Balozi Tsere akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari kuhusu msaada uliotolewa na Serikali ya Tanzania.
=============================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TANZANIA YAIKABIDHI MALAWI MSAADA KWA AJILI YA WAHANGA WA MAFURIKO
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhi Tani 1,200 za Mahindi na
Dawa za Binadamu kwa Serikali ya Malawi ikiwa ni msaada wake kwa wahanga
wa mafuriko yaliyotokea nchini humo mwezi Januari mwaka huu na
kusababisha maafa makubwa.
Msaada
huo umekabidhiwa hivi karibuni na Mhe. Patrick Luciano Tsere, Balozi wa
Tanzania nchini Malawi kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na kupokelewa
na Katibu Mkuu na Kamishna wa Idara ya Maafa, Bw. Paul Chiunguzeni kwa
niaba ya Serikali ya Malawi. Aidha, msafara uliopeleka msaada huo kutoka
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), uliongozwa na Luteni Kanali B.B.
Kisinda.
Katika
hotuba yake fupi wakati wa makabidhiano, Balozi Tsere alisema kwamba
msaada huo umetolewa na Tanzania ikiwa ni agizo kutoka kwa Mhe. Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana
na kuguswa kwake na maafa hayo makubwa na pia kuitikia wito uliotolewa
na Rais wa nchi hiyo Mhe. Prof. Arthur Bingu Mutharika kwa Jumuiya ya
Kimataifa na watu mbalimbali wenye uwezo kutoa msaada kwa wahanga hao wa
mafuriko.
Aidha,
Balozi Tsere alieleza kwamba, Malawi na Tanzania ni nchi jirani,
marafiki na zinazoshirikiana katika masuala mbalimbali ikiwemo majukwaa
ya kimataifa kama vile Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa.
“Hivyo,
kwa kutambua mahusiano hayo ya ujirani mwema na udugu baina ya nchi
hizi na watu wake, Tanzania imeona ni jambo jema kushirikiana na jirani
yake katika kupunguza athari za maafa hayo kwa wahanga hao kwani siyo
vyema kuona jirani yako amepatwa na matatizo na kisha unakaa kimya”
alisema Balozi Tsere.
Mhe.
Tsere aliongeza kwamba ingawa msaada huo hautoshelezi kutatua tatizo
hilo kabisa bado utaweza kusaidia wahanga hao na kupunguza tatizo
lililopo kwa kiasi Fulani.
Malawi
ilikumbwa na mafuriko mwezi Januari mwaka huu. Mafuriko hayo
yalisababisha maafa makubwa ikiwemo watu kupoteza maisha, nyumba
kuharibiwa na mazao mashambani kusombwa na maji. Kwa hivi sasa familia
katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo hazina mahali pa kuishi na
zinahitaji msaada wa chakula na kumekuwa na magonjwa ya mlipuko katika
maeneo hayo kama vile kipindupindu.
IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
27 MACHI, 2015
|
No comments:
Post a Comment