Baadhi
ya Washirika wa Maendeleo wakipita jirani na unapojengwa mmoja wa
mitambo wa kupokea gesi katika eneo la Kinyerezi, Jijini Dar es Salaam,
walipotembelea maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kupokea gesi.
Pichani
ni mmoja wa Mtambo wa kuzalisha umeme ambao ni miongoni mwa mitambo
itakayotumiwa katika kuzalisha kiasi cha megawati 150 za umeme katika
Mradi wa Kinyerezi I.
Meneja
Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha kuzalisha Umeme cha Kinyerezi I kutoka
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi, Saimoni akiuleza jambo
ujumbe wa Washirika wa Maendeleo wakati walipotembelea kuona maendeleo
wa ujenzi wa mradi huo.
Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi, akiwaongoza Washirika
wa Maendelo kuangalia namna utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi wa Kituo cha
Kuzalisha Umeme na kituo cha kupokea Gesi unavyoendelea katika eneo la
Kinyerezi Jijini Dar es Salaam. Pembeni ni mojawapo ya mapipa
yatakayotumika kuhifadhi mafuta ambayo yatatumika wakati wa dharura.
Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Washirika
wa Maendeleo kutoka taasisi mbalimbali nchini waliotembelea Mradi wa
kuzalisha Umeme wa Kinyerezi I na kituo cha kupokea Gesi wameeleza
kufurahishwa na kuridhika na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo.
Mkurugenzi
Mkaazi wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Tanzania, Uganda na
Burundi, Philippe Dongier, akiongea kwa niaba ya washirika hao ameeleza
kuwa, wameridhishwa na hatua ambazo miradi hiyo imefikia na kupongeza
jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba inafanyia kazi changamoto ya
upatikanaji umeme wa uhakika Tanzania. Pia Dongier ameitaka Serikali
kushirikiana na wadau katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya umeme ili
iweze kufikia lengo lake la kuhakikisha Tanzania inazalisha umeme wa
kiasi cha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza
wakati ujumbe huo ulipotembelea kituo cha kuzalisha umeme wa kiasi cha
megawati 150 na kituo cha kupokea gesi katika eneo la Kinyerezi jijini
Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
ameeleza kuwa, Wizara imeona ni jambo la msingi kwa wadau hao
kutembelea miradi hiyo ili kujionea hatua mbalimbali ambayo miradi hiyo
imefikia.
Aidha,
Maswi ameongeza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini,
imedhamiria kuleta mabadiliko ya kiuchumi kupitia sekta ya nishati
hususani kupitia gesi asilia na kuongeza kuwa, hakuna kinachoshindikana
hivyo, miradi hiyo inatarajiwa kukamilishwa kwa wakati kama
ilivyopangwa.
Kwa
mujibu wa Meneja Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Shirika la
maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Musomba, ameeleza
kuwa, ujenzi wa kituo cha kupokea gesi cha Dar es Salaam umekamilika
kwa asilimia 60. Naye Meneja Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha kuzalisha
Umeme cha Kinyerezi I kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
Mhandisi,
Saimoni Jilima ameeleza kuwa, ujenzi wa kituo hicho umekamilika kwa asilimia 70.
Washirika
wa Maendeleo waliotembelea miradi hiyo ni pamoja na Benki ya Dunia,
GIZ, USAID, MCC, Korea Exim Bank, Benki ya Maendeleo ya
Afrika(ADB),DFID, Umoja wa Ulaya,Ubalozi wa Sweden, Ubalozi wa Norway,
Ubalozi wa Ujerumani na Ubalozi wa Ufaransa.
No comments:
Post a Comment