Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
UTEKELEZAJI wa shinikizo la kuvuliwa
madaraka kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
linaloendelea kutolewa na wabunge na baadhi ya wanasiasa kwa Rais Jakaya
Kikwete, huenda ukaacha masononeko kwa wananchi walionufaika na kipindi
kifupi cha uongozi wa waziri huyo.
Profesa Muhongo
aliyejitengenezea uadui kwa wafanyabiashara na wanasiasa, kutokana na
misimamo yake ya kulinda maslahi ya umma na kuzungumza ukweli, huku
akijiamini kulikotafsiriwa kuwa ni dharau, hatima ya uongozi wake ipo
mikononi mwa Rais Kikwete, ambaye ameshauriwa na Bunge kutengua uteuzi
wake.
Katika azimio la saba, kati ya maazimio manane ya Bunge la
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lililomalizika mwishoni mwa mwezi
uliopita, kuhusu utoaji wa fedha katika akauti ya Tegeta Escrow,
iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mamlaka ya uteuzi wa
Profesa Muhongo, imeshauriwa kutengua uteuzi huo.
“Bunge
linashauri na kuazimia Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu, Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, wawajibishwe na mamlaka ya uteuzi itengue uteuzi
wao,” limeeleza azimio hilo la saba.
Usambazaji umeme
Kama
Rais Kikwete atatekeleza ushauri huo wa Bunge na shinikizo la wanasiasa
na wafanyabiashara, uongozi wa muda mfupi wa Profesa Muhongo takribani
miaka miwili, utakumbukwa kwa umahiri wa kusambaza umeme vijijini.
Kabla
ya kuteuliwa kwa Profesa Muhongo, Watanzania asilimia 14 tu ndio
waliokuwa wakitumia nishati ya umeme, kati yao asilimia 12 walikuwa
watumiaji wa mijini na asilimia mbili tu, ndio walikuwa watumiaji wa
vijijini.
Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, kati ya mwaka 2007
na mwaka 2010, kulikuwa na ongezeko la asilimia nne tu la watumiaji wa
umeme, hali iliyoonesha kuwa ongezeko la Watanzania waliokuwa wakipata
umeme, lilikuwa asilimia moja kwa mwaka.
Lakini baada ya
kuteuliwa kwa Profesa Muhongo katika nafasi hiyo, katika muda mfupi wa
uongozi wake, idadi ya Watanzania wanaotumia umeme iliongezeka na
kufikia asilimia 36 katikati ya mwaka huu.
Kwa hatua hiyo,
uongozi wa Profesa Muhongo ulivuka malengo ya Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), ambayo ndio msingi wa utekelezaji wa malengo ya
Serikali, iliyotaka Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2015, asilimia 30
ya Watanzania wawe wanapata umeme.
Baada ya kupita malengo ya
Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Profesa Muhongo aliamua kuweka malengo mapya,
ambapo alitarajia ifikapo 2015, asilimia 45 mpaka 50 ya Watanzania wawe
na fursa ya kutumia umeme.
Miongoni mwa Watanzania wanaokiri
hilo ni Diwani wa Kata ya Manga wilayani Tarime, Omolo Ochola ambaye pia
ni mchimbaji mdogo wa madini kutoka Rorya.
Ochola alipozungumza
na gazeti hili wiki hii, alisema Waziri Muhongo amefanya kazi kubwa,
amesambaza umeme vijiji vingi hapa nchini na kudhibiti ubadhirifu
uliokuwepo hapo awali.
Mbali na Ochola, Mbunge wa Ntera,
Livingston Lusinde (CCM), alisema yeye hawezi kuona aibu kuzungumzia
mafanikio ya uongozi wa Profesa Muhongo, huku akitoa mfano wa Tanesco
kupigia simu wateja ili ikawaunganishie umeme, kuwa haikuwahi kutokea
kabla ya uongozi wake.
Bei ya uunganishaji
Katika
kutimiza malengo hayo, uongozi wa Profesa Muhongo, ulitangaza punguzo la
gharama za kuunganisha umeme majumbani kutoka Sh 177,000 za awali hadi
Sh 27,000 vijijini.
Awali, punguzo hilo lilitolewa kwa mikoa ya
Lindi na Mtwara, ambako bomba la kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam
limeanzia na limepita, lakini baada ya muda gharama hizo zilishushwa kwa
vijiji vyote nchi nzima.
Profesa Muhongo mwenyewe alisema
gharama hizo zitahusu miradi inayosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini
(REA), katika kipindi ambacho wakandarasi watakuwa wakiendelea na awamu
ya pili ya miradi iiliyoanza Machi mwaka huu na kutarajiwa kukamilika
kati kati ya mwakani.
Profesa Muhongo alisema kuwa katika awamu
ya kwanza ya miradi iliyomalizika Desemba mwaka jana, wanavijiji
walilipa gharama kubwa, hivyo uongozi wake uliamua kupunguza malipo
hayo, ili huduma hiyo ya nishati iwafikie watu wengi zaidi.
Kufuta mgawo
Kuhusu suala la mgawo wa umeme, Profesa Muhongo mwaka 2012 alisema mgao wa umeme hautakuwepo tena na haukubaliki kamwe.
Profesa
Muhongo alisema hadi Juni 2012 uwezo wa mitambo ya kufua umeme
(installed capacity) ulikua megawati 1,375.74 (gesi asilia ikiwa ni
asilimia 40, maji asilimia 41 na mafuta asilimia 19).
Alifafanua
kuwa uwezo huo, ulikuwa ni ongezeko la megawati 367 sawa na asilimia 36
ikilinganishwa na uwezo wa megawati 1,013.74 uliokuwepo Juni, 2011.
Alisema
mahitaji ya juu ya umeme kwa mwaka 2011/12 yalifikia wastani wa MW
820.35 ikilinganishwa na MW 730 kwa mwaka 2010/11. Tangu wakati huo,
hakujatokea mgawo mkali wa umeme kama uliotokea mwanzoni mwa mwaka 2011,
na miaka ya nyuma ya hapo.
Tanzania kabla ya uongozi wa Profesa
Muhongo, ilikuwa ikikabiliwa na mgawo wa umeme wa mara kwa mara, ambao
mbali na kuathiri maisha ya watu wa kawaida kutokana na kusababisha
mfumko wa bei, pia uliathiri sekta ya viwanda ambapo baadhi vilitishia
kufunga.
Kutokana na mgawo wa mara kwa mara, mwanzoni mwa mwaka
2011, Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), liliwahi kutoa taarifa
ya kutishia kufungwa kwa viwanda 50 kati ya 280, huku vingine
vikitishia kupunguza uzalishaji, kutokana na makali ya mgawo wa umeme.
Wamiliki
hao walidai kupitia CTI kwamba, hawana uwezo wa kutumia jenereta kwa
ajili ya shughuli za uzalishaji viwandani, kwa vile umeme wa jenereta
utawalazimu kulipia gharama za matumizi ya nishati hiyo maradufu,
tofauti na ile inayozalishwa na Shirika la Umeme (Tanesco).
Walitoa
mfano kuwa wakitumia umeme wa Tanesco kwa kila kilowati moja, wanalipia
senti za dola ya Marekani nane mpaka tisa, lakini wakitumia umeme wa
jenereta, kwa kila kilowati moja, wanatumia senti za dola ya Marekani 18
mpaka 20.
Mbali na hao, CTI ilieleza pia kuwa asilimia 15 ya
wanachama walitishia kuongeza bei ya kuuzia bidhaa wanazozalisha na
athari yake kwa mapana, ilielezwa kuwa viwanda vitakosa mapato, ajira
kwa watumishi wa viwandani zitapotea na Serikali pia itakosa mapato
yanayotokana na kodi za viwanda.
Aidha Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS), ilieleza kuwa mfumko wa bei ulipanda na kufikia asilimia 6.4
kutoka asilimia 5.6, sababu kubwa ikiwa ni mgawo wa umeme.
Ofisi
hiyo ilitoa mfano wa bei ya vyakula na vinywaji baridi, kwamba ilipanda
kutoka asilimia 2.9 na kufikia asilimia 6.7 kutokana na mgawo wa umeme.
Kushusha bei ya umeme Baada ya kufanikiwa kufuta mgao wa umeme,
kusambaza umeme kwa wananchi na kuunganisha umeme kwa wananchi kwa
gharama nafuu, mwanzoni mwa mwaka huu, Profesa Muhongo, alitangaza
kusudio lake la kushusha bei ya umeme.
Diwani Ochola wa Manga wilayani Tarime, alisema Profesa Muhongo alikuwa amejiandaa kushusha zaidi gharama za umeme mwakani.
Naye
Musa Onyango, mchimbaji mdogo kutoka Rorya, alisema gharama za umeme
zilikuwa zikipanda kila mwaka na kuwakatisha tama Watanzania
ikilinganishwa na kipindi cha mwaka mmoja wa Profesa Muhongo ambapo
kumekuwa na ahueni kubwa ikilinganishwa na wakati wa viongozi
waliotangulia Kusudio hilo la kushusha bei, lilitarajiwa kuanza
kuonekana mara bomba la gesi kufika jijini Dar es Salaam na mitambo ya
umeme kuanza kutumia gesi badala ya mafuta mazito.
Uongozi wa
Profesa Muhongo, uliweka wazi kuwa wafanyabiashara wanaouzia umeme
Tanesco, wanauza uniti moja kwa kati ya Dola ya Marekani senti 33 na 50.
Bei hiyo ya umeme kwa Tanesco kwa mujibu wa takwimu za
Serikali, ni kubwa kuliko bei ya umeme ambayo shirika hilo linauza kwa
Watanzania wanaotumia umeme mdogo wa majumbani, umeme wa kati kwa
wafanyabiashara, umeme wa kati wa viwandani na umeme mkubwa kwa viwanda
vikubwa, na kubwa kuliko bei ya umeme ya mashirika ya umeme ya nchi za
Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Takwimu za Tanesco, wateja wa
majumbani, uniti moja ya umeme wanauziwa kwa dola ya Marekani senti 19,
wateja wa biashara senti 13 na viwanda vya kati na vikubwa senti 10.
Umeme
wa taa za barabarani ni senti 19, wakati Tanesco inanunua kwa senti 33
na 50. Profesa Muhongo alisema bei ya umeme iliyopo, ni kwa muda tu na
itashuka sana bomba la gesi likikamilika, kwa sababu hata mitambo ya
kufua umeme inayotumia mafuta nayo, itatumia gesi na mitambo mipya ya
gesi italetwa.
Alisema Serikali inataka umeme mwingi utokane na
gesi, jua, upepo na joto ardhi, lakini wapo wanaokataa bomba lisije Dar
es Salaam na nyuma yao, wapo wafanyabiashara ambao wanahofia kuwa mwisho
wa biashara yao ya kuuzia Tanesco umeme kwa bei ya juu umefika.
Msimamo
huo wa Profesa Muhongo, uliwahi kuungwa mkono na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, aliyesema mwishoni mwa Januari mwaka huu alipokuwa Mtwara, kuwa
Serikali imedhamiria kuachana na umeme huo wa mafuta na kama
wafanyabiashara hao watataka kuendelea na biashara hiyo, ni vyema
wabadilishe mitambo yao iwe ya gesi na sio ya mafuta kama ilivyo sasa
hivi.
Wataalamu wa gesi
Kutokana na ugunduzi mkubwa
wa gesi uliofanyika nchini, Profesa Muhongo pia alianzisha utaratibu wa
kusomesha Watanzania wengi zaidi katika vyuo vya nje ya nchi katika
masuala ya gesi na mafuta, ili wananchi wasimamie rasilimali hiyo kwa
manufaa ya taifa lao na vizazi vyao.
Lengo la Profesa Muhongo
katika hilo, ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya kwanza yenye
wataalamu wengi wa mafuta na gesi, katika nchi za bara la Afrika, baada
ya miaka mitano ijayo kwa kuwa na wataalamu zaidi ya 300 watakaokuwa
wamesomea masuala hayo nje ya nchi.
Pia amefanya juhudi
kushawishi watanzania ambao ni wataalamu mafuta na gesi zaidi ya 10
wanaofanya kazi nje ya nchi hususani nchini Canada na Uingereza, mpaka
wakakubali kurejea kufanya kazi hizo nchini.
Utata wa kumwajibisha
Hatua
ya Bunge kutaka Profesa Muhongo awajibishwe, imetokana na maoni ya
Mwenyekiti wa Bunge wa Kamati ya Fedha za Serikali (PAC), Kabwe Zitto,
kuwa fedha hizo Sh bilioni 321 ni za umma na utoaji wake na kwamba hatua
ya kulipwa kwa kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL),
iligubikwa na harufu ya ufisadi.
Hata hivyo, Profesa Muhongo
katika utetezi wake, alisema wakati wa kufunga akaunti hiyo kulikuwa na
Sh bilioni 182.77 tu, wakati deni baada ya kupiga hesabu, lilikuwa Sh
bilioni 275.20 na zote ni fedha za IPTL, zilizotokana na mauzo ya umeme
wake katika Shirika la Umeme (Tanesco), na hivyo bado kampuni hiyo
inaidai shirika hilo la umeme Sh bilioni 123.90.
Mbali na
kueleza kuwa kampuni hiyo ya IPTL bado inaidai Tanesco, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Frederick Werema, ambaye naye anatakiwa kuondolewa,
alisisitiza kuwa akaunti ya Escrow haikatwi kodi, ila kodi hiyo hukatwa
kwa mpokeaji wa fedha hizo na kutaka Mamlaka ya Mapato (TRA), kwenda
kudai kodi yake kwa IPTL.
Profesa Muhongo na Werema mpaka sasa
msimamo wao ni kwamba fedha hizo si za umma, huku Profesa Muhongo
akisisitiza kuwa mbali na kuwa si za umma, pia Serikali bado inadaiwa Sh
bilioni 123.90.
Lakini hata taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), hajathibitisha kuwa fedha hizo ni za umma,
bali ilieleza kuwa kuna uwezekano kuwa katika fedha hizo, kuna fedha za
Tanesco, fedha za Serikali kwa maana ya kodi na fedha za IPTL, ambazo
ni mauzo ya umeme kwa Tanesco.HABARILEO
No comments:
Post a Comment