya kisasa ya Vigwaza
mkoani Pwani inavyofanya kazi na kuahidi kujenga mizani ya namana hiyo
nchini mwao kutokana na utendaji kazi wa haraka na unaozingatia
teknolojia.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri huyo wa Usafirishaji,Ujenzi na Madaraja
ameishukuru Tanzania kwa hatua mbalimbali inazochukua kuipatanisha nchi
yake ili amani na utulivu viwepo. Pia amesisitiza kuwa ziara za mafunzo
za viongozi wa nchi hiyo zitaendelea na kuwaalika watanzania nao kwenda
Sudan Kusini kujifunza.
Naye
Mkurugenzi wa Mipango wa TANROADS Eng. Jasson Rwiza ameuhakikishia
ujumbe huo kuwa ushirikiano uliopo baina ya taasisi zao utaendelezwa ili
kubadilishana uzoefu na hivyo kuwezesha barabara za ukanda wa Afrika
Mashariki na Kati zipitike kwa urahisi na kukuza uchumi wa nchi zao.
No comments:
Post a Comment