![]() |
| Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha,Liberatus Sabas |
Na
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wananchi
wa Tarafa ya Endabashi iliyopo wilayani Karatu wamefurahishwa na utaratibu mpya
wa jeshi la Polisi wa kupeleka askari 15 kila Tarafa kwa lengo la kuimarisha
ulinzi katika maeneo yao.
Akimshukuru Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, kwa
niaba ya wananchi hao Diwani wa kata ya Buger Bw. Emmanuel Tlaqho, alisema
kwamba mbali na mpango huo pia wamepokea kwa mikono miwili uanzishaji wa Dawati
la Jinsia na Watoto.
Bw.
Tlaqho alisema kwamba Dawati hilo litasadia katika mambo mengi ya kijamii ikiwa
ni pamoja na kutatua migogoro ya ndoa na utelekezwaji wa familia.
Alisema
pamoja na kuwepo kwa Dawati hilo pia viongozi wa mtaa wa maeneo hayo wanatakiwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni
pamoja na kuwaasa wanandoa ili waishi
kwa amani ndani ya familia zao pia kutotumikisha watoto pamoja na
kutowanyanyasa.
Naye
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Liberatus Sabas akizungumza na viongozi na wananchi wa maeneo ya Tarafa hiyo
ambayo ina jumla ya vijiji 16 na wakazi wapatao 68,339, alisema kwamba mpango
huo wa kupeleka askari 15 kila Tarafa una nia ya kuliweka Jeshi la Polisi
karibu na wananchi ili waweze kushirikiana katika utatuzi wa matatizo ya
kiulinzi na kiusalama kabla hayajafika kwa Mkuu wa Polisi wa wilaya.
Kamanda
Sabas aliongeza kwa kusema kwamba, mbali na askari hao kuimarisha ulinzi katika
maeneo hayo pia watakuwa wanatoa elimu ya Polisi Jamii kwa askari wa vikundi
vya ulinzi shirikishi ili wajue namna ya utendaji wa kazi za ulinzi ikiwa ni
pamoja na ukamataji salama na pia kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano
mbalimbali ili waweze kujua haki zao na wajibu wao katika suala zima la ulinzi.
Kamanda
Sabas aliwasisitizia wakazi wa Tarafa hiyo wawe wanatumia mbinu za Ulinzi
Jirani katika nyumba zao. Alisema suala la ulinzi ni la kila mmoja na
haliihitaji kusubiri kudra ya M/mungu kwani uwezo wa kuzuia uhalifu upo ndani
yao.
Akimalizia
kutoa elimu hiyo kwa wakazi hao, Kamanda Sabas aliwaambia katika suala la
ulinzi itikadi za kisiasa na udini hazina nafasi kwani mhalifu anapovamia eneo
lolote hamuulizi mtu kwamba ni wa Chama gani au Dini gani bali yeye anatekeleza
kile alichokikusudia.
Kwa
upande wake mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la John Bula alisema
kwamba, inaonyesha dhahiri kwa sasa jeshi la Polisi limeamua kushirikiana na
wananchi kwani katika maisha yake hayawahi kuongea na Kamanda wa Polisi wa Mkoa
ana kwa ana mbali ya kumuona kwenye runinga au akiwa katika msafara wa Viongozi
wa kitaifa lakini kupitia kikao hicho ameweza kuongea naye.
Bw.
Bula alisema kutokana na hamasa iliyotolewa na Kamanda Sabas yeye kwa
kushirikiana na wananchi wenzake watakuwa bega kwa bega na askari hao waliopo
tarafani hapo ambao wanaongozwa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Robert Majenga.
Mpaka
hivi sasa katika Mkoa wa Arusha tayari Kamanda Sabas amekwisha toa elimu juu ya
ulinzi shirikishi kwa wananchi wa Tarafa
mbalimbali za wilaya nne huku bado akisubiri kumalizia wilaya mbili ambazo ni
Ngorongoro na Longido.



إرسال تعليق