Pages

July 9, 2014

KISA CHA CHADEMA KUPONZWA NA UKAWA CHATAJWA.

http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/04/ukawa6.jpg
IMEBAINIKA kwamba msukosuko unaotokea katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) unatokana na hasira za serikali kushindwa kushawishi chama hicho na vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kurejea kwenye Bunge la Katiba mwezi ujao.

Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali zinasema kuwa hata mgogoro kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na CHADEMA una msukumo wa serikali, ili kudhoofisha chama kikuu cha upinzani kabla ya kuendea vingine kabla ya Agosti, mwaka huu.

Serikali imekuwa inashinikiza kila taasisi itoe kauli dhidi ya msimamo wa UKAWA kutorejea bungeni, lakini nguvu kubwa imeelekezwa kwa CHADEMA kwa kuwa ndicho kinaonekana kuongoza UKAWA, na kwamba hicho kikiyumba, vingine vitayumba na kuingiliwa kirahisi.

Baadhi ya makada wa CCM ambao hawakubaliani na msimamo wa chama chao kuhusu rasimu ya pili ya katiba, waliliambia gazeti hili kwamba hata suala la mgogoro unaoibuka kati ya CHADEMA na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ni wa kutengenezwa ili kudhoofisha chama hicho.

Akizungumza kwa kujiamini, na akikubali kunukuliwa bila kutajwa jina, kada huyo alisema:

“Unajua, serikali imeshindwa kushawishi wapinzani wakubaliane na msimamo wetu kuhusu rasimu. Mara kadhaa umesikia viongozi wa upinzani wakitoa matamko kwamba hawatarejea kwenye Bunge la katiba, la sharti lao ni moja, kwamba ili warejee lazima mjadala ujikite katika rasimu iliyoletwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Sasa ukichunguza, utaona kwamba kweli wapinzani wana hoja, lakini sisi chama chetu kimeamua kufuata kauli ya mwenyekiti, kwamba serikali tatu haziwezekani, zitavunja Muungano, ingawa si wote tunakubaliana naye katika hilo.

“Lakini woga wa kumpinga mwenyekiti ndiyo umetufikisha hapo, maana hata sisi tusiokubaliana naye tunalazimika kunyamaza tu.

“Sasa bwana mkubwa ameona atumie viongozi wa dini na watu wenye sauti katika jamii, ili kusukuma hoja hii, na ndiyo maana unasikia baadhi ya viongozi wa dini wanasema UKAWA warejee bungeni bila masharti.

“Hata ofisi ya msajili imeshinikizwa, kwamba kwa kuwa CHADEMA ndicho kinaongoza UKAWA, kikishatetereshwa, uongozi uka-panic kwa sababu ya presha ya migogoro, hawatakuwa na uwezo wa kusimamia UKAWA, na wakishalegea hao, itakuwa rahisi kushughulika na wenzao CUF na NCCR-Mageuzi.”

Alisema ofisi ya msajili inajua fika kwamba Katiba ya CHADEMA haina matatizo, lakini kwa kuwa wapo wanachama waliofukuzwa ambao walilivalia njuga suala hilo, na kwa kuwa chama kipo katika uchaguzi wa ndani, na kwa kujua nafasi ya viongozi wakuu wa chama katika mchakato huo, serikali iliona ijaribu hata mbinu hiyo.

Hata hivyo, mbinu hiyo imeshindwa kuitikisa CHADEMA kwa kuwa kimeonyesha kumbukumbu za maelezo kuhusu hoja husika, na viongozi hawajishughulishi na propaganda hizo, bali wanaendelea na kazi zao.

Katika wiki moja iliyopita, vyombo vya habari vimekuwa vinaripoti habari kutokana na matamko kutoka kwa watu na taasisi kadhaa nchini yanayowataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kurejea bungeni bila masharti ili kuhakikisha katiba mpya inapatikana.

Waziri Mkuu alitoa kauli yenye kuonyesha kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa utategemea uwapo wa katiba mpya. Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu Jaji Mark Bomani alizugumza na vyombo vya habari akisema ni vema wajumbe wajikite kwenye masuala mengine kwanza badala ya kubishania hoja ya muungano na muundo wake.

Mara mbili ndani ya wiki moja, viongozi waandamizi wa Kanisa Katoliki wametoa kauli za kuwataka wajumbe hao warudi bungeni bila masharti.

Tamko la hivi karibuni ni lile la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), lililotolewa juzi na Rais wake, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa.

Katika tamko hilo, waliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wawe wamoja na kufanya kazi yao kwa mtazamo usioegemea siasa za vyama.

Waliwakumbusha wajumbe hao kuwa yeyote anayedharau hitaji la katiba mpya ama anayejaribu kupuuza na kuweka kando rasimu ya pili, huyo si mwakilishi wa utashi wa watu, na kwamba mwisho wake historia itamhukumu.

“Kwa moyo wa sala na tafakari makini, tulifuatilia mlivyojadiliana katika Bunge la Katiba kuanzia Februari hadi Aprili 2014. Katika siku 67 ninyi wateule wa rais mpatao 600, mlijadiliana pasipo umoja, mkishambuliana kwa kauli kali kati yenu, mkikashifiana pasipo udhibiti wa uongozi mliojichagulia wenyewe kwa kanuni na sheria mlizojitungia,” lilisomeka tamko hilo.

Kwa mujibu wa TEC, mwenendo huo ulikuwa wa kusikitisha na kuchukiza katika mahali pale panapoheshimika. Kwamba, kanisa lilitegemea majadiliano katika kuheshimiana hoja za kizalendo na kiungwana zitokanazo na mambo ya masuala makuu yaliyopendekezwa katika rasimu ya pili ya katiba.

“Badala yake, tulijionea mabishano makali na mpasuko uliosababisha upotoshaji wa nia iliyokusudiwa. Hatimaye hila na gilba zikateka kabisa jukumu adili la Bunge la Katiba.

“Tukumbuke Rais Jakaya Kikwete kwa uthubutu na ujasiri wa kipekee, alianzisha mchakato wa kuunda katiba mpya, na kisha aliridhia kwa kuipokea kwa furaha rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” lilisomeka tamko hilo.

Kwamba, ni lazima kujiuliza ni nini kilitokea hadi kugeuza kabisa mwelekeo mzima wa mchakato wa katiba kwa kuikejeli na kuishutumu vikali rasimu hiyo katika wakati wa kipekee kabisa wa kihistoria wa uzinduzi wa Bunge Maalumu. Hata kusahau gharama kubwa ambayo ilibebwa na walipa kodi.

“Na sasa hali hii inaonyesha dhahiri jambo hili limeiingiza nchi katika mgogoro mkubwa unaoashiria hatari mbeleni,” walisema maaskofu hao.

Maaskofu waonywa kuhusu UKAWA

Hata hivyo, Mwinjilisti Medard Kyabashasa wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), wa Mbagala, Dar es Salaam, amekerwa na matamko ya viongozi wa dini dhidi ya UKAWA, bila kujali sababu iliyowafanya kususia Bunge, na bila kumkemea Rais Jakaya Kikwete aliyesababisha mzozo huo.

Kwa mujibu wa Mwinjilisti huyo, msimamo wa UKAWA ni kusimamia maoni ya wananchi, wakiwemo maaskofu wenyewe. Hivyo, kilichowatoa bungeni ni kutetea maoni ya wananchi yanaachwa, ambayo watawala wanataka yapuuzwe, tume itukanwe na kuacha watu wakileta mawazo yao ya mifukoni.

Kutokana na hali hiyo, Kyabashasa amewataka viongozi wa dini wawe wawazi, waache unafiki wa kupamba jambo ovu.

“Viongozi wa dini waache unafiki, kama wanadhamiria kweli kusaidia katiba ipatikane, lazima wawakemee wabunge wa CCM na mwenyekiti wao kwa kuvuruga mchakato na kung’ang’ania kujadili vitu ambavyo havimo katika rasimu ya pili na ambavyo vipo kinyume cha sheria,” alisema Kyabashasa.

Aliongeza kuwa viongozi wote wa dini wanajua wazi kuwa aliyevuruga mchakato wa katiba mpya ni Rais Jakaya Kikwete. Badala ya maaskofu na viongozi wengine wa dini kumkemea moja kwa moja, wamekuwa wakifumbafumba halafu wanalaumu UKAWA na kuanza kuwasihi warejee bungeni.

Alihoji kuwa maaskofu wanapowaomba UKAWA kurejea bungeni, kinachoenda kujadiliwa baada ya UKAWA kukubali wito wao ni nini? Je, ni rasimu ya pili yenye maoni ya wananchi kama ilivyoandikwa na Tume ya Jaji Warioba au kwenda kujadili msimamo wa CCM unaolazimisha maoni ambayo hayapo kwenye rasimu?

“Tuliona UKAWA walitumia kila njia kuhakikisha maoni ya wananchi yanajadiliwa ikashindikana na baada ya hapo, wakaamua kutoka kama njia ya kuonyesha shinikizo kwa wajumbe wenzao kurejea katika mstari wa kujadili rasimu halali iliyopitishwa kisheria,” alisema.

Mwinjilisti huyo akitoa mifano kutoka katika Biblia, aliwataka maaskofu na viongozi wengine watakaotoa matamko, kuiga mfano wa Yohana Mbatizaji, alivyomwambia Herode waziwazi kuwa kuchukua mke wa ndugu yake lilikuwa kosa.

“Mungu ametupa akili na uelewa, tusifanye mambo kwa makusudi halafu tunaanza kutegemea maombi, ni kama vile tunaona mtu anatunywesha sumu kwa makusudi, halafu tunakazana kuomba Mungu sumu isituue,” alisema mwinjilisti huyo.

Aliwataka viongozi wa dini wailamu CCM wazi wazi, waeleze kosa la CCM na Kikwete waziwazi, ndipo wapate ujasiri wa kuwasihi UKAWA kurejea bungeni wakakae wajadili rasimu ya pili ya katiba.

“Viongozi wa dini wawaambie viongozi wa CCM kuwa wanavuruga nchi kwa makusudi kwa jeuri ya wingi wao bungeni, jeuri ya fedha na dola, hadi kulazimisha mambo ambayo yapo kinyume cha maoni ya wananchi,” alisema.

CCM hawakuwa na nia ya dhati ya kuleta katiba mpya, walijua mchakato ukianza ni wapi wataivuruga, hivyo wa kulaumiwa ni wao, ndio maana wanatamba kwamba mchakato ukikwama turejee kwenye katiba ya zamani.

“Viongozi wa dini tuna nafasi kubwa sana ya kuirejesha serikali kwenye mstari kama Bunge limeshindwa. Tuikemee serikali waziwazi inapokwenda kinyume, tumechoshwa na wizi, leo unasikia Escrow, leo rushwa, lakini viongozi tunapotoa matamko tunaogopa kuiambia CCM kuwa imefanya hayo, tumebaki tunaomba kusali ili amani iliyopo iendelee…, iendelee ili waendelee kuiba, kula rushwa na kufanya ujangili?” alihoji.

Tangu UKAWA waamue kutoka bungeni Aprili 16 mwaka huu, kumekuwa kukitolewa matamko na watu pamoja na taasisi mbalimbali za kidini, huku mengi yakiishia kuwasihi UKAWA kurejea bungeni bila kuangalia kiini kilichowafanya watoke.TANZANIA DAIMA.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...