Pages

March 13, 2015

NI MAFANIKIO KUWA NA ASKARI WANAWAKE KATIKA ULINZI WA AMANI UN-MHE SIMBA

Katika picha hii ya maktaba anaoneka Mhe. Asha-Rose Migiro ( Mb) wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa na baadhi ya askari wanawake kutoka JWTZ wanaoshiriki katika operesheni ya kulinda amani kupitia Umoja wa Mataifa huko Lebanon. Katika mchango wake, Mhe. Simba pamoja na mafanikio mengine ambayo Tanzania imeyapata katika miaka 20 tangu mkutano wa Beijing ni pamoja na askari wanawake kupata fursa za kushiriki katika operesheni za kulinza amani zinazoratibiwa na Umoja wa Mataifa.
Mhe. Sophia Simba ( Mb) Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto akizungumza (alhamisi) katika majadiliano ya jumla katika mkutano wa Kamisheni 59 kuhusu Hadhi ya Wanawake. Mhe. Waziri anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwamo wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.Tanzania ni kati ya nchi 13 zinazoiwakilisha Afrika katika Kamisheni hii inayoundwa na nchi 45.
Sehemu ya ujumbe wa Mawaziri kutoka nchi za Afrika wakati wa mkutano wao uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Nchi za Afrika.
Pamoja na kuzungumza katika majadiliano ya jumla, Mhe Waziri Sophia Simba pia alipata fursa ya kuhushiriki Mkutano wa Mawaziri kutoka Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Afrika karibu na UN. Mkutano huo ulikuwa wa kujadiliana na kupitisha maazimio mbalimbali kuhusu maudhui ya mwongo wa wanawake wa Afrika. Pichani Mhe. Waziri akiwa na Katibu Mkuu wake Bi. Anna Maembe wakifuatilia majadililano hayo.

Na Mwandishi Maalum, New  York

Ushiriki wa askari wanawake   katika Operesheni za Ulinzi wa Amani za  Umoja wa Mataifa,  ni baadhi ya  mafanikio ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajivunia miaka 20 baada ya Mkutano wa Kihistoria wa wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.

Waziri wa  Maendeleo ya Jamii, Jinsia na  Watoto, Mhe. Sophia Simba ( Mb) ameyasema hayo  leo ( alhamis) wakati alipokuwa akitoa tathmini na changamoto za utekelezaji wa  maazimio muhimu yaliyofikiwa katika mkutano huo wa  wanawake Beijing. 

Mhe. Waziri Simba, anaongoza ujumbe wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania  katika Mkutano wa Hadhi ya Wanawake ( CSW) unaoendelea hapa  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  katika Ujumbe huo  wa Tanzania unajumuisha na washiriki kutoka  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akiwamo  Mhe. Zainab Omar Mohammed,  Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, vijana, wanawake na watoto, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. 

“ Katika miaka  miaka  20 iliyopita, yapo  mambo mengi ambayo Tanzania tumepiga hatua za kuridhisha, katika maeneo ya uwezeshwaji  na fursa sawa kwa wanawake. Katiba za pande zote mbili za Muungano  zinaainisha vema kuhusu hadhi ya mwanamke. Na   Katika  katiba mpya inayopendekezwa  hivi sasa  kuna   eneo  ambalo linazungumzia kwa kina Usawa wa Jinsia na Uwezeshwaji wa wanawake.” anasema Waziri Simba.

Vile vile ameeleza  baadhi ya sheria  ambazo ama zimefanyiwa marejeo au kutungwa kwa lengo la kuboresha usawa wa kijinsia. Amezitaja baadhi ya  sheria hizo kuwa ni sheria zinazohusu watoto,  sheria zinazohusu usafirishaji wa binadamu,  sheria ya ardhi, HIV/AIDS na sheria ya makosa ya kujamiana.

 Kuanzishwa kwa dawati la jinsia na watoto katika vituo vya Polisi,  vituo  vya kuhifadhi  watoto,  vituo kwaajili ya  wanawake wanaofanyiwa ukatili na mtandao wa viongozi wa madhehebu ya dini kuhusu ukatili dhidi ya wanawake. Ni baadhi ya mafanikio ambayo yameelezewa na Mhe. Waziri.

Ameeleza  zaidi kwa kusema, Wanawake wengi sasa wanashiriki katika siasa ambapo  kwa mfano  asilimia 36 ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ni wanawake na   kwa upande wa Zanzibar asilimia 33 ya  Wawakilishi ni wanawake. Na  kwamba  kumekuwapo  pia ongezeko  la idadi ya  wanawake Majaji na Mahakimu na wanaoshika nafasi za uongozi.

Mhe. Simba amewaeleza wajumbe wanaoshiriki  mkutano huo  kwamba katika kuhakikisha  panakuwa na fursa sawa  katika  ajira  utumishi wa Umma,   kuna  kifungu   katika sheria za utumishi wa umma vinavyoainisha kwamba  pale  mwanamke na mwanaume wanapokuwa na sifa zinazolingana, basi mwanamke atafikiriwa kwanza.

Kwa upande wa elimu,  pamoja na  kuwa na  uwiano sawa kati ya wavulana na wasichana katika shule za msingi. Anasema elimu ya  msingi inatolewa bure katika shule za serikali   na kwamba utaratibu huo pia utafanyika katika  shule za  sekondari  za umma. Aidha  ameelezea ongezeko la wanafunzi wa kike wanaochukua masomo ya sayansi.

Kwa upande wa Afya,  Mhe. Waziri amesema  Tanzania imepiga hatua za kuridhidha katika upunguzaji wa  vifo vya wanawake wajawazitio na vya watoto wachanga.

Hata hivyo pamoja na  mafanikio  hayo na mengine mengi ambayo  Tanzania inajivunia kuhusu hadhi ya wanawake na watoto wa kike,  anasema kama ilivyo kwa mataifa mengi yanayoendelea, Tanzania pia bado inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo  za uhaba wa fedha kwa miradi inayohusu masuala  ya jinsia,  ndoa na mimba za utotoni,  umaskini wa kaya na ukatili dhidi ya wanawake.


Mhe. Waziri Simba, Tanzania imejifunza kutokana na changamoto hizo na nyinginezo na kwamba imejipanga vema kutekeleza baadhi  ya changamoto hizo  hususani  upunguzaji wa umaskini,  kupitia malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya  2015.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...