Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu
vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan akionyesha gazeti la
"Tuwasiliane" linalochapishwa na UTPC na kusambazwa kwa wadau na maeneo
mbalimbali ya jijini Mwanza kwa Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa
Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
nchini, Alvaro Rodriguez aliyetembelea makao ya ofisi hizo kwa ajili
ya mazungumzo na kuboresha ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa Umoja
huo wa vilabu vya waandishi wa habari nchini.
Na Mwandishi Wetu
WIMBI kubwa la kuwa na vijana wasiokuwa
na kazi limeelezwa kuwa tatizo duniani kote na serikali mbalimbali
zinatakiwa kuliangalia hilo kwa undani na kulitatua.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Mkazi
wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa shirika la
maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez.
Mratibu huyo alisema hayo katika
mazungumzo yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi
wa Habari (UTPC) Abubakar Karsan.
Alisema ukosefu wa kazi kwa sasa ni
tatizo la kijamii na kwamba, shauri hilo lisipoangaliwa kwa makini
linaweza kuwa chanzo cha matatizo makubwa ya usalama na amani katika
taifa.
Alvaro Rodriguez ambaye alifika katika
ofisi za UTPC kuangalia mambo yanayofanyika katika ofisi hiyo wakati
akiwa ziarani Mwanza wiki iliyopita, alisema kama tatizo la ajira
litaendelea kuwapo, vijana wanaoathirika wanaweza kufikiria njia
nyingine isiyo ya kistaarabu kufanikisha mambo yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu
vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan akizungumza na Mratibu
Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kushoto)
aliyeambatana na Mshauri wa masuala ya haki za binadamu kutoka ofisi ya
mratibu mkazi wa UN Tanzania, Bi. Chitra Massey (kulia) alipotembelea
makao makuu ya ofisi hizo jijini Mwanza.
Alisema Umoja wa Mataifa unaendelea
kushirikiana na serikali mbalimbali kuhakikisha kwamba tatizo la ajira
kwa vijana linamalizwa ili jamii isiingie katika mtafaruku
utakaokosesha amani na usalama na hivyo kusimamisha maendeleo
yaliyofikiwa katika jamii.
Bila kutaja makundi ya kigaidi
yanayotikisa dunia kwa sasa kama Al - Qaeda na washirika wake Boko
Haram, Al - Shabab, Islamic State of Iraq na Levant (ISIL) alisema
makundi mengi ya kigaidi duniani yanatokana na vijana kutojua wafanye
nini na mazingira waliyonayo na hivyo kuwa rahisi kushawishika.
Alisema makundi ya hatari mara nyingi ni
ya vijana ambao wanashindwa kupata riziki au hawajui wafanye nini kupata
riziki na serikali zimewaacha bila kuwaangalia.
Aidha alisema Umoja wa Mataifa utaendelea
kusaidia kuhakikisha kwamba masuala muhimu yanayowezesha maendeleo kama
demokrasia yanazingatiwa ili kuiwezesha jamii kufanya maamuzi sahihi ya
vile wanavyotaka kupanga maendeleo yao.
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa
Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu (kulia) akichangia jambo
wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya
Waandishi wa Habari (UTPC) Abubakar Karsan makao makuu ya ofisi za umoja
huo jijini Mwanza.
Alisema Demokrasia huwezesha wananchi
kujua namna wanavyoweza kutengeneza mustakabali wao katika masuala ya
ustawi wa jamii na maendeleo huku haki zao za msingi zikilindwa.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Bw.
Karsan alimwambia mratibu huyo mambo ambayo yamefanywa na umoja huo na
changamoto walizokumbana nazo kwa kuzingatia mpango mkakati wake wa
mwaka 2011-2013.
Umoja huo ambao ulianzishwa mwaka 1996 na
kusajili na wizara ya mambo ya ndani kama taasisi isiyokuwa ya
kiserikali (NGO) mwaka uliofuata, umefanikiwa kuanzisha mfuko wa
kusaidia vyombo vya habari kwa jina la Daudi Mwangosi, aliyekuwa
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari wa Iringa (IPC).
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa
Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa
Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan wakati
wa mazungumzo ya kuboresha mahusiano baina ya mashirika ya umoja wa
mataifa na umoja wa vilabu vya waandishi wa habari nchini Tanzania.
Aidha alimwambia kwamba wamefanikisha
mafunzo ya kuongeza umahiri wa uandishi wa habari na pia kuwaelezea
umma juu ya uhuru wa vyombo vya habari.
Pia alielezea mafanikio yaliyopatikana
katika kampeni za kuelimisha umma na kuelewana miongoni mwa wadau
mbalimbali wa sekta ya habari.
Alisema hata hivyo bado wanaendelea na
kampeni yao kutaka mabadiliko ya malipo kwa waandishi wa habari
wanaojitegemea ambao ndio wanatoa mchango wa asilimia 75 hadi 80 za
habari zinazotangazwa au kuchapishwa.
Aidha wanaendelea kutoa mafunzo ya kanuni
na maadili kwa waandishi wa habari na kuendelea kukabiliana na tatizo
la usalama katika mpango mkakati wa mwaka 2015 – 2019.
Katika ziara hiyo ya kanda ya Ziwa,
mratibu huyo aliambatana na mshauri mwandamizi wa masuala ya haki za
binadamu Dk Chitralekha Massey na Mtaalamu wa mawasiliano wa umoja huo
hapa nchini HoyceTemu.
No comments:
Post a Comment