Pages

April 8, 2014

WAASISI ZANZIBAR WATOA YA MOYONI KUMBUKUMBU YA KIFO CHA SHEIKH ABEID AMANI KARUME.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akiweka shada la mauwa katika kaburi la Marehemu Rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume,wakati wa hitma na dua iliyoombwa na wananchi wa Zanzibar katika Ofisi ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar leo mchana,[Picha na Ramadha Othman,Ikulu.]

 
MKE wa marehemu Abeid Amaan Karume, Mama Fatma Karume aliwataka vijana kuyaenzi Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa kuacha chuki za ukabila, kidini ambazo zinaweza kuleta mgawanyiko wa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliyasema hayo katika Hitma ya Hayati Karume aliyeuawa kikatili Aprili 7 mwaka 1972 katika jengo la Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui pamoja na viongozi wengine wa chama cha ASP.

Katika mashambulio hayo aliyekuwa Katibu Mkuu wa ASP Shekhe Thabit Kombo alijeruhiwa kwa kupigwa risasi ya mguu.

“Vijana tuachane na chuki za ukabila na za kidini ambazo zinaweza kuleta mgawanyiko wa wananchi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania....tuishi kama walivyotuagiza wazee wetu,” alisema.

Hitma hiyo iliongozwa na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Shekhe Khamis Haji na kuhudhuriwa na viongozi wa kidini na serikali, akiwemo Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Katika maelezo yake, Mama Fatma alisihi vijana kuishi kama alivyofikiria muasisi huyo wa mapinduzi ya Zanzibar ya kutokuwepo kwa ubaguzi wa aina yoyote ile.

Alisema ukombozi wa nchi ya Zanzibar umeletwa na Mapinduzi ambapo kabla ya hapo hakuna mwananchi aliyekuwa na uwezo wa kumiliki ardhi kwa ajili ya kujenga nyumba au shughuli za Kilimo.

“Tunapomkumbuka hayati Karume basi tunatakiwa kuyaenzi yale mambo yote mema ambayo yeye aliyasimamia kwa kipindi chote cha uhai wake,” alisema Mama Fatma.

Alisema Karume alichukia chuki na ukabila zilizowabagua Waafrika katika nchi yao, mambo ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yaliyosababisha kufanyika kwa Mapinduzi ya mwaka 1964.

Naye mmoja wa viongozi wa waasisi walioshiriki katika Mapinduzi ya mwaka 1964, Mzee Juma Ame (88) alisema utu wa Mwafrika ulikuwa huru kutokana na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yaliyoongozwa na Karume.

Ame, ambaye alipata kushika nyadhifa mbalimbali katika Chama cha ASP hadi Chama Cha Mapinduzi, alisema Karume mara baada ya kushika hatamu ya kuongoza dola, alitekeleza manifesto ya chama cha ASP ambayo iliweka kipaumbele suala la wazalendo kumiliki ardhi ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi.

“Karume alitekeleza manifesto ya ASP kwa kugawa ardhi eka tatu tatu kwa wananchi wa Unguja na Pemba kwa ajili ya kazi za kilimo na ujenzi wa nyumba katika mwaka 1965,” alisema.

Naye aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, Makame Mzee aliwataka Wazanzibari kuyaenzi yale mambo yote muhimu yaliyoasisiwa na Karume ambayo yameleta manufaa makubwa wa Wazanzibari, ikiwemo Muungano.

“Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo mambo makuu ambayo Karume aliyapa kipaumbele..... tulipofanya Mapinduzi mwaka 1964 tulikaa muda wa miezi minne tu tukaungana na wenzetu wa Tanzania Bara na kuzaliwa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano,” alisema Mzee.

Katika kisomo cha hitma kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano, Alhaji Ali Hassan Mwinyi pamoja na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Aidha katika kisomo cha hitma kilichohudhuriwa pia na wanawake akiwemo mjane wa marehemu mama Fatma Karume, wake wa viongozi wakuu pamoja na wajukuu wa marehemu.

Wakati huo huo, vijana wa Chama Cha Mapinduzi wametakiwa kumuenzi rais wa kwanza wa Zanzibar Abeid Amaan Karume kwa kufanya kazi na kuweka maslahi ya taifa mbele.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Khamis Juma wakati akifunga kongamano la vijana wa Chama Cha Mapinduzi kuhusu wajibu wao na kumuenzi hayati Karume.

Alisema miongoni mwa taasisi ambazo zilipewa kipaumbele cha kwanza na Karume ni Umoja wa Vijana wa ASP, ambapo aliamini kwamba vijana ndiyo nguvu za chama imara watakaojenga taifa.

Aidha, Sadifa aliwataka vijana kamwe kuacha kuyumbishwa na watu mbali mbali wasioitakia mema Zanzibar pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni kielelezo cha taifa.

Alisema miongoni mwa mambo ambayo yalipewa kipaumbele na Karume ni kuziunganisha nchi mbili zilizokuwa huru na kuzaliwa kwa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, mwaka 1964.

Alisema faida za Muungano zinaonekana hii leo ambapo wananchi wa Zanzibar wapo huru kuishi sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupiga hatua kubwa za maendeleo na uchumi.

“Tunapomkumbuka hayati Karume basi tunatakiwa pia kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni matokeo ya juhudi binafsi za mwasisi wa taifa hili,”alisema.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unatimiza umri wa miaka 50 ifikapo Aprili 26 mwaka huu, ukiwa Muungano wa kupigiwa mfano ulioweza kudumu duniani hadi sasa.

Kongamano la kumuenzi hayati Karume lilitayarishwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi kwa kushirikiana na ofisi ya mkoa wa Mjini Magharibi ya chama hicho.

Katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete ameongoza wananchi mbali mbali katika hitma ya kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume iliyofanyika katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa.

Aidha viongozi wakuu wa nchi waliweka shada la maua pamoja na wanafamilia wa marehemu na waliokuwa waasisi wa mapinduzi walioshirikiana na marehemu.

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliweka shada la maua katika kaburi la marehemu lililopo pembeni mwa jengo la Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.

Aidha Rais Kikwete aliweka shada la maua katika kaburi la marehemu ambaye hadi anauawa alikuwa makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kiongozi aliyeshiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar, Juma Ame naye aliweka shada la maua katika kaburi la marehemu kwa niaba ya wazee walioshiriki katika Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964.HABARILEO

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...