Waathirika wa mvua ya mawe na upepo
mkali iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 40 katika kijiji cha Mwakata
wilayani Kahama, Shinyanga, jana walitawanywa kwa mabomu ya machozi na
polisi wa kutuliza ghasia (FFU) baada ya kufunga barabara kuu ya Isaka-Kahama kuelekea nchi jirani za Rwanda, Uganda na Burundi,kwa kulala barabarani na kuweka mawe na miti.
Tukio hilo lililotokea alfajiri jana
liliathiri baadhi ya wasafiri wa mabasi makubwa yaliyokuwa yakisafiri
kwenda mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na mikoa ya jirani.
Waathirika hao walichukua uamuzi huo
baada ya misaada ya chakula, magodoro, mablanketi na maturubai
uliotolewa na wasamaria wema, ukiwa umefungiwa ndani ya darasa na
wahusika wakishindwa kutimiza agizo la Waziri Mkuu Mizengo Pinda la
kuwataka kuwapa msaada huo.
Mwathirika wa tukio hilo, Benjamini Ndege, alisema wananchi waliamua kuchukua hatua hiyo kutokana na serikali kutowajali.
“Hawa
waliofanya hivi ni wale ambao nyumba zao zimeharibika upande, zikiwa na
mifugo na mali nyingine, lakini tunashindwa kuhudumiwa mahitaji
muhimu…wanataka wote tukusanyike shuleni, sasa tunakaa hapo na mifugo
yetu,” Ndege.
Alishangazwa na hatua ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, kutumia polisi kuvurumisha mabomu wakati wakiwa katika majonzi ya kupoteza ndugu zao katika janga hilo.
Alisema mabomu yalirushwa na polisi hao,
yamesababisha akinamama na watoto kukimbilia porini wakihofia maisha
yao na kutowahi kuona hali hiyo.
“Tumeahidiwa
misaada mbalimbali, lakini hatupewi na mvua inanyesha tunabaki kulowa
nje wakati maturubai yapo…tunaomba tufanyiwe yale aliyoahidi waziri mkuu,”Maganga.
NIPASHE
Hatimaye Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra CCC) limesikia kilio cha wananchi na kuahidi kushusha nauli za daladala na mabasi yaendayo mikoani.
Katibu Mkuu wa Sumatra CCC, Oscar
Kikoyo, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema nauli ya
daladala itashuka kwa shilingi 50 na mabasi ya kwenda mkoani itashuka
kwa asilimia 15 hadi 24 kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta duniani.
“Kwa mikoani basi la kutoa Dar es Salaam kwenda Arusha nauli itashuka toka Sh. 36,000 hadi Sh. 28,325 kwa mabasi ya luxury,” Kikoyo.
Alisema sekta ya mafuta ni muhimu kwa
kuwa inachangia kati ya asilimia 20 hadi 30 katika sekta ya usafirishaji
na kuwa baraza hilo linaangalia pande zote mbili kwa mtoa huduma na
mteja ili kuweka unafuu wa gharama.
Alisema mtoa huduma akipata zaidi ya
asilimia 25 ya faida lazima nauli itashuka lakini ikiwa chini ya
asilimia tano nauli zitapanda na mapendekezo hayo watayawasilisha
Sumatra Jumatatu ili nauli ziweze kushuka mapema iwezekanavyo.
Hata hivyo, alisema kuwa iwapo Sumatra itakataa mapendekezo hayo basi watayapeleka Tume ya Ushindani kwa usuluhishi zaidi.
Hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza kushusha bei za mafuta ya taa, petroli na dizeli nchi nzima.
Bei za jumla zimepungua tofauti na
ilivyokuwa mwezi uliopita ambapo petroli imeshuka kwa Sh. 148.66 kwa
lita sawa na asilimia 7.16, dizeli Sh.118.69 kwa lita sawa na asilimia
6.16 na mafuta ya taa Sh.105.81 kwa lita sawa na asilimia 5.59.\
NIPASHE
Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Inspekta Prisca Komba, ameibuka mshindi wa Tuzo ya Mwanamke mwenye Mafanikio Tanzania kwa mwaka 2014.
Inspekta Komba, ambaye pia anasimamia
Dawati la Jinsia kwenye mkoa huo wa kipolisi, pia alishinda Tuzo ya
Mwanamke Mwenye Mafanikio katika Sekta ya Umma.
Wengine waliopata tuzo mbalimbali ni pamoja na Debora Mwenda, aliyepata tuzo ya Mwanamke mwenye mafanikio ya maisha, Penina Mlama, Utamaduni na Sanaa, Mary Gitanho, Ustawi wa Jamii, Sharmillah Bhatt, Sayansi na Teknolojia, Jennifer Shigoli, Mwanamke mdogo mwenye Mafanikio, Blandina Sembu, Habari na Mawasiliano.
Pia Dk. Wineaster Anderson, Taaluma,
Nahida Esmail, Elimu, Devotha Likokola, Biashara na Ujasiriamali,
Jacqueline Mkindi, Kilimo, Mpendwa Chihimba, Afya na Angel Eaton,
Michezo.
Tuzo hizo, zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Taasisi ya Tuzo za Wanawake Wenye Mafanikio Tanzania (TWAA) inayoandaa tuzo hizo zilizokutanisha wanawake zaidi ya 700.
Rais na Mwandaaji wa tuzo hizo, Irene
Kiwia, akikabidhi tuzo hizo alisema jumla ya Wanawake 36 waliingia tatu
bora katika vipengele 12 vilivyokuwa vinashindaniwa na kati ya hizo
jumla ya tuzo 14 zimetolewa.
“Katika
kuelekea siku ya wanawake Duniani ambayo inafanyika kitaifa leo tumeona
ni vyema tukawapatia tuzo wanawake ambao wameleta mabadiliko chanya
ndani ya jamii, kwani mafanikio yao yanaleta hamasa kwa wanawake wengine
wenye malengo,” Kiwia.
Alivitaja vipaumbele vya mwanamke ambaye
anataka kuleta mabadiliko ndani ya jamii kuwa ni ndoto, uthubutu,
kufuatilia ndoto, uvumilivu na ustahimilivu.
Akizungumzia tuzo hiyo, Ispekta Komba,
ameishukuru jamii kwa kutambua umuhimu na kazi ambazo amekuwa akizifanya
ndani ya jamii na kwamba amepata nguvu ya kuendelea kufanya kazi hiyo
kwa ufanisi zaidi.
“Sikutegemea
kupata tuzo hii na nimelia kwa chozi la furaha, namuomba Mkuu wa Jeshi
la Polisi Tanzania (IGP), Ernest Mangu, pamoja na Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mathias Chikawe, kutoa vyeo kwa wakati ili kuongeza motisha wa
kufanya kazi,”Komba.
Aliitaka serikali na mahakama
kuhakikisha inasimamia kesi za udhalilishaji na ukatili wa kijinsia
zinatolewa hukumu mapema ili kumaliza vitendo hivyo ndani ya jamii na
pia kupunguza kasi ya udhalilishaji ambayo inatokana na watuhumiwa
kutochukuliwa hatua kwa wakati.
MWANANCHI
Rais Paul Kagame amemshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuhudhuria mkutano wa tisa wa nchi zilizoungana kutekeleza Miradi ya Miundombinu Ukanda wa Kaskazini za Northern Corridor Projects
uliofanyika jijini Kigali, Rwanda, akisema ni hatua muhimu katika
kufungua utekelezaji wa miradi ya miundombinu katika kanda nyingine za EAC.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana
ilisema kuwa Rais Kikwete alihudhuria kikao hicho kwa mwaliko wa Rais
Kagame na kwamba mkutano huo ulifanyika kwenye Hoteli ya Serena mjini
Kigali.
Naye Rais Uhuru Kenyatta
wa Kenya alisema kuwa ni jambo la kufurahisha kwamba Rais Kikwete
ameweza kuhudhuria mkutano wa jana kwa sababu sasa njia imefunguka
kuanza kazi ya utekelezaji wa miradi kwenye Ukanda wa Kati wa Central
Corridor unaokatisha katikati ya Tanzania.
Marais Kagame na Kenyatta walikuwa
wanazungumza wakati wa hotuba za ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika
zaidi ya saa mbili baada ya Rais Kikwete kuwasili Kigali akitokea Dar es
Salaam.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Rwanda.
Mbali na nchi hizo, Burundi na Sudan
Kusini pia zilialikwa kwenye mkutano huo kujadili hatua za utekelezaji
wa miradi mbalimbali kulingana na maelekezo yaliyotolewa katika mkutano
wa nane uliofanyika Nairobi, Kenya, Desemba 11, mwaka jana Marais hao
wawili wamekuwa wakitofautiana katika suala la waasi wa Rwanda baada ya
Rais Kikwete kumshauri Kagame kukaa meza moja na waasi wa Rwanda ili
kumaliza tofauti zao zinazosababisha maisha ya watu kupotea.
MWANANCHI
Wakati ikiwa imesalia siku chache kabla
ya kipenga cha kuruhusu wananchi kujitokeza kuwania urais, ubunge na
udiwani, moto unawaka kwenye majimbo mbalimbali ambako wabunge
wanapigana vikumbo na watu wanaoonekana kutaka kuwarithi.
Vita iliyo wazi ni ile inayohusisha wenyeviti wa vyama vya NCCR-Mageuzi na TLP, James Mbatia na Augustine Mrema
ambao wameshatoleana maneno ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano,
lakini mchuano ni mkali kwenye majimbo mengine, wakiongozwa na mbunge wa
CCM, Ester Bulaya ambaye ameeleza dhamira yake ya kutaka Jimbo la Bunda, ambalo linashikiliwa na Waziri wa Chakula na Kilimo, Steven Wassira pamoja Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Ummy Mwalimu ambaye ameonyesha nia ya kwenda Tanga.
Mchuano huo unazidishwa na kitendo cha
wabunge walioingia kwenye Bunge la Kumi kwa tiketi ya viti maalumu,
ambao sasa wataka kurejea kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kwa
kuchaguliwa na wananchi.
Wabunge wengi wa viti maalumu wameanza
kuonyesha makucha majimboni wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii
katika kile kinachoonekana ni kujiweka karibu na wananchi.
Wengi wanajishughulisha na kuchangia masuala ya maendeleo pia kuendesha au kudhamini mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu.
Kwenye baadhi ya majimbo, mchuano ni
mkali zaidi kutokana na ukweli kuwa waliokuwa wanayashikilia na ambao
baadhi walikuwa wanaonekana mibuyu, kutangaza kutorudi tena kuomba kura
kutokana na kuona imetosha au kufikiria kuwania nafasi nyingine.
Muungano wa vyama vya upinzani, Ukawa,
pia umeongeza joto hilo kutokana na ukweli kuwa vyama vya NCCR-Mageuzi,
NLD, CUF na Chadema vimepania kusimamisha mgombea mmoja kwenye majimbo
mengi.
“Nimetafakari
kufuatia maelekezo ya chama changu, nimejipima na nimetazama hali
halisi ya maendeleo na kero ya huduma na matatizo, nikaona ni wakati wa
kutatua haya,” Abdulaziz Ahmad alipoulizwa kuhusu nia yake ya kuwania ubunge wa Jimbo la Lindi, ambalo kwa sasa linashikiliwa na Salum Barwany wa CUF.
Mwanachama mwingine wa CCM, Joseph Mhagama, ambaye analitaka Jimbo la Peramiho linaloshikiliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Utaratibu wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema haoni kama mbunge wa sasa anawatumikia wananchi.
HABARILEO
Kazi anayofanya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana
katika ziara zake mikoani, sasa ni dhahiri ameanza kurejesha chama
hicho katika misingi ya asili yake ya Ujamaa, iliyoasiswa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Hilo limejidhihirisha katika kauli na
hotuba zake kwa wanachama na wananchi, kwenda kinyume na taswira
iliyoanza kujijengea mizizi, kuwa chama hicho kimeanza kuondoka katika
misingi ya Ujamaa, iliyojengwa tangu kuasisiwa kwake.
Uadilifu Katika moja ya kauli zake
alizotoa jana alipohutubia wakazi wa Mkoka katika wilaya ya Kongwa,
akiwa katika ziara ya kutembelea mkoa wa Dodoma, Kinana alisisitiza
umuhimu wa uadilifu wa wagombea kwa mtindo uliokuwa ukisisitizwa wakati
wa Mwalimu Nyerere.
Kwa mujibu wa Kinana, sifa namba moja
inayozingatiwa na wananchi katika kumpata kiongozi wa kuwaongoza, hata
kama ni mchapakazi wa kiwango cha juu, uadilifu utasimama kuwa sifa
namba moja.
Alisema kutokana na kumomonyoka kwa
maadili ya uongozi, tofauti na enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere,
wananchi sasa hawazingatii suala la uhodari na uchapakazi kama sifa
namba moja ya kumchagua mtu kuwa kiongozi wao. “Wananchi sasa wanaangalia nani muadilifu, nani sio mwizi, nani si mlaji, wapo tayari kukusamehe mambo mengine yote, lakini si suala la uadilifu,” Kinana.
Alisema kutokana na kutambua hilo, CCM
itakuwa makini na viongozi wake watakuwa wakali, katika kuhakikisha kuwa
watu wasio waadilifu wanadhibitiwa wasishike nafasi za uongozi kupitia
chama hicho, ili kujenga heshima na imani ya wananchi kwa chama hicho.
Ishara ya ukaidi Kinana aliweka wazi
kuwa moja ya ishara ya kutetereka kwa uadilifu katika utumishi wa umma,
ni tabia iliyoibuka siku za hivi karibuni, ambapo viongozi wanaokiuka
misingi ya maadili ya uongozi wa umma, wanapoombwa kukaa kando kutokana
na makosa waliyofanya, wanagoma kuondoka madarakani jambo ambalo
halikuwepo zamani.
HABARILEO
Siri ya mafanikio ya Padri feki, Josephat Asenga,
aliyekamatwa mkoani Morogoro, katika kuongoza Misa ya Kanisa Katoliki
kwa kufuataa ya Kanisa Katoliki kwa kufuata taratibu zote maalumu bila
kutiliwa shaka, imebainika.
Asenga aliyetumia vitambulisho feki,
alipojitambulisha kwa uongozi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu
Maria Madeko mkoani Morogoro, alipopewa fursa ya kuongoza Misa,
alitekeleza wajibu huo wa kipadri bila kuacha shaka.
Akizungumza na gazeti hili jana,
kiongozi mmoja wa Kanisa Katoliki (jina limehifadhiwa), alithibitisha
kuwa Asenga alipofika Parokiani hapo kati ya Mei na Juni mwaka jana,
hakutiliwa shaka hata kidogo kuwa si Padri.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Asenga
alifika kanisani hapo akiwa amevaa mavazi ya kipadri na kujitambulisha
kuwa yupo nchini kwa mapumziko, akitokea nchini Marekani, alikodai ndipo
anakofanyia shughuli zake za upadri katika Jimbo Kuu la New York.
Mbali na kuvalia mavazi ya kipadri,
Asenga pia alionesha kitambulisho na kusababisha uongozi uamini kuwa ni
Padri na kumpa makaribisho ya Padri mwenzao.
“Alipoonesha
kitambulisho tulimwamini na jinsi alivyokuja na mavazi ya upadri na
muonekano wake alionao, haikuwa rahisi kumtilia shaka,” alisema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo alithibitisha kuwa Asenga
aliongoza vyema misa hiyo, kwa kufuata taratibu zote za kanisa hilo
kama zinavyofuatwa na mapadri wengine.
Taratibu Kwa kawaida Misa katika Kanisa
la Katoliki, huanzia Sakestia, sehemu ambayo mapadri na waministranti,
ambao ni wasaidizi wao, huvaa majoho na kusali kabla ya kuingia kanisani
wakisindikizwa na nyimbo. Baada ya kuingia madhabahuni, Padri hubusu
madhabahu kabla ya kualika waumini katika Misa.
Mualiko huo hufuatiwa na maelezo kidogo
na kuanza Ibada ya Kitubio, ambayo waumini hutubu dhambi zao na
kujiweka tayari kusikiliza neno la Mungu. Ibada ya kusomwa neno, kwa
kawaida masomo matatu kutoka vitabu vya Agano la Kale na Jipya katika
kitabu cha Bibilia Takatifu, Padri huanza kutoa mahubiri.
JAMBOLEO
Wakati Serikali ikipambana kutokomeza
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi inasemekana baadhi ya waganga wa
kienyeji wanatajirika kwa kiwango kikubwa na biashara hiyo.
Inadaiwa baadhi ya waganga hao hupata
takribani dola za Marekani 75,000 sawa na zaidi ya milioni 100 kutokana
na biashara hiyo ambayo Rais Kikwete aliikemea vikali kwamba inatia aibu
Taifa.
Hayo yalibainishwa katika ripoti ya
chama cha msalaba mwekundu kuhusu vitendo hivyo vilivyoshamiri hasa
katika ukanda wa Ziwa Victoria.
Ilidai kuwa baadhi ya watu wenye imani
za kishirikina huagiza viungo vya albino kwa ajili ya kutengenezea dawa
ambayo huamini ina nguvu maalumu yenye kuleta bahati nzuri.
Baadhi ya wanasiasa wanadaiwa kuagizwa
na waganga wa kienyeji wasio waaminifu kuwapelekea viungo hivyo ili
nyota zao zing’ae wakati wa uchaguzi.
No comments:
Post a Comment