Pages

April 5, 2014

ISMAIL JUSSA, TUNDU LISSU, MNYIKA WAUMBULIWA NA MKOSAMALI BUNGE MAALUM LA KATIBA DODOMA



TABIA ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, hasa kutoka vyama vya upinzani waliounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutafuta kasoro ndogo ndogo za kutaka Bunge liahirishwe mara kwa mara, imewatokea puani. Jana baadhi ya wajumbe hao akiwepo Ismail Jussa Ladhu, Tundu Lisu, John Mnyika na Moses Machali, walisimama kupinga marekebisho ya kanuni za Bunge Maalumu kwa madai kuwa yameletwa haraka haraka na yana nia ovu.

Mtindo wao Alianza Jussa, akasema wajumbe hawana jedwali la marekebisho ya Kanuni hivyo ni bora hoja ya marekebisho hayo iahirishwe ili kuwapa nafasi ya kuyapitia na kuleta jedwali lao la marekebisho.

Wakati Jussa akidai wengi wao hawana jedwali hilo la marekebisho, alishangaa kuona wajumbe wenzake wengi, akiwemo aliyekaa naye wakipepea juu jedwali hilo, kuonesha ni yeye peke yake na baadhi ya wachache hawakuwa na jedwali husika kwa kuwa wengi walikuwa nayo.

Lissu Jussa alilazimika kukaa baada ya kuona hali hiyo, lakini akasimama Lissu na kutoa hoja ya kutaka mjadala wa marekebisho hayo, uahirishwe kwa madai kuwa hawajayasoma.

“Je, ni busara kwa wajumbe kujadili mapendekezo ya marekebisho haya sasa hivi wakati hatujafanya mashauriano, hatujasoma wala hatujayatafakari?” Alihoji Lissu na kuendelea; “Naomba uahirishe kikao hiki…haiwezekani kujadili mabadiliko haya bila kuyapitia Makamu Mwenyekiti.”

Mnyika Mnyika alisimama na kuunga mkono hoja ya Lissu na Jussa kwa madai mapendekezo hayo yameletwa ghafla ghafla, wakati sehemu kubwa walikuwa nayo tangu mwishoni mwa wiki iliyopita na waliyatumia kukataa marekebisho hayo huku Lissu akiyaita ni takataka.

Huku akisema kuwa mapendekezo hayo yameletwa ghafla ghafla, Mnyika alisahau na kusema kuwa mapendekezo hayo yaliwahi kuletwa kwa maana alishayaona na ndiyo yalikataliwa, sasa yameletwa tena yakiwa yameongezwa kipengele kipya cha C.

Akijadili mapendekezo ya marekebisho hayo, alitaka Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu, isipewe mamlaka zaidi ikiwemo ya kuongeza muda na kupanga sura za rasimu ya Katiba za kujadili kwa madai kuwa haina usawa wa mgawanyo wa makundi ndani ya Bunge hilo.

Pia alipinga mapendekezo hayo kumuongezea Mwenyekiti wa Kamati mamlaka ya kusimamia nidhamu ndani ya Kamati ambapo akiona kuna mjumbe analeta fujo, anaruhusiwa kuagiza mpambe wa Bunge, kumtoa mjumbe husika nje ya ukumbi na asihudhurie kikao kwa siku nzima.

Machali Machali alipopewa nafasi, aliendelea kuunga mkono kuwa mapendekezo hayo yameletwa ghafla ghafla na wamepewa dakika 15 kuyajadili, kama wanataka kuleta mabadiliko hawatapata haki hiyo. Pia alipinga mapendekezo hayo kuongeza madaraka kwa Mwenyekiti wa Kamati kumtoa nje mjumbe anayehatarisha utulivu wakati wa majadiliano, akidai kuwa baadhi ya wenyeviti wanatukana wajumbe.

“Sitarajii Mwenyekiti wa Kamati atumie lugha isiyo ya staha, halafu mjumbe akitumia atolewe nje kwa kutumia mpambe wa Bunge,” alisema Machali.

Waumbuliwa Wakati wajumbe hao wa Ukawa wakipendekeza Bunge liahirishwe jana wapate nafasi ya kujadili mapendekezo hayo ya mabadiliko ya Kanuni, ikiwezekana walete majedwali yao ya mabadiliko, mjumbe mwenzao Felix Mkosamali, alisimama na kuhoji wajumbe hao ni wapinzani wa aina gani.

Mkosamali aliyeunga mkono mapendekezo hayo kwa asilimia 100, aliwataka wapinzani wenzake waachane na tabia ya kupinga vitu vidogovidogo visivyo na msingi wowote.

“Wapinzani lazima tupinge mambo ya msingi na sio kupinga vitu vidogovidogo, huo ni upinzani wa aina gani? Mpinzani akipinga suala la kura ya wazi na kutaka kura ya siri, hilo ni suala la msingi.

“Lakini ni mpinzani gani anayepinga wajumbe kupewa muda wa kupumzika na kufanya utafiti siku ya Jumamosi kama inavyopendekezwa katika kifungu cha 14?”

Alihoji huku akipigiwa makofi. Alisema hata Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu si kamati ya vichaa kuleta hoja ya kubadili Kanuni na kuongeza muda wa kujadili sura za rasimu ya Katiba.

“Tumeona wote hapa siku mbili hazitoshi, eti mpinzani anaamka na kupinga…mnapinga vitu vidogovidogo wakati mambo ya msingi mnabadilika badilika, tusipoteze muda hapa,” alisisitiza Mkosamali.

Kauli ya Mkosamali iliungwa mkono na wajumbe wengi, akiwemo Job Ndugai, Fahmy Dovutwa na Jafo, lakini mjumbe Ezekiel Oluoch, alizidi kuwashambulia wapinzani hao huku akikubaliana na Mkosamali.

“Naunga mkono mapendekezo ya marekebisho na suala la kuahirisha sio hoja hapa hata kidogo katika Bunge hili...hapa niliposimama nyuma yangu kuna walimu 36,000 hawajalipwa fedha zao zote za posho ya kujikimu, wako waliolipwa posho ya siku nne badala ya siku saba, kisa fedha hakuna.

“Wako walimu hawajapanda madaraja kisa fedha za kuwapandisha madaraja hakuna, kisha nyie mnaleta hoja ya kuahirisha Bunge ili mle posho za bure, haifai,” alisema Oluochi. Siri hadharani Wakati wenyeviti karibu wote wa kamati za Bunge wakitetea suala la utulivu, uvumilivu na staha kwamba ndivyo ilivyokuwa katika kamati ambazo mijadala yake ni siri, jana wajumbe wao wametoa siri kuwa hali haikuwa hivyo.

Hali hiyo ilianza na Machali kudai kuna Mwenyekiti wa Kamati alitukana mjumbe na kusisitiza kuwa hilo haliwezekani. Baada ya Machali kutoa hoja hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Namba Kumi, Anna Abdallah, alisimama akasema katika kamati anayoiongoza ambako Machali ni mjumbe wake, hakukuwa na tukio kama hilo, labda amesema ya kusikia kutoka katika kamati zingine jambo ambalo si zuri.

Kutokana na hoja hiyo, Machali alisimama na kutoa ufafanuzi kuwa si Anna aliyetukana, bali alikasimu madaraka kwa Makamu Mwenyekiti, Salmin Awadh Salmin, ambaye alisema baadhi ya wajumbe wanafanya uhuni. Kauli hiyo ya Machali, ilimuamsha Mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Dk Ave Maria Semakafu, ambaye alisema anaona Kanuni zinatumika kufanya uhalifu kwa kuwa mjumbe aliyepita, yaani Machali, wakati wenzake wakijadili, alikuwa akitoa ishara ya kidole na kichwa kuonesha kuwa wenzake hawana akili.

“Mwenyekiti Machali ndiye aliyekuwa mhuni,” Dk Ave Maria alirudia neno hilo ambalo Machali alidai ni tusi. Baada ya Dk Ave Maria, alisimama mjumbe Faida Bakari, ambaye naye alimshambulia Machali kwamba amekuwa na tabia mbaya katika Kamati, anaropoka mara kwa mara ndio maana hataki mapendekezo ya Kanuni, yanayomruhusu Mwenyekiti kumtoa nje mjumbe anayehataraisha utulivu wa Kamati. Oluoch alipokuwa akichangia alisema wajumbe wengi hawafanyi utafiti wanasimama na kitabu kimoja tu cha Mwalimu Nyerere.

“Nimeshuhudia watu wanauliza fulani kapigaje kura, akiambiwa kapiga ya Ndiyo na yeye anapiga kura ya Ndiyo,” alisema Oluoch.

Mjumbe huyo alifikia kusema kuwa Kamati hizo zimeanza kutumika kama sehemu za mipasho, mjumbe akichangia anajibiwa ni kwa sababu anataka madaraka.

“Tunajadili Muungano, mtu anasimama na kusema eti ving’ora vilikuwa viwili wanataka kutuongezea cha tatu...wanasema unga wa ngano, hapa huo unga wa ngano unahusu nini?” Alihoji Oluoch na kuongeza kuwa kamati hizo zimefikia hatua habari za ugomvi katika nyumba za watu zimehamia huko.

Kauli hizo zilimuibua Makamu Mwenyekiti wa Kamati namba tano, Assumpter Mshama, ambaye alisema Oluoch pia aliomba kitabu hicho cha Nyerere na kumshangaa kwa kubeba kompyuta na kwenda nayo katika kamati.

Kuona hali inaenda pabaya, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisimama na kupendekeza kwa Makamu Mwenyekiti mambo hayo yasiendelee kwa kuwa wajumbe wameanza kujiumbua mbele ya wananchi na kuongeza kuwa kama mjadala kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya Kanuni yameisha, mjadala ufungwe.

Mapendekezo hayo ya mabadiliko ya Kanuni za Bunge yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Ameir Pandu Kificho, yalipitishwa na Bunge, baada ya Makamu Mwenyekiti wa Bunge, Samia Suluhu kuwahoji wajumbe na wengi kukubali yapite.HABARILEO

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...