Na Rashid Nchimbi waJeshi la Polisi Arusha
Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Jumanne Muliro
amevitaka vikundi vya ulinzi shirikishi pindi wanapokuwa katika kazi za doria kutowabughudhi
wananchi badala yake wanatakiwa kufanya kazi zao kwa kufuata sheria.
Alisema utendaji bora wa kazi kwa kuzingatia nidhamu na sheria
utaongeza imani kwa wananchi hali ambayo itawafanya wajitolee na kuendelea kuvichangia
vikundi hivyo hatimaye kuboresha maslahi yao wenyewe na vikundi hivyo kwa ujumla
kwa maana ya vifaa.
“Hakuna sheria inayomkataza
mtu yoyote kutembea usiku lakini pia ni jukumu lenu nyinyi askari kumhoji yeyote
mtakayekutana naye usiku kwa kutumia taaluma mlionayo nayo ili kuweza kubaini ukweli”
Alifafanua Mkuu huyo wa Polisi.
Hayo aliyasema wakati wa Uzinduzi wa vikundi viwili vya Ulinzi
Shirikishi uliofanyika juzi katika kata ya Moshono ambapo jumla ya askari 50 wa
vikundi hivyo walihudhuria. Alisema ili kazi zao ziende vizuri na kuendelea kujenga
imani kwa wananchi wanatakiwa wanapoingia kazini wasiwe wamelewa hali ambayo itaendelea
kuleta uelewa na masikilizano baina ya wanaohoji na wanaohojiwa na kuepusha matukio
ya kutojichukulia sheria mkononi.
Aliongeza kwa kusema, kuwepo na kuongezeka kwa vikundi hivyo kutasaidia
kuimarisha ulinzi katika wilaya ya Arusha na kutumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi
pamoja na askari wa vikundi hivyo na pia kutoa wito kwa maeneo mengine kuiga mfano
huo.
“Usalama wa eneo lolote usitegemee askari toka Kituo kikuu
cha Polisi ila kila mtaa unatakiwa uwe na vikundi hivyo kwani eneo lolote ambalo
halina ulinzi linatoa mwanya kwa wahalifu”.Alisema Mkuu huyo wa Polisi.
Alimalizia kwa kuwataka askari wa vikundi hivyo kuratibu maeneo
korofi ili Jeshi la Polisi wilayani hapa liweze kuongeza nguvu katika operesheni
hizo ambazo zitasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Moshono Paulo Mattysen alivipongeza
vikundi hivyo pamoja na viongozi wao na kuahidi kushirikiana nao.
Awali wakitoa elimu kwa vikundi hivyo hivyo Mkuu wa Polisi Jamii
wilaya ya Arusha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Maria Maswa pamoja na Mkaguzi Msaidizi
wa Polisi katika Tarafa ya Suye Frimina Massao waliwaeleza wanavikundi hao umuhimu
wa ulinzi shirikishi na hali hii inatokana na uchache wa askari wa Jeshi la
Polisi na kuwataka wawe na mipaka katika utendaji wao wa kazi.
Wana vikundi hao walitakiwa kuendelea kutoa taarifa za uhalifu
hali ambayo itasaidia kuimarisha ushirikiano baina yao na Jeshi la Polisi na kuwasisitiza
watumie falsafa ya ukamataji salama.
Uzinduzi huo wa vikundi hivyo vilivyopewa majina ya Sekei Moivaro
Polisi Jamii na Mbung’o Moshono kaskazini Polisi Jamii uliambatana na utoaji wa
filimbi,tochi na vitambulisho ambavyo vitasaidia katika utendaji wao wa kazi.
No comments:
Post a Comment