Pages

February 27, 2015

MAGARI YAPOPOLEWA MAWE KATIKA VURUGU ZA MGAMBO NA MACHINGA ARUSHA.

 
Arusha.Mvutano kati ya Mgambo wa Jiji la Arusha na wafanyabiashara ndogondogo umeendelea jana baada ya pande mbili kushambuliana kwa mawe na kusababisha kuvunjwa magari mawili vioo.

Tukio hilo lilitokea Mtaa wa Pangani jirani na Soko Kuu la Arusha,jambo lililozua taharuki ya watu kukimbia ovyo kujihifadhi kwenye maduka yaliyo jirani.

Mmoja wa walioshuhudia tukio hilo,Edward Mollel  mkazi wa Olorien alisema vurugu hizo zilianza baada ya Mgambo wa jiji kukamata Mkokoteni wa mfanyabiashara na kuuweka kwenye gari jambo lililoamusha hasira na kuanza kushambuliana.

"Mgambo wanatembea wakiwa na mawe kwenye gari lao kwaajili ya kujihami na kushambulia wafanyabiashara kwasababu wanafahamu sio jambo rahisi kuwazuia kufanya biashara kwenye eneo hili wakati hawajatenga eneo la kuwaweka,"alisema

Kutokana na vurugu hizo magari mawili yaliyokua yameegeshwa mbele ya Soko Kuu yalivunjwa vioo ambayo  Toyota Escudo yenye namba za usajili T 672 AVB na Toyota Carina yenye namba za usajili T 572 BGR mali ya Gevas Kimario.

Mmoja wa wananchi waliojeruhiwa ambaye baadae alikimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru,Fransis Maganga alisema wakiwa Sokoni hapo alishtuka kubondwa na jiwe kwenye mkono wake wa kushoto kutoka kwenye gari la Mgambo wa Jiji na kumsababishia maumivu makali.

"Nashindwa kuelewa kama wao ni walinzi wa amani au wanavuruga amani,wanapaswa kutimiza wajibu wao bila kubughudhi wananchi wengine,"alisema Maganga

Naye mkazi wa Olorien jijini hapa,Prosper Mfinanga ambaye anajishughulisha na biashara katika Soko Kuu alisema ameshtushwa na Mgambo kujaza mawe kwenye gari lao na kuwashambulia wananchi na kushauri wakati wa utekelezaji wa majukumu yao watumie askari polisi ili kuondoa kasoro zilizojitokeza.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...