
JEURI
ya wazi inayoonekana kuwemo ndani ya taarifa ambazo zimekuwa zikichapishwa mara
kwa mara na vyombo vya habari vya serikali ya Rais Paul Kagame wa Rwanda dhidi
ya Rais Jakaya Kikwete na serikali yake, inaelezwa kujengwa na ushirika wake wa
kiintelijensia alioupandikiza ndani ya mfumo wa serikali na taasisi mbalimbali
hapa nchini,MTANZANIA limedokezwa.
Taarifa zilizolifikia gazeti la
MTANZANIA kutoka kwa watu waliokaribu na viongozi wa Rwanda na wale walioko
kwenye taasisi mbalimbali za kiserikali hapa nchini,zinaeleza kuwa taarifa
ambazo zimekuwa zikiripotiwa na vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo,
msingi wake unaweza kuwa mtandao ambao serikali ya Kagame imeujenga hapa
nchini.
Kwamba Rwanda, mbali na kufanikiwa kupenyeza watu wake kwenye
mifumo ya kitaasisi hapa nchini, pia imefanikiwa kujenga ushirika na watu wa
kada mbalimbali wenye umaarufu,ushawishi na wanaoheshimika nchini, wakiwemo
baadhi ya wasomi na wanasiasa.

Kuvuja
kwa taarifa hizi, kumekuja wakati ambao gazeti la serikali ya Rwanda,Rwanda
Times na mtandao wa News of Rwanda, yakiripoti taarifa zinazoigusa serikali ya
Rais Kikwete, ikinukuu vyanzo vya kutoka hapa nchini, japo ukweli wa taarifa
hizo ukiwa haujulikani,kutokana na Ikulu ya Dar-es-salaam kuzikanusha mara kwa
mara.
Dhana hii inapewa nguvu na taarifa mpya kabisa zilizotufikia,
ambazo zinadai kuwa katika kuendelea kuimarisha mtandao wake, Serikali ya Rwanda
imechangisha fedha kwaajili ya baadhi ya vyama vya siasa hapa nchini ili kulinda
maslahi yake.Taarifa hizo zinamtaja Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo, Profesa
Silas Lwakabamba, ambae aliwahi kusoma na kuishi nchini kuwa ndiye aliye endesha
harambee hiyo ambayo inadaiwa ilimshirikisha Rais Kagame.
Habari zaidi
ambazo MTANZANIA imezipata zinadai kuwa katika harambee hiyo, iliyohudhuriwa na
baadhi ya Mawaziri wa serikali ya Rwanda pamoja na wafanyabiashara wakubwa
nchini humo,Rais Kagame kwa upande wake alichangia Dola
500,000.
Gazeti hili limedokezwa kuwa, lengo la harambee hiyo, ni
kuhakikisha ushawishi wake unafanikiwa, hasa kwa watu ambao wamekuwa wakiiunga
mkono Rwanda, hususani wakati huu mgumu ambao inakabiliwa na tuhuma za kuchochea
mapigano katika eneo la Mashariki ya Congo, ambako Tanzania imepeleka wanajeshi
wake.
Katika mkakati huo, walengwa ni vyama vya upinzani, kutokana na kuwa na
uhusiano wa shaka na serikali iliyoko
madarakani.
Tayari mara kadhaa vyombo vya habari
Rwanda, hususani vile vya serikali, vimekuwa vikitumia kauli zinazotolewa na
wapinzani hapa nchini, kama hoja ya utetezi wake dhidi ya uhusiano mbaya na
Ikulu ya Dar-es-salaam.
Profesa Lwakabamba, ambaye
anatajwa kuongoza zoezi la sasa, inaelezwa kuwa serikali ya Rwanda imeamua
kumtumia kutokana na uelewa wake kuhusu
Tanzania.
Kabla ya taarifa hizi, Lwakabamba aliwahi
kuripotiwa na gazeti moja (si MTANZANIA) kwamba ni waziri mwenye asili ya
Tanzania aliyechaguliwa katika serikali ya
Rwanda.
Inaelezwa kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkuu
wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, lakini pia alisoma Chuo Kikuu Dar-es-salaam
(UDSM) Kitivo cha Uhandisi, na mwaka 1981 alikuwa Mkuu wa kitivo cha Uhandisi,
kazi aliyoifanya mpaka anaondoka nchini.
Profesa
Lwakabamba, ambaye anaelezwa kuijua vyema Tanzania kutokana na kuishi muda
mrefu, alipata elimu ya msingi Muleba, mkoani Kagera na baadaye kujiunga na
shule ya sekondari ya Ihungo.
Mwaka 1971 na 1975
alipata Shahada ya Uzamivu katika Kitivo cha Uhandisi, baada ya kujiunga na Chuo
cha Leeds, Uingereza kwaajili ya shahada ya fani
hiyohiyo.
Msomi huyo anaelezwa kwenda Rwanda mwaka
1997,baada ya kuombwa na Rais Kagame, ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya
wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu katika taifa lake, baada ya
kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka
1994.
Gazeti hili lilimtafuta Profesa Lwakabamba kwa
njia ya mtandao ili kupata ufafanuzi kuhusiana na harambee hiyo, lakini hakuweza
kujibu maswali aliyoulizwa.
Juhudi za kumtafuta
Profesa Lwakabamba bado zinaendelea. Wakati hayo yakitokea,taarifa nyingine
zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa katika mkakati huo,mbunge mmoja (jina
tunalo), hivi karibuni alisafiri kwenda Rwanda akipitia Afrika
Kusini.
Inaelezwa kuwa mbunge huyo alionana na
baadhi ya viongozi wa serikali ya nchi hiyo, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Rais
Kagame kuhakikisha anaimarisha mtandao wake hapa
nchini.
Mbali na mbunge huyo,taarifa hizo zimewataja
baadhi ya wanasiasa wengine ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifaidika na fedha
za serikali ya Rais Kagame, kwa kujua ama pasipo kujua kama lengo lake ni
kuwaweka katika mtandao wake
huo.
Chanzo:
Mtanzania
Post a Comment