Pages

March 4, 2015

ASILIMIA 30 YA MAZAO HUPOTEA BAADA YA MAVUNO

Filbert Rweyemamu,Arusha
Wakulima hapa nchini wamenufaika na utafiti wa mpango wa kuwawezesha kufanya ushawishi na utetezi wa sera ili kuleta mabadiliko chanya ambao lengo lake ni kuhakikisha usalama wa chakula kwa kupunguza kiwango cha mazao yanayopotea baada ya  mavuno.

Mradi huo wa miaka miwili uliondeshwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania(Mviwata)ulitekelezwa katika wilaya za Monduli mkoa wa Arusha,Simanjiro mkoa wa Manyara na Hai mkoani Kilimanjaro na uliitimishwa mwishoni mwa wiki wilayani Monduli.

Mmoja wa wakulima kutoka Kijiji cha Enguik Kata ya Monduli Juu wilaya ya Monduli,Lakindi Saluni alisema kupitia mpango wa Sauti ya Wakulima wamejifunza mbinu mbalimbali za ushawishi wa sera na kukabiliana na changamoto katika sekta ya kilimo.

“Wakulima  wadogo tumejifunza mambo mengi yakiwamo kutambua wahusika tunaopaswa kuwaona wakati  tunapokua tukifatilia mambo yanayohusu sekta ya kilimo kwa ujumla ,wakati mwingine pembejeo zinachelewa au makampuni ya mbegu yanatuuzia mbegu zisizo na ubora,”alisema Saluni

Mkulima mwingine kutoka Kata ya Mto wa Mbu,wilaya ya Monduli,Josefa Pius alisema ili kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha chakula cha kutosha serikali haina budi kusimamia ipasavyo pembejeo kuwafikia wakulima kwa wakati ili zilete tija iliyokusudiwa.

Alisema kutokana na mafunzo aliyopata amebaini mbinu sahihi za uvunaji unaopunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa jambo litakalomwongezea kipato katika familia yake.

Akizungumzia mafanikio ya mradi huo,Msimamizi Mkuu wa Mradi,Godfrey Kabuka alisema Umoja wa Ulaya(EU)ulitoa ufadhili katika nchi za Tanzania,Uganda na Kenya ukiwa na lengo la kuwashirikisha wakulima kuibua masuala ya kisera yanayohusu usalama wa chakula.

Alisema mambo yaliyofanyiwa kazi ni Upotevu wa mazao au chakula baada ya mavuno na Mkakati wa kuhifadhi mazao  jambo ambalo limeonekana kuwa ni changamoto katika nchi Afrika Mashariki wakitumia nyenzo ya ushauri elekezi kwa wakulima ambayo imeonyesha mafanikio .

“Hii nyenzo imetuwezesha kufanya mashauriano na wanachama kutambua changamoto na namna ya kuzitatua ambapo wanachama 1,800 katika wilaya hizo walifikiwa na kutoa maswala yanayowatatiza katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula,”alisema Kabuka

Alitaja changamoto hizo kuwa ni Upungufu wa maafisa ugani,ucheleweshaji wa pembejeo,kutokuwepo kwa maghala ya kuhifadhia chakula au kutokuwepo kabisa,ukosefu wa masoko na kukosa elimu ya kuhifadhi mazao.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...