Rais Jakaya Mrisho
Kikwete akiwa na Rais Salva Kiir Mayardiy wa Sudan ya Kusini (kushoto), Makamu
wa Rais wa zamani wa Sudan Dkt Riek Machar Teny (wa pili kulia) na Bw. Deng
Alor Kuol wakitia saini mkatana wa makubaliano ya kukiunganisha upya
chama cha SPLM chaSudani Kusini katika hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Jumatano Januari 21, 2015 usiku. Nyuma yao ni mjane wa marehemu John
Garang aliyekuwa Mwenyekiti wa SPLM Mama Rebecca Nyandeng de Mabior na Afisa wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bw. Thobias Makoba.
Nyuma yao wakishuhudia utiaji saini huo ni Makamu wwa Rais Dkt Mohamed Ghalib
Bilali, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
akifurahia wakati Rais Salva Kiir
Mayardiy wa Sudan ya Kusini (kushoto) na Makamu wa Rais wa zamani wa Sudan Dkt
Riek Machar Teny (wa pili kulia) wakipeana mikono na kubadilishana nyaraka
baada ya kutia saini mkatana wa
makubaliano ya kukiunganisha upya chama cha SPLM cha Sudani Kusini
katika hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha Jumatano Januari 21, 2015 usiku.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na
Bw Deng Alor Kuol wakifurahia wakati
Rais Salva Kiir Mayardiy wa Sudan ya Kusini (kushoto) na Makamu wa Rais
wa zamani wa Sudan Dkt Riek Machar Teny (wa pili kulia) wakipeana mikono na
kubadilishana nyaraka baada ya kutia saini mkatana wa makubaliano ya kukiunganisha upya chama cha
SPLM cha Sudani Kusini katika hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha Jumatano Januari
21, 2015 usiku.
**********
MKATABA
wa kujenga tena umoja na kukiunganisha upya Chama Tawala cha Sudan
Kusini cha Sudan People’s Liberation Movement (SPLM)
ulitiwa saini usiku wa jana, Jumatano, Januari 21, 2015, katika sherehe ya
kufana iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Ngurdoto, Wilaya ya
Arumeru, Mkoa wa Arusha.
Mkataba
huo unaojulikana kama Agreement on the Re-unification of Sudan
People’s Liberation Movement umepongezwa kuwa ni hatua muhimu katika
kulitoa taifa changa la Sudan Kusini katika hali ya machafuko, vita vya wenyewe
kwa wenyewe, kutoelewana na kutoaminiana, mambo ambayo yameligubika taifa hilo
tokea mwishoni mwa 2013 wakati kutokuelewana kulipozuka ndani ya SPLM na
hatimaye katika Serikali ya nchi hiyo.
Viongozi
waliotia saini ni Mheshimiwa Salva Kiir Mayardit, Rais wa Sudan Kusini ambaye
pia ni Mwenyekiti wa SPLM na anayeongoza kundi linalojulikana kama
SPLM in Government (SPLM-IG), Mheshimiwa
Dkt. Riek Machar ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa SPLM na pia
aliyekuwa Makamu
wa Rais wa Sudan Kusini anayeongoza kundi la SPLM in Opposition (SPLM-IO)
na Dkt. Deng Alor Kuol ambaye anaongoza kundi la SPLM Leaders- Former
Detainees (SPLM Leaders – FD).
Sherehe
hiyo ilishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho
ndicho kimesimamia mazungumzo yaliyozaa Mkataba huo. Rais Kikwete pia ndiye
mdhamini mkuu wa Mkataba huo.
Wengine
walioshuhudia tukio hilo muhimu ni Rais wa Uganda, Mheshimiwa Jenerali Yoweri
Kaguta Museveni; Rais Uhuru Muigai Kenyatta wa Kenya; Naibu wa Rais wa
Jamhuri ya
Afrika Kusini Mheshimiwa Cyril Ramaphosa, Makamu Mwenyekiti wa zamani wa CCM
Mheshimiwa John Samwel Malecela ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa mazungumzo
yaliyozaa Mkataba huo na Katibu Mkuu wa CCM Mheshimiwa Abdulrahman Kinana
ambaye alikuwa mwezeshaji wa mazungumzo.
Mazungumzo
yaliyozaa Mkataba huo yalianza mwishoni mwa mwaka jana baada ya Rais Kikwete na
Chama cha CCM kuombwa na Rais Kiir Mayardit kukubali chama hicho tawala cha
Tanzania kutumia uzoefu na ujuzi wake wa miaka mingi wa uongozi na siasa
kujaribu kuleta suluhu ndani ya SPLM.
Mazungumzo
hayo ya kutafuta suluhu ambayo yamefanyika kwa awamu mbili, ya kwanza yakiwa
yamefanyika Oktoba mwaka jana na pili yakiwa yameanza mwanzoni mwa mwezi huu,
Januari 2015, yameongeza thamani kwenye
mazungumzo mengine yanayofanyika Addis Ababa, Ethiopia chini ya usimamizi wa
taasisi ya IGAD na yanayojadili jinsi ya kurejesha amani nchini
humo.
Viongozi
wa SPLM wanaamini kuwa kwa sababu mgogoro wa kisiasa nchini mwao ulianzia ndani
ya chama hicho na kwa sababu SPLM ndicho chombo pekee ambacho kinawaunganisha
wananchi wote wa Sudan Kusini, basi busara inaelekeza kuwa suluhu
ianze kutafutwa
ndani ya chama hicho.
Mkataba
wa jana, kimsingi, unalenga kuweka mazingira ya kujenga utulivu,
maelewano, amani
na umoja wa kudumu ndani ya chama hicho na nchini humo kwa kuhakikisha kuwa
utekelezaji wa mambo ya msingi yaliyokubaliwa kuhusu shughuli za siasa, uongozi
na oganisheni ya chama hicho yanafanyika bila
kukawia.
Mkataba
huo pia unalenga kuhakikisha kuwa chama cha SPLM kinabuni na kutekeleza sera za
kuondokana na ukabila, makundi yenye mitazamo finyu na mwenendo wa kijeshi
katika siasa za Sudan Kusini.
Aidha,
Mkataba huo unalenga kuhakikisha kuwa chama cha SPLM kinafanya mageuzi ya
kuanza kujenga utamaduni wa kuvumiliana na ujenzi wa misingi ya
demokrasia.
Mkataba
huo pia unataka watu wote ambao walishiriki katika mauaji na umwagaji damu
katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wasiruhusiwe kugombea wala kushika nafasi
ya uongozi wa umma ndani ya chama hicho.
Pia
viongozi wote wa Sudan Kusini wanatakiwa, chini ya Mkataba huo, kuwaomba radhi
wananchi wa nchi hiyo ya Sudan Kusini kwa kuruhusu nchi hiyo kuingia katika
machafuko ya umwagaji damu mkubwa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu
– Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment