Uonevu! Rapa mwenye ‘swagger’ za Ja-Rule
Bongo, Rashid Makwilo ‘Chid Benz’, anadaiwa kukwaa kisanga kingine
kibaya baada ya kukurupuka kutoka nyumbani kwake na kwenda kumvamia staa
mwenzake, Rehema Chalamila ‘Ray C’ nyumbani kwake anapoishi na
kumtwanga makonde ikiwa ni siku chache tangu jamaa huyo apate msala
mwigine wa aina hiyo.
TUJIUNGE NYUMBANI KWA RAY C
Ilidaiwa kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa
kuamkia Alhamisi iliyopita nyumbani kwa Ray C, Changanyikeni jijini Dar
es Salaam ambapo ilisemekana kwamba Chid Benz alimvamia mishale ya saa
4:00 usiku kwa gia ya kumsaka mzazi mwenzake aliyemtaja kwa jina moja la
Mariam.
CHID BENZ ATAKA KUMUONA MWANAYE
Ilidaiwa kwamba Chid Benz alisema kuwa
alizungumza na mpenziye huyo kwamba alitaka kwenda kumuona mwanaye
ambapo Mariam alimjibu kwamba kwa muda huo alikuwa nyumbani kwa Ray C
Changanyikeni.
UNGA WATAJWA
Sosi wetu alidai kwamba baada ya
kujibiwa hivyo, Chid Benz alianza kulalama na kumwambia anamfuata
palepale kwa nini usiku ule alale kwa Ray C, wakati ana uwezo wa kwenda
nyumbani au amekwenda kwa staa huyo ili kunywa dawa zao za kuondoa sumu
ya madawa ya kulevya ‘unga’, jambo ambalo jamaa huyo siku zote huwa
hataki hata kulisikia masikioni mwake.
Staa wa muziki wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’.
CHID BENZ AWAVAMIA
“Huwezi kuamini baada ya muda kama wa saa
moja, Ray C na Mariam wakiwa ndani wakitazama TV, ghafla mlango
ulisukumwa kwa nguvu kisha akaingia Chid Benz na kumdaka Mariam na
kuanza kumshushia kipigo.“Yaani huo mshtuko walioupata walidhani
wamevamiwa na Al-Shabaab.
KIBAO CHAMGEUKIA RAY C
“Mungu mkubwa kwa sababu Mariam alifanikiwa kuchoropoka na kukimbilia chumbani ndipo kibao kikamgeukia Ray C.
Sehemu ya damu chumbani kwa Ray C kutokana na kipigo cha Chidi Benz..
“Ray C akiwa anashangaa ghafla naye alipokea kipigo kikali kutoka kwa Chid na kumsababishia majeraha mbalimbali mwilini.
RAY C AKIMBILIA KWA MAJIRANI
“Baada ya kuona maji yanazidi unga,
Ray C alitafuta upenyo na kukimbilia kwa majirani huku akipiga kelele za
kuvamiwa, mara moja majirani waliambatana naye mpaka nyumbani kwake.
“Walipofika Chid Benz alikuwa
ametumia staili za kininja kwa kuruka geti na kutokomea kusikojulikana
huku akiwaacha Ray C na Mariam wakiangua vilio kwa kipigo kikali
walichopokea.
RAY C AVUJA DAMU
“Ray C aliumia mkono na mguu ambao
ulionekana ukivuja damu. Mariam alikuwa akililia mbavu zake kuchakazwa
kwa makonde mazito na upande mwingine baadhi ya vyombo vya ndani
vikionekana kuvunjwa na vingine kusambaratishwa kufuatia tafrani
iliyozuka muda mfupi baada ya Chid Benz kutia maguu nyumbani hapo,”
chanzo kilishusha madai hayo mazito.
RAY C ATIRIRIKA SAKATA LILIVYOKUWA
Akizungumzia na gazeti hili Alhamisi
iliyopita juu ya sakata hilo, Ray C alisimulia mkasa mzima: “Kweli Chid
Benz alikuja nyumbani kwangu na kunivamia.
“Alinipiga vibaya sana na kuvunja
baadhi ya vitu vya ndani kwangu, jambo ambalo lilinishangaza zaidi ni
namna alivyopafahamu nyumbani kwangu hadi kuja kunifanyia fujo nikiwa na
mzazi mwenzake, Mariam ambaye nilitoka naye ofisini kwangu.
“Ujue jana (Jumatano) tulikuwa na
kazi sana ofisini kwangu mimi na Mariam, sasa kutokana na kubanwa na
kazi kweli muda ulienda sana hivyo nikamwambia Mariam akalale kwangu.
“Kwa kuwa muda ule ilikuwa ngumu kwenda kwao Mbezi Beach, Mariam alikubali na tulikwenda wote nyumbani kwangu.
“Huko nyuma Mariam alikuwa
mwathirika wa madawa ya kulevya lakini baada ya kusikia mimi nimeacha,
naye aliachana nayo na kuanza kutumia dawa za kuondoa sumu.
“Tumeendelea kutumia naye dawa na
sasa ameshapona kabisa hivyo kuna baadhi ya kazi nimekuwa
nikimshirikisha kunisaidia kwenye ofisi yangu. Pia alishawahi
kumshawishi Chid Benz ili aje kutumia dawa lakini jamaa alikataa na
kumfanyia vurugu sana huku akimkataza kuwa na mimi kwa madai mimi ndiyo
namfanya amwambie kuachana na utumiaji dawa za kulevya.
“Sasa jana alipojua hivyo nadhani Chid Benz alikuja kutimiza dhamira yake ambayo siku nyingi alikuwa akiahidi kunipiga.”
SOO LIPO POLISI
Ray C alisema baada ya tukio hilo
alikwenda kuripoti kwenye Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Kinondoni na
kufunguliwa jalada la kesi ambapo Chid Benz anasakwa na polisi.
Juhudi za kumpata Chid Benz
hazikuzaa matunda kwani simu yake haikuwa hewani hivyo jitihada
zinaendelea na kama ana ufafanuzi au utetezi anaweza kutupigia.
CHID BENZ NI TATIZO?
Chid Benz anadaiwa kuwa ni tatizo
kwani tukio hilo la Ray C amelifanya wakati akiwa na tukio la pili kwa
wanawake kwani kwenye Mahakama ya Mwanzo, Ilala ana kesi mbichi
aliyoshitakiwa kwa kosa la kumpiga mrembo aitwaye Mwanaisha.
Mbali matukio hayo pia Chid Benz ana rekodi ya kukorofishana na wasanii wenzake kama Kalapina na marehemu Ngwea.
No comments:
Post a Comment