Pages

May 30, 2014

Majaji EACJ waruhusu Spika Eala kung’olewa


Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Dk Magreth Zziwa.PICHA|MAKTABA 
Na Peter Saramba, Mwananchi

Arusha. Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Dk Magreth Zziwa amekalia kuti kavu kutokana na uwezekano wa kung’olewa madarakani baada ya Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), kuruhusu bunge hilo kuendelea na shughuli zake kulingana na kanuni na taratibu zake.
Jopo la majaji watatu wa EACJ, wakiongozwa na Jaji Mfawidhi Jean-Bosco Butasi lilitupilia mbali maombi ya zuio la muda kuhusu Kanuni za Bunge zinazohusu suala la kumwondoa madarakani spika lililowasilishwa na Taasisi ya Mbidde Foundation Ltd ya nchini Uganda na Spika Zziwa mwenyewe.
Wabunge wa Eala wanataka kumng’oa Spika Zziwa kwa madai ya kupendelea makundi na dharau miongoni mwa wabunge, matumizi mabaya ya madaraka na kushindwa kumudu majukumu yake.
Mwanzoni mwa Aprili, bunge la Eala lilivunjika baada ya kuibuka malumbano kati ya makundi mawili yanayosigana, moja likitaka kumng’oa Spika na jingine likimtetea.
Zziwa ni Spika wa tatu wa bunge la Eala na wa kwanza mwanamke kukalia kiti hicho. Spika wa kwanza alikuwa Abdulrahama Kinana wa Tanzania aliyefuatiwa na Abdirahin Haithar Abdi kutoka Kenya.
Katika uamuzi wao wenye kurasa 16, Jaji Butasi na wenzake, Jaji Isaac Lenaola na Jaji Monica Mugenyi walisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili za wadai na wadaiwa, mahakama imejiridhisha kuwa wadai wa kwanza na wa pili, hawatapata madhara makubwa iwapo zuio la muda lisipotolewa.
Madai ya msingi yaliyopo mbele ya mahakama katika maombi yao ya msingi, taasisi ya Mbidde Foundation Ltd na Spika Zziwa wanaiomba mahakama kutoa ufafanuzi kuhusu uhalali wa kanuni na taratibu za uendeshaji wa Bunge la Eala wakijielekeza katika kanuni ya tisa inayoelekeza jinsi ya kumwondoa madarakani Spika wakidai zinakiuka baadhi ya vifungu vya katiba ya kuanzishwa EAC.
Mdaiwa wa kwanza katika shauri hilo ni Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard Sezibera anayewakilishwa na Mawakili Wilbert Kaahwa na Stephen Agaba, wakati Mwanasheria Mkuu wa Uganda, ambaye ni mdaiwa wa pili akiwakilishwa na jopo la mawakili watatu, Christine Kaahwa, Oburu Odoi na Madete Geofrey. Wabunge wa Eala wameanza utaratibu wa kumwondoa madarakani Spika kwa kuwasilisha hoja iliyosainiwa na wabunge zaidi ya wanne kutoka kila nchi mwanachama

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...