Pages

January 10, 2015

TAMKO LA POLISI KUHUSU ZOEZI LA KUAPISHWA SERIKALI ZA MITAA

Advera-Senso
Kufuatia kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji na hivi sasa kuendelea kwa zoezi la kuapishwa kwa viongozi hao katika maeneo mbalimbali hapa nchini, kumejitokeza tabia ya baadhi ya wananchi kufanya vurugu na fujo katika zoezi hilo.Baadhi ya wananchi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kihalifu kwa kufanya fujo na vitendo vya vurugu ikiwemo kuwapiga baadhi ya watendaji wanaosimamia zoezi la kuapisha na kuwapiga viongozi wateule waliochaguliwa kihalali na wananchi kwa madai kuwa hawakushinda kihalali katika uchaguzi huo jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi.Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini, linatoa onyo kwa wananchi wenye tabia hiyo kuacha
mara moja na badala yake kama mtu hakuridhika na matokeo ya uchaguzi huo, afuate utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yake kwenye ngazi husika ili yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.Aidha, Jeshi la Polisi linawata Wakurugenzi na Maafisa watendaji wenye dhamana ya kusimamia mchakato wa kuwaapisha wenyeviti waliochaguliwa, kufuatilia kwa karibu migogoro inayojitokeza na kuitatua migogoro hiyo mapema ili kuepusha migongano inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu ama kikundi chochote kitakachofanya vurugu ama fujo kwa kisingizio cha ushabiki wa siasa na badala yake atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Imetolewa na:
Advera J. Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

No comments:

Post a Comment