Arusha. Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zinatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam kujadili mikakati ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa bei nafuu kupitia nishati mbadala.
Mkutano huo ulioandaliwa na EAC kwa kushirikiana na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), utafanyika Oktoba 31hadi Novemba Mosi, mwaka huu ambapo wafanyabiashara wa nishati mbadala watapata fursa ya kuonyesha huduma na bidhaa zao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa EABC, Jonne Bruecher aliwambia waandishi wa habari jijini Arusha jana kuwa mkutano huo utahudhuriwa na watu zaidi 200 wakiwemo viongozi wa Serikali, Wataalamu, Wafanyabiashara na wadau wa sekta ya nishati mbadala.
“Nishati ya uhakika na nafuu ni nyenzo muhimu katika juhudi za nchi wanachama wa EAC kujikwamua kiuchumi. Lazima pawepo mbinu na mikakati ya pamoja katika upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala kwenye Ukanda huu wa EAC,” alisema Bruecher ambaye ni Meneja maendeleo ya biashara wa EACB.
Utafiti wa EABC kuhusu matumizi ya nishati kwa nchi za EAC inaonyesha kuwa Kenya na Rwanda ndizo zinaongoza kwa kusambaza umeme kwa asilima 28 ya wananchi wake, Tanzania ni ya tatu kwa asilimia 19, Uganda asilimia 16 wakati Burundi ni asilimia nne pekee.
Kwa upande wake, Mshauri wa Sera na Utafiti wa EABC, Michael Baingana alisema matumizi ya nishati mbadala utaongeza kiwango cha matumizi ya nishati ya umeme kwa wananchi wa EAC, hasa vijijini ambao ni asilimia 80 ya raia wote wa EAC wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 140 milioni.
“Hadi sasa ni asilimia ndogo tu ya wakazi wa EAC wenye kufikiwa na huduma ya nishati ya umeme, nah ii ni moja kati ya changamoto zinazotukabili katika harakati za kujiletea maendeleo,” alisema Baingana.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa EABC, Andrew Luzze alisema ni muda muafaka kwa nchi za EAC kutumia fursa ya upatikanaji wa jua na upepe wa ukakika kuzalisha umeme mbadala badala ya kuendelea kutegemea vyanzo vingine kama maji, mafuta na gesi ambavyo ni ghali.
Luzze alisema matumizi ya nishati mbadala siyo tu itawahakikishia raia wa EAC uhakika wa umeme, bali pia utapunguza bei ya bidhaa na huduma kutokana na gharama nafuu ya uzalishaji.
No comments:
Post a Comment