Pages

January 2, 2015

Waziri ataka vuguvugu linaloupinga Uislamu Ujerumani lijadiliwe

Waziri wa Maendele wa Ujerumani Gerd Müller ametoa wito wa kuwepo na mjadala wa haki juu ya maandamano yanayofanywa na vuguvugu linalopinga Uislamu - PEGIDA, akihoji kuwa raia wanapaswa kuondolewa hofu.
Waziri wa Maendeleo Gerd Müller alisema katika mahojiano na gazeti la Augsburger Allgemeine toleo la Ijumaa, kuwa wanasiasa wanahitaji kujadili hofu za raia wa Ujerumani kufuatia kumiminika kwa wakimbizi nchini humu.
Mwanasiasa huyo wa chama cha Christian Social Union CSU, alisema licha ya jitihada bora, bado kuna mamilioni ya familia maskini nchini Ujerumani, na kuongeza kuwa wakimbizi wanatizamwa kama tishio, hasa katika miji mikubwa.
"Watu wanateseka, wanahisi kwamba wamesukumwa hadi mwisho na wanaanza kuvutia usikivu kwao, kwa sababu hawajioni wakiwakilishwa kikamilifu", Müller aliliambia gazeti hilo, na kuongeza kuwa viongozi wa Ujerumani wanapaswa kuelekeza usikivu wao kwa masuala hayo.
Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller. Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller.
Maandamano zaidi
PEGIDA, au vuguvugu la Wazalendo wa Ulaya wanaopinga kusilimishwa kwa mataifa ya magharibi, limekuwa likiitisha maandamano ya mara kwa mara katika miji mbalimbali ya Ujerumani tangu mwezi Oktoba, na viongozi wake wanapanga mikutano siku ya Jumatatu mjini Cologne na miji mingine.
Lakini uongozi wa Kanisa la Cologne, ambalo ni moja ya maeneo maarufu zaidi ya utalii nchini Ujerumani, wameamua kuzima taa za nje wakati wa maandamano hayo, hatua iliyosifiwa na mbunge wa CDU Norbert Röttgen aliesema propaganda za PEGIDA zinakwenda kinyume na Ukristu.
Asilimia 13 waunga mkono maandamano
Utafiti uliyofanywa na kampuni ya Forsa kwa ajili ya jarida la Stern la hapa Ujerumani, umeonyesha kuwa asilimia 13 ya Wajerumani wangehudhuria maandamano ya vuguvugu hilo iwapo yatafanyika katika eneo la karibu. Utafiti huo ulibaini pia kuwa asilimia 29 ya raia wanaamini Uislamu umekuwa na ushawishi mkubwa katika maisha ya Ujerumani, na hivyo maandamano hayo yanastahili.
Wakati theluthi mbili ya wale waliohojiwa wanaamini dhana ya kuisilimisha Ujerumani imetiwa chumvi, Wajerumani wengi wana wasiwasi kuhusu idadi ya watafuta hifadhi wanaokimbia nchi zao kama vile Syria.
Siku ya Alhamisi, Kansela Merkel alizusha mjadala mkali nchini Ujerumani kwa ukosoaji wake wa vuguvugu la PEGIDA, alivyowaleza viongozi wake kuwa wanasukumwa na chuki, na kuliita vuguvugu hilo kama linalowalenga watu wa rangi tofauti, na kwamba taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya linapaswa kuwakaribisha watu wanaokimbia migogoro na vita.
Hakuna Shariah barani Ulaya, linasomeka bango hilo la waandamanaji wa Pegida. Hakuna Shariah barani Ulaya, linasomeka bango hilo la waandamanaji wa Pegida mjini Dresden.
CSU yanyooshewa kidole
Alex Gauland, kiongozi wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha Alternative für Deutschland AfD, alikosoa matamshi hayo ya Kasela, akisema alikuwa anaelemea watu ambao hawajui. Chama cha mrengo wa shoto cha Die Linke na watetezi wa mazingira Die Grün, wamesema CSU ambacho ni sehemu ya muungano unaotawala, inawajibika kwa kuongeza umaarufu wa PEGIDA.
CSU, ambayo ndiyo inatawala katika jimbo la kusini la Bavaria, imelaumiwa pia kwa kuchochea chuki dhidi ya wageni. Zaidi ya maombi 200,000 ya hifadhi yaliwasilishwa kwa ajili ya kuidhinishwa nchini Ujerumani mwaka uliyopita, na kuifanya kuwa nchi yenye idadi kubwa zaidi ya maombi ya hifadhi duniani.
DW


No comments:

Post a Comment