Pages

January 13, 2015

HAUSIGELI ASAKWA WIZI WA MTOTO



 
RPC Mara akiwa na mtoto aliyeibiwa(kushoto) ni mama wa mtoto huyo.
MFANYAKAZI wa ndani anayefahamika kwa jina la Paulina Sobe anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa mtoto wa bosi wake, Diana Meshack, mwenye umri wa miaka miwili, huko Musoma mkoani Mara, tukio lililotokea Januari 3 mwaka huu.Kamanda wa Jeshi hilo mkoani Mara, ACP Philip Kalangi, aliliambia gazeti hili kuwa kwa kushirikiana na askari wa Kanda Maalum ya Kipolisi Tarime/Rorya,wamefanikiwa kuwakamata watu wawili walioshirikiana na hausigeli huyo kumuiba mtoto.

ILIKUWAJE?

Chanzo kilicho karibu na familia hiyo kinasema kuwa Januari 3 mwaka huu, msichana huyo wa kazi alionekana na majirani akiondoka na mtoto huyo na kwenda naye kusikojulikana na tokea wakati huo hakuonekana tena.

HALAFU?

Lakini mara tu baada ya kuondoka nyumbani hapo, mama wa mtoto huyo, Gadioza Meshack alipokea simu kutoka kwa watu wasiojulikana, waliomtaka kuwapa shilingi milioni 3 ili wamrudishe binti yake, vinginevyo wangeenda kumuuza kwa watu wanaonunua watoto.

 
Kamanda wa Jeshi mkoa wa Mara, ACP Philip Kalangi.

ASHINDWA, ALIFIKISHA POLISI

Kamanda Kalangi alisema baada ya mama huyo kulifikisha suala hilo Polisi, wao kwa kushirikiana na kampuni za mitandao ya simu, walianzisha msako wa kuwasaka watu hao na kufanikiwa kuwanasa Januari 7 mwaka huu katika kijiji cha Kitamwi, kilichopo mpakani mwa nchi jirani ya Kenya.

“Tulifanikiwa kuwakamata Vicent Magesa (19) na Erick Range, wote wakazi wa Getabwaga nchini Kenya, wakiwa na mtoto huyo ambaye pia tulimkuta akiwa salama,” alisema Kamanda Kalangi.

MAMA AELEZA ILIVYOKUWA

Akisimulia mkasa wa kuibwa kwa mtoto wake, Gadioza Meshack alisema Januari 3 mwaka huu, kabla ya kwenda kazini kwake,alimuacha mtoto akiwa na mfanyakazi huyo aliyempa shilingi 15,000 ya kulipa bili ya maziwa na 10,000  ya matumizi.

“Nalishukuru Jeshi la Polisi kwa kufanya jitihada za kupatikana kwa mtoto wangu licha ya kwamba yule mfanyakazi aliyeondoka naye hajapatikana, ila naamini kutokana na kazi kubwa iliyofanywa ya kumpata mtoto hata yeye atapatikana,” alisema mama huyo.

Aliwataka wazazi kuwa makini na watu wanao wachukua kwa lengo la kulea watoto kwani wengine sio wazuri na baadhi hubadilika kwa kushawishiwa.
CHANZO: GAZETI LA UWAZI

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...