Pages

August 26, 2014

UGONJWA WA EBOLA WAPITENA TENA HODI DRC CONGO.


 
SERIKALI ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imebaini kuwepo kwa mlipuko wa maradhi ya homa kali maeneo ya Kaskazini mwa nchi hiyo, ambayo sasa imethibitika kuwa ni ugonjwa wa ebola. 

Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Dk Felix Numbi, aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jana, kwamba watu wawili wamepimwa na kugundulika wanaumwa ebola, maradhi ambayo hadi sasa yameshaua watu 13 katika jimbo la Equateur.

Lakini, maradhi hayo yako maeneo ya vijijini na imeelezwa kuwa ebola hiyo, ni tofauti na ile inayosumbua nchi za Afrika Magharibi. Shirika la Afya Duniani (WHO) limekiri kuwa mlipuko wa ebola kwa sasa hautarajiwi kuwa na kasi kubwa katika nchi za Afrika Magharibi, ambako tayari watu 2,615 wameshakumbwa na maradhi hayo tangu ulipuke Machi mwaka huu.

Hadi sasa maradhi hayo hayana tiba, lakini baadhi ya wagonjwa wamepona baada ya kupewa dawa aina ya ZMapp, ambayo bado iko kwenye majaribio.

Hata hivyo, dawa hizo zimemalizika na hazipo tena. Dk Numbi alisema watatangaza karantini ya watu kuingia na kutoka katika mji wa Boende, ambako wagonjwa wa homa hiyo wamegundulika.

Mji huo upo kilometa 100 kutoka jiji la Kinshasa. Alisema kuibuka tena kwa mlipuko huo, kumesababisha idadi ya milipuko ya homa ya ebola kufikia saba tangu 1976 mgonjwa wa kwanza alipogundulika karibu na Mto Ebola.

Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu tishio la ugonjwa huo katika nchi jirani na Tanzania, Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii anayeshughulikia Dharura na Maafa, Dk Elias Kwesi, alisema Serikali imeendelea kuimarisha ulinzi na usalama mipakani na katika viwanja vya ndege.

Dk Kwesi alisema ulinzi huo, umeenda sambamba na upimaji wa afya za watu wanaoingia nchini, ili kukabiliana na ugonjwa huo. Alisema mpaka sasa hakuna taarifa rasmi kutoka WHO za kuwepo kwa ugonjwa huo nchini Kongo.

Dk Kwesi alisema mpaka sasa tayari wameshafunga vifaa vya kisasa katika viwanja vyote vya ndege.

Mpango uliopo ni kufunga vifaa vingine katika mipaka yote na tayari utekelezaji wa mpango huo, umeshaanza katika mpaka wa Namanga.

Kwa mujibu wa Dk Kwesi, wiki hii wanatarajia vifaa vingine vya upimaji kuwasili na vitasambazwa katika mipaka ya Holili, Sirari na Mtukula.

Lengo ni kuhakikisha mipaka yote imefungwa vifaa hivyo, ili watu wanaoingia kupitia mipaka hiyo, wapimwe afya zao kwanza.

Alisema tayari wameshatoa mafunzo kwa wataalamu wa afya wa mikoa mbalimbali, ikiwemo mikoa ya pembezoni ambayo nao wanatakiwa kufundisha wahudumu wa afya na jamii dalili za ugonjwa huo na namna ya kukabiliana nao. Dalili zake ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuuma kichwa na vidonda kooni.

Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa damu ndani na nje mwilini. Muda wa kuonekana kwa dalili za ugonjwa huo ni kati ya siku mbili hadi 21 baada ya kupata maambukizi.

“Ugonjwa wa ebola unaambukiza kwa kasi na unaenea kati ya mtu na mtu kwa kugusa damu na majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo, kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo na kugusa wanyama walioambukizwa mizoga na wazima kama vile sokwe na swala wa msituni,” imeeleza taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa hivi karibuni.

Katika hatua nyingine, baada ya ugonjwa huo kuua madaktari na wataalamu wa maabara, Taasisi ya Kupambana na Magonjwa Ambukizi Kusini mwa Jangwa la Sahara (SACIDS), imeamua kutoa mafunzo kwa wataalamu hao, ili kusaidia waepukane na hatari ya kuambukizwa magonjwa hayo.

Wataalamu na wanafunzi hao 45 kutoka katika ukanda huo, ikiwemo, Kenya, Uganda, Kongo DRC, Zambia, Msumbiji, Afrika Kusini na mwenyeji Tanzania, walikutana mkoani Morogoro kujadili umuhimu wa kuongeza usalama katika kuhifadhi sampuli za ugonjwa huo ili zisisambae.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Profesa Mark Rweyemamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), alisema wameamua kuchukua wataalamu na wanafunzi kutoka katika nchi hizo, ili wapate elimu ya jinsi ya kujikinga, ikiwa kutatokea mlipuko wowote wa ugonjwa huo.

Alisema kuwa asilimia 20 ya watu katoka katika ukanda huo, hufariki dunia kwa magonjwa ya kuambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa bindamu.

Mhadhiri wa SUA, Esron Karimuribo, alisema Bara la Afrika limekuwa likikumbwa na magonjwa mengi ambukizi, ikiwemo ebola na magonjwa mengine yanayofanana na hayo.

Alisema kuwa ushirikiano kati ya sekta ya afya na mifugo, ni muhimu kwa kuwa magonjwa mengi yanayowapata binadamu yanatokana na mifugo.

Mkuu wa Idara ya Maikrobayolojia na Parasitolijia katika Kitivo cha Mifugo cha SUA, Gerald Misinzo, alitoa mfano wa homa ya bonde la ufa, kuwa huathiri wanyama na binadamu.

Mkurugenzi wa Sayansi ya Uhai Tanzania, Flora Ismail, alisema bioteknolojia inatoa suluhu kinzani za magonjwa, ikiwa ni pamoja na kuzalisha chanjo ya magonjwa mbali mbali yanayosababishwa na wanyama na katika kilimo wamepata suluhu kwa kuchagua mbegu bora. 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...