Pages

August 17, 2014

GARI LA HOSPITALI YA MUHIMBILI ILIYOKUWA IMEBEBA MAITI 10 KUPATA AJALI BAADA YA KUGONGA WAENDESHA PIKIPIKI KUFARIKI DUNIA MOROGORO.


Polisi wa Usalama Barabarani akikagua gari lililokuwa limebeba maiti 10 kutoka Dar es Salaam kwenda Ifakara baada ya kupata ajali eneo la Mikese katika barabara ya Dar es Salaam-Morogoro kisha kuwagonga waendesha pikipiki wawili na kufariki dunia papo hapo mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda

Morogoro.
Gari la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), lililokuwa likisafirisha maiti 10 za watu kwenda katika Hospitali ya Mtakatifu Francis Ifakara, wilayani Kilombero, limewagonga watu wawili waliofariki dunia papohapo, eneo la Mtego wa Simba, Mikese mkoani Morogoro.

Waliokufa katika ajali hiyo iliyotokea saa 5:25 asubuhi jana ni dereva na abiria wa bodaboda.

Maiti hizo zilizokuwa zimehifadhiwa katika mifuko maalumu ya plastiki, zinaelezwa kuwa zilikuwa zikipelekwa katika Hospitali ya Mtakatifu Francis, ili zitumike kwa mafunzo.

Akizungumzia ajali hiyo katika eneo la tukio, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro, Boniface Mbao alisema kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Pankrasi Pascal, mkazi wa Ifakara, wilayani Kilombero.

Mbao aliwataja waliokufa kuwa ni Shaaban Rajabu na Ally Benulo, wakazi wa Kijiji cha Mikese, waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki.

Tukio hilo limekuja siku kadhaa baada ya mabaki ya miili ya binadamu kugunduliwa ikiwa imetupwa katika dampo moja lililoko Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Chuo kimoja cha mafunzo ya udaktari wa magonjwa ya binadamu, kilihusishwa na tukio hilo lililozua hofu kwa wakazi wengi wa jiji hilo.

Kamanda Mbao alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa gari ambaye kwa sasa, anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.

Kuhusu maiti 10 zilizokutwa kwenye gari hilo, ofisa huyo wa polisi alisema wanafanya mawasiliano ili kupata usafiri wa kuzifikisha katika Hospitali ya Mtakatifu Francis, ilipokusudiwa.

Mashuhuda wa ajali hiyo walisema chanzo ni mwendokasi wa dereva wa gari, huku wakilalamikia kukithiri kwa ajali katika eneo hilo.

Walisema ajali hizo zimekuwa zikisababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia na kwamba kuna haja Serikali kuweka matuta na vibao vya kuashiria kona zilizopo eneo hilo.Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...