RAIS Jakaya Kikwete amekubali kuongeza muda wa Bunge Maalumu la
Katiba katika mazungumzo aliyofanya na mwenyekiti wake, Samuel Sitta.
Hayo yalisemwa na
Mwenyekiti huyo wakati akijibu swali la waandishi wa habari katika mkutano wake
jana, Dar es Salaam, baada ya kumaliza mkutano wake na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo katika Kanisa la Mtakatifu
Yosefu.
Ziara hiyo ambayo amesema ni utaratibu aliouanza kukutana na
viongozi wa dini, pia ilimkutanisha na Mufti wa Baraza la WaislamU Tanzania
(BAKWATA), Shekhe Issa Bin Shaaban Simba. Sitta alikutana na Rais Kikwete juzi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Sitta, Rais Kikwete hajataja ni lini Bunge
hilo litaanza tena kwa nyongeza ya siku 20 kwa mujibu wa sheria, baada ya siku
70 zinazomalizika mwezi huu, kuisha ili kufanya jumla ya siku 90. Lakini amesema
uongozi wa Bunge umekusudia lianze tena Agosti mwaka huu.
Alisema lengo
la kukutana na viongozi hao wa kidini ni kuwaeleza kinachoendelea Dodoma, kwa
kile alichodai viongozi hao wana ushawishi na wafuasi wengi nyuma yao, hivyo si
busara kusikia mitaani.
Katika mkutano huo Sitta alikanusha habari ya
gazeti moja lililodai anakwenda kuwaangukia viongozi hao na kusema hana dhambi
za kufanya hivyo.
“Leo (jana) nimepanga kukutana na viongozi wa dini
zetu na si hawa tu nitakaokutana nao, nitaendelea na utaratibu huu kwa viongozi
wengi hata wenye wafuasi wachache, hawa wana ushawishi japo hawahusiki sana na
siasa lakini ni viongozi wa jamii, wanapaswa kupata taarifa sahihi ya nini
kinachoendelea Dodoma,” alisema Sitta.
Alisema katika mazungumzo yake na
Kardinali Pengo jana asubuhi, amemweleza kwa kifupi mchakato unavyoendelea
Dodoma na yeye (Pengo) alimhakikishia kuwa Kanisa Katoliki linaliombea Bunge
Maalumu la Katiba na wajumbe wote ili lengo lifikiwe na Watanzania wapate Katiba
mpya na yenye ubora.
Baada ya kutoa maelezo hayo mafupi ya mkutano wake
na Pengo, Sitta akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa Bunge
hilo, ikiwemo kama muda wa takribani wiki tatu uliobaki unatosha kumaliza kazi
iliyo mbele yao, alisema muda huo hautoshi.
“Ni dhahiri mpaka Aprili 28
tutakuwa hatujamaliza Bunge, itabidi tupishe Bunge la Bajeti la Muungano,
Wawakilishi watarejea Zanzibar na sisi wengine tutabaki Dodoma, bajeti
itafanyika si chini ya miezi miwili, yaani Mei na Juni,” alisema na kuongeza:
“Jana nilionana na Rais Jakaya Kikwete nikamweleza hali halisi ilivyo, kimsingi
alikubali ataongeza muda ingawa hatukufikia kutaja ni lini. Ila sisi tunakusudia tuanze tena Agosti, nimemweleza
kwa undani maana hata baadhi ya nchi nyingi zimechukua muda kuandika Katiba,
akaona ukweli huu akatuongezea”.
Sitta alisema Bunge litatangaza rasmi
utaratibu huo utakapokamilika ila alisisitiza kuwa, kwa hali inavyoendelea
hawawezi kuendelea kubaki Dodoma kwa ajili ya Katiba kwa kuwa kisheria siku
zitakwisha na pia mwingiliano wa sikukuu za Pasaka na Muungano Aprili 26,
zitapunguza siku.
Muundo wa Muungano:
Awali, akizungumzia kuhusu
muundo wa muungano hasa baada ya kuibuka kwa madai ya kutaka Hati ya Muungano
wakati wa mjadala wa sura ya kwanza ya sita ya Rasimu ya Katiba uliofanyika
katika kamati, Sitta aliwataka wabunge kutopoteza muda kujadili serikali ngapi
ziwepo.
Aidha, Sitta amesema ipo hatari ya kupoteza muda mwingi
kuzungumzia muundo wa serikali uweje, jambo analoona kwa baadhi ya watu,
wanataka serikali nyingi kwa uchu wa madaraka wakijua wakikosa uongozi upande
mmoja, watapata upande mwingine.
Alisema ingawa suala la serikali ni
muhimu kwa kuwa ndio linalotoa dira, ila haja kubwa ipo katika kuipitia rasimu
Ibara kwa Ibara kama alivyoagiza Rais Kikwete.
Alitolea mfano suala la
uadilifu na kushauri wajumbe wakipitia vizuri, watashauri mfumo gani uwekwe
kuwabana zaidi viongozi.
“Kiongozi anapaswa ajue anaingia katika
utumishi wa umma si kuchota fedha na kufanya ufisadi bali suala kubwa ni
maendeleo ya nchi, ustawi wa wafanyakazi, wakulima na vijana, kuhakikisha sheria
zinakuwepo kuzuia mikataba mibovu, kwa mfano Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania)
inavyopandisha umeme, wananchi wanaumia.”
“Tukiingia katika sura
nyingine za rasimu, Katiba lazima ibane tutunge sheria zilizo wazi, angalia
suala la Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tunajaza fomu kisha zinakuwa siri,
sasa zina haja gani, ni za nini, si bora tuache, maana naweza kujaza nina
kijumba kibovu kimoja, kumbe nina majumba,” alitoa mfano Sitta.
Alisema,
“Ili kuzuia viongozi kujitajirisha, ni lazima sheria ziwe kali la sivyo wizi
utaendelea, sheria inapaswa kuwakwamisha wanaopenda madaraka…., maombi yangu
kuhusu mchakato, pamoja na purukushani, kutaka kuonekana, vijana machachari,
lakini wengi wanataka Katiba mpya ipatikane.”
Sitta akifafanua kuhusu
ama serikali tatu ama mbili, alinukuu alichowahi kusema mwanasiasa mkongwe
nchini, Kingunge Ngombale- Mwiru kuhusu suala hilo kwamba ni kama wanaotaka
serikali tatu wanataka madaraka, kwamba akikosa uongozi katika upande mmoja,
apate kwingine.
Hati ya Muungano; Sitta aliwaambia waandishi
wa habari kumekuwepo na madai ya hati ya Muungano katika kamati na kwamba, ni
ajabu kuona ndoa iliyodumu kwa miaka mingi, wahusika sasa wamekuwa vikongwe,
anatokea mtu anadai cheti cha ndoa.
“Ni kama haamini kwamba hiyo ndoa
ilifungwa ama! Ni ajabu kweli, vielelezo ni pamoja na Sheria ya Bunge ya Aprili
5 mwaka 1964, Msekwa akiwa Katibu wakati huo alikwenda katika kamati kueleza
yaliyotokea wakati ule, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema
amekwenda kueleza.” “Ndoa watu wamefunga miaka, wamekuwa vikongwe, wajukuu leo
wanadai cheti cha ndoa, ni upuuzi, mtu anayehitaji utafiti aendelee, hakuna
anayemzuia ila haituzuii sisi kuendelea,” alieleza Sitta.
Ripoti za
Kamati; Kwa mujibu wa Sitta, Alhamisi na Ijumaa wiki hii, taarifa za
kamati zitatolewa bungeni na maoni ya wengi na ya wachache yataelezwa ili
kuruhusu mjadala kuanza ndani ya ukumbi na kwamba katika sura ya kwanza hadi ya
sita, kila mjumbe atachangia.
“Baada ya hapo kazi itakuwa nyepesi,
siwezi kutabiri kitakachotokea lakini hoja yenye maana itashinda, ukiacha
wachache wenye utamaduni wa fujo, wengi wanataka ifike mahali tupate Katiba
mpya, tusichezee mabilioni ya Watanzania bure.
Uzoefu wa Kenya;
Sitta alitumia nafasi hiyo kutolea uzoefu wa nchi jirani ya Kenya mwaka
2007 walipoingia katika machafuko ya kisiasa baada ya kushindwa kufanya
mabadiliko katika Katiba yao na kufanya uchaguzi.
Alisema kazi
inayofanyika Dodoma ni kubwa hivyo inapaswa kufanyika kwa umakini mkubwa vile
vile. Akiwa na Mufti Mkuu Akizungumza mara baada ya kukutana na Mufti wa
Tanzania, Shekhe Issa Bin Shaaban Simba, Sitta alisema ujumbe wake ulipokewa
vizuri katika Ofisi za Bakwata, Dar es Salaam na kwamba Mufti alishukuru hatua
hiyo ya Waislamu kushirikishwa.
“Ukweli Mufti amefurahia huu ujio wangu
hapa na kuueleza kuwa anafuatilia kwa makini kile kinachoendelea kwa sasa kule
Dodoma na zaidi ameuombea mchakato huu uweze kuisha kwa amani na utulivu hadi
katiba mpya itakapopatikana” “Zaidi ametutaka wajumbe wote kuvumiliana na
kufanya kazi yetu tukitanguliza maslahi ya Taifa na kuachana na misuguano ili
hatimaye katiba iweze kupatikana,” alisema Sitta.HABARILEO
No comments:
Post a Comment