Malecela na Riek Machar.
UONGOZI wa ngazi ya juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umetinga katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro ndani ya chama cha SPLM kinachotawala Sudan Kusini.
Ujumbe huo unaoongozwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana.
Kwa upande wa SPLM, mazungumzo hayo yanaongozwa na Taban Deng Gai, Daniel Awet Akot na Deng Alor Kuol. Mkutano huo ambao umeingia awamu ya pili unakutanisha makundi matatu yanayopingana ndani ya chama cha SPLM.
Miongoni mwa makundi hayo ni kutoka chama cha SPLM, kundi kutoka kwa wafungwa wa kisiasa pamoja na kundi lililojitenga kutoka chama cha SPLM.
Mkutano huo wa usuluhishi pia unahudhuriwa na mjane na kiongozi wa kwanza wa chama cha SPLM, John Garang ambaye aliongoza mapambano ya kupigania uhuru hadi kupatikana na ambaye alifariki katika ajali ya helikopta.
Akifungua mazungumzo hayo ya siku tano, Kinana alisema mkutano huo ni muhimu katika kuleta utengamano na amani ndani ya nchi ya Sudan Kusini.
Kinana alisema mkutano huu una lengo la kusimamia mazungumzo ya kuunganisha umoja ndani ya chama cha SPLM ambacho kwa sasa kimemeguka mapande matatu na makundi yote matatu yalishiriki mazungumzo hayo yaliyofanyika Desemba 15, mwaka jana.
Kumeguka katika makundi hayo matatu na kusababisha jeshi kwa upande wake kumeguka katika makundi hayo na kusababisha wananchi nao kugawanyika katika makundi hayo matatu.
Kutokana na tofauti zao hizo kati ya watu 10,000 na 20,000 wameuawa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka tangu chama hicho kumeguka katika vipande hivyo vitatu.
Alisemaa watu zaidi ya milioni moja hawana mahala pa kuishi tangu mifarakano hiyo itokee mwaka 2013. Hivyo, alisema mazungumzo hayo ni muhimu katika kufikia amani ili waweze kukiunganisha tena chama chao cha SPLM ili kuleta umoja, mshikamano ndani ya chama hicho, Serikali na ndani yaJeshi.
Alisema wakati wa mazungumzo hayo ya Arusha, CCM itatoa uzoefu wa jinsi Tanzania ilivyoshiriki katika kusimamia vyama vya ukombozi katika nchi za kusini mwa Afrika.
Alisema mazungumzo ya kuleta umoja ndani ya chama cha SPLM yalianza Arusha Oktoba mwaka jana mazungumzo yanayolenga kuleta amani, utulivu na umojandani ya chama cha SPLM.
Alisisitiza kwamba umoja, utengamano, utulivu na amani ni mambo ya msingi katika taifa la Sudan Kusini nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta barani afrika.
Hivyo Kinana alisema CCM inatoa mwito kwa makundi hayo matatu yanayopingana na kupigana katika nchi hiyo kumaliza tofauti zao haraka ili wananchi wa Sudan Kusini waishi kwa amani na utulivu.
Kwa upande wake, Malecela akizungumza kabla ya ufunguzi wa mkutano huo wa siku tano alisema tofauti zilizojitokeza ndani ya chama hicho hakuna mtu mwingine wa kumaliza, bali ni wananchi na wanachama SPLM na Sudan Kusini wenyewe.
Malecela, ambaye ndiye aliyepewa jukumu la kusimamia mazungumzo haya na CCM, amezitaka pande zote tatu zinazopingana kutumia busara na hekima kumaliza tofauti hizo ili wananchi wa Sudan Kusini wasiendelee kuteseka na pia kupoteza maisha.
Mazungumzo hayo pia yanahudhuriwa na wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, Norway, Misri, Umoja wa Mataifa na Ethiopia.HABARILEO
No comments:
Post a Comment