Pages

January 9, 2015

POROJO ZA ANKO KIDEVU JUU YA IDARA YA HABARI MAELEZO

WASOMAJI na wadau wangu nawasalimu na naimani kuwa Mwenyezi Mungu ametujalia tumeuona mwaka mpya wa 2015 salama salmini. Nawatakia heri na fanaka katika mwaka huu pia na karibuni tena katika porojo zangu za ukweli.
IDARA ya Habari –MAELEZO ndiyo idara ya serikali inayoshughulika na kufanya kazi zake kama chombo cha usimamizi wa vyombo vya habari na waandishi wake.
Idara hiyo pia ndio msemaji wa masuala mbalimbali ya serikali lakini pia ndiyo idara yenye jukumu la kusajili au hata kuyafutia usajili magazeti hapa nchini na vyombo mbali mbali vya hjabari.
Waandishi wa habari waajiriwa na wale wa kujitegemea wameanza mchakato wa kujaza fomu kwaajili ya kupatiwa vitambulisho vipya vya kazi (PRESS CARD) kwa mwaka 2015.
Jambo hili ni zuri kwa waandishi wa habari maana kitambulisho hicho cha serikali hutolewa kwa waandishi walio na sifa za uandishi tu na sio wale waparamia fani za watu maarufu kama kanjanja.
Ndio! Uandishi wa habari ni taaluma kama taaluma nyingine, kwa hiyo kila mwanahabari anatakiwa kuwa na Press Card ambacho ndicho kitambulisho cha serikali, kama huna basi wewe sio muandishi au laa hujakomaa kuwa muandishi. 
Nakama umekomaa lakini sifa za kupata 'Leseni ya Uandishi' huna basi tambua fika fani ya uandishi wa habari haikufai na unatakiwa kwenda kwenye fani nyingine, na hii uiache maana utaleta usumbufu tu mitaani.
Vigezo vya kupewa Press Card kwa mwandishi wa habari ni lazima awe na kiwango cha elimu ya ngazi ya Stashahada na uzoefu katika kazi hiyo.
Bila mwandishi wa habari kuwa na kitambulisho kinachotambuliwa na Serikali, mwandishi huyo anakuwa hatambuliki vyema na huenda katika ofisi nyingine asipate huduma (taarifa) anazohitaji.
Bunge linataraji kuanza vikao vyake Januari 27 mwaka huu, lakini waandishi wa habari wasio na Press Card hawata ruhusiwa kuripoti tukio lolote katika Bunge hilo mjini Dodoma.
Hili ni agizo lililotangazwa kwa wanahabari tangu mwaka jana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Assa Mwambene.
Ingawa utaratibu wa press card umekuwepo kwa miaka, hapakuwa na shuruti kwa waandishi wa maswala muhimu kama bunge kuwa nayo ilimradi tu watambulike na wawe na barua kutoka vyombo vyao.
Hili naliunga mkono, maana pasipo tumika vitambulisho hivyo itakuwa ni shida kufuatia wingi wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii iliyopo nchini kwa sasa.
Leo porojo zangu nazipiga katika huu mtindo wa namna utaratibu unaoutumika wa utoaji huo wa vitambulisho ambapo kila mwaka waandishi wanatakiwa kujaza fomu maalum za maombi na kulipia.
Idara hii nyeti ya kuisemea serikali  inapaswa kuendana na mfumo wa Sayansi na teknolojia hasa mfumo wa kidijitali wa utunzaji wa taarifa za kila mwandishi tofauti na ilivyo sasa. 
Hivi kuna haja gani mimi nipo katika tasnia hii huu mwaka wa 14 sasa kila wakati naleta picha 3, nakala ya vyeti vyangu vya kitaaluma na kujaza fomu tatu za maombi hayo ya kitambulisho? 
Mfumo wa Dijitali kama ungekuwa unatumika MAELEZO, chini ya Mkurugenzi wake Kijana, Assa Mwambene, ungeweza kabisa kuweka taarifa zetu waandishi katika mtandao na wao kuzitumia kuhakiki waombaji wa vitambulisho hivyo.
Ni makaratasi kiasi gani watakuwa wakiyapokea mwaka hadi mwaka kutokana na utoaji wa vitambulisho hivyo.
Pia suala lingine ambalo mimi naliona ni kikwazo na hata waandishi wengine wamekuwa wakilizungumzia ni haja ya kutoa vitambulisho hivyo kila mwaka. 
Kwanini MAELEZO wasitoe vitambulisho vya walau miaka mitatu au hata mitano kwa waandishi hawa ambao wameridhia wanavigezo na sifa za kufanya kazi hiyo?
Endapo mwandishi atakiuka utaratibu wa kazi idara hii ya habari Maelezo inauwezo wa kumpoka kitambusho hicho mwandishi husika kama ambavyo Polisi usalama barabarani wanaweza kufanya kwa dereva anaekiuka sheria na kusababisha ajali.
Tunajua kuwa Press Card kutolewa kila mwaka ni moja ya mradi maana waandishi wanatozwa fedha, ili kuongeza mapato ya idara husika na serikali kwa ujumla, lakini wanaweza kutoza malipo ya miaka 3 hadi mitano basi lakini waandishi wakaondokana na kero ya kujaza fomu kila mwaka na kusubiri kwa muda mrefu kupata vitambulisho  hivyo.
Aidha fomu basi zingeweza kuanza kutolewa tangu mwezi Novemba ili ifikapo Desemba vitambulisho vipya viwe  vimeshatoka kulingana na kumalizika kwa muda wa matumizi ya kitambulisho cha mwaka uliopita.
Lakini haya mnatengeneza vya mwaka mmoja moja lakini vipi ubora wake nao, kitambulisho kinapendeza sana siku unakabidhiwa lakini ikishapita wiki moja ile nembo ya taifa ya bibi na bwana inafutika.
Ni vyema sasa wanaosimamia ubora wa vitambulisho hivyo wakaangalia malighafi inayoweza kudumu kwa kipindi cha mwaka mzima na kubaki na alama zote zinazotakiwa kuwepo. 
Pia kutoa vitambulisho hivyo kwa wakati ili kuepusha usumbufu unaoweza kuwakumba waandishi ambao kwa sasa wanatumia vitambulisho vilivyopita mudawake.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...