Msemaji wa Serikali na
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene (kushoto) akizungumza na
wahariri wa Gazeti la Jamhuri Bw. Deodatus Balile, Muhariri Mtendaji (katikati)
na Bw. Manyerere Jackton , Naibu Muhariri Mtendaji (kulia) alipotembelea Ofisi
za gazeti hilo mtaa wa Samora jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya
utaratibu wa watendaji wa Idara ya Habari kuvitembelea vyombo vya habari kwa
lengo la kuimarisha ushirikiano na kutatua changamoto zinazoikabili tasnia ya
Habari nchini.
Muhariri Mtendaji wa Gazeti
la Jamhuri Bw. Deodatus Balile (kulia) akizungumza jambo na viongozi wa Idara ya
Habari waliotembelea ofisi za gazeti hilo leo jijini Dar es salaam. Kutoka
Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari-Usajili wa Magazeti Bw.
Raphael Hokororo,Afisa habari wa Idara ya Habari Bi. Jovina Bujulu na Mkurugenzi
wa Idara ya Habari na Msemaji wa Serikali Bw. Assah
Mwambene.
Mkurugenzi Msaidizi wa
Idara ya Habari-Usajili wa Magazeti Bw. Raphael Hokororo akifafanua utaratibu wa
utoaji wa vitambulisho kwa waandishi wa habari (Press Card) na namna Idara ya
Habari inavyozingatia kigezo cha elimu cha taaluma ya Habari katika kutoa
vitambulisho kwa waandishi wa Habari (Press Card) hapa
nchini.
Na. Aron Msigwa
–MAELEZO.
Vyombo vya habari nchini
vimeaswa kutoa kipaumbele kwa habari zinazojenga jamii kwa kuihamasisha
kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo, kudumisha uzalendo na kuepuka
habari zinazoweza kusababisha mgawanyiko na chuki katika
jamii.
Wito huo umetolewa leo
jijini Dar es salaam na Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw.
Assah Mwambene alipotembelea ofisi za gazeti la Jamhuri zilizoko mtaa wa Samora
jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa Idara hiyo kuvitembelea
vyombo mbalimbali vya habari nchini kwa lengo la kukuza ushirikiano na kujadili
changamoto mbalimbali za tasnia ya habari hapa nchini.
Amesema kuwa serikali
inaheshimu mchango mkubwa unaotolewa na tasnia ya habari hapa nchini na
kuongeza kuwa habari ni moja ya sekta inayokuwa kwa kasi, yenye uwekezaji
mkubwa na inayoajiri watu wengi hapa nchini.
“Sisi kama serikali ni
wajibu wetu kuhakikisha kuwa tasnia ya habari hapa nchini inapiga hatua kutokana
na umuhimu wa pekee ilio nao katika jamii,hivyo utaratibu huu wa kuvitembelea
vyombo vya habari ni wa kawaida ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu na
kujadili namna ya kutatua changamoto mbalimbali zilizopo” .
Akizungumza na wahariri wa
gazeti hilo Bw. Mwambene amesema kuwa vyombo vya habari hapa nchini vinao wajibu
mkubwa wa kuhakikisha kuwa vinatoa kipaumbele kwa habari zinazogusa masuala
mbalimbali ya wananchi na kuibua changamoto mbalimbali zilizo katika jamii kwa
lengo la kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ustawi wa taifa.
Amelipongeza gazeti hilo
kwa kuendelea kuzingatia weledi katika utoaji wa habari zake kwa kuweka
msisitizo wa utoaji wa habari zinazohamasisha uzalendo.
“Kwanza nawapongeza kwa
kazi mnayoendelea kuifanya hasa moyo wa uzalendo mliouonyesha mlipokuwa
mkiandika habari na kuchapisha makala kuhusu uhusiano wa Tanzania na nchi za
Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia katika masuala mbalimbali yenye
kuhamasisha uzalendo nchini”
Ameeleza kuwa hivi sasa
taifa la Tanzania liko katika mchakato wa masuala makubwa yanayogusa maisha ya
watu na maendeleo yao yakiwemo ya Uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka ujao na
zoezi linaloendelea la kupata katiba mpya na kufafanua kuwa katika hilo vyombo
vya habari vina wajibu wa kuhamasisha umoja wa kitaifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara ya Habari – Usajili wa Magazeti Bw. Raphael Hokororo amesema
kuwa katika kuhakikisha kuwa taaluma ya habari inaendelea kulindwa hapa nchini
na waandishi wa habari wanafanya kazi zao bila vikwazo idara ya Habari imekuwa
ikitoa vitambulisho vya waandishi wa habari (Press Card) kwa waandishi wenye
sifa na taaluma ya habari.
Amesema utoaji wa
vitambulisho kwa waandishi wa habari umesaidia kudhibiti uwepo wa waandishi
wasio na sifa katika shughuli mbalimbali za serikali ikiwemo mkutano wa Bunge
Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
“Katika hili tumeweka
msisitizo wa matumizi ya vitambulisho hivi na tumeanza na Bunge maalum la Katiba
waandishi wote wanaoandika habari za bunge la katiba tumewapatia vitambulisho”
Amesema Bw. Hokororo.
Kwa upande wake Muhariri
Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri Bw. Deodatus Balile amewapongeza viongozi hao wa
Idara ya Habari wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara hiyo Bw. Assah Mwambene
kufuatia utaratibu huo wa kuvitembelea vyombo vya habari na kuongeza kuwa
unaongeza ushirikiano baina ya vyombo vya habari na
serikali.
Kuhusu mchakato wa kupata
katiba mpya na uchaguzi mkuu ujao Bw. Balile ameeleza kuwa gazeti la Jamhuri
linaendelea kutoa kipaumbele kwa habari zenye maslahi kwa taifa na pia habari za
vyama vya siasa vyenye kujenga hoja kwa wananchi.
Aidha amesema kuwa wao kama
chombo cha habari makini wataendelea kuihabarisha jamii kwa kuzingatia maadili,
uzalendo na kukemea vitendo viovu vinavyorudisha nyuma maendeleo ya taifa
No comments:
Post a Comment