Pages

December 16, 2013

RAIS JAKAYA KIKWETE ATEKA MAZISHI YA MANDELA






Qunu: Rais Jakaya Kikwete jana aliyateka mazishi ya Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alipotoa salamu mbele ya maelfu ya waombolezaji na wageni wa kimataifa walioshiriki katika mazishi hayo.
Rais Kikwete aliweka bayana jinsi Tanzania ilivyoshiriki katika vita ya ukombozi si kwa Afrika Kusini pekee bali kwa nchi nyingi za Kusini mwa Afrika zikiwamo Angola, Msumbiji, Zimbabwe na Namibia.
Kadhalika alizungumzia jinsi wapigania uhuru wa ANC walivyoweka kambi zao na kufungua ofisi za chama hicho nchini Tanzania ambako walipewa makazi na vifaa, maelezo ambayo yalishangiliwa na umati wa watu uliohudhuria.
“Kwa hakika ANC walipata makazi mapya Tanzania ambayo waliyatumia kuendesha mambo yao, kujipanga na kuendeleza vita ya ukombozi. Kutoka Tanzania ANC waliweza kuwafikia makada wake na wanachama waliobaki Afrika Kusini kwa kutumia mawasiliano ya siri,” alisema Kikwete na kuongeza:
“Kimsingi Serikali ya Tanzania ililazimika kuanzisha redio maalumu kwa ajili ya vita ya ukombozi ambayo ANC waliitumia kupaza sauti ambazo walikuwa wamenyimwa na utawala wa ubaguzi wa rangi.”
Rais Kikwete aliyekuwa na kazi ya kumwelezea Mandela kama mpigania uhuru, alieleza jinsi Mandela alivyofika Tanzania Januari 1962 bila kuwa na hati ya kusafiria na kwamba katika mazungumzo yake na Hayati Mwalimu Nyerere alieleza mpango wa kudai uhuru kwa njia ya mapambano.
“Mwalimu Nyerere alikuwa na maoni tofauti kuhusu mpango wa kuendesha mapambano kwa kutumia silaha, lakini baadaye walikubaliana na Tanzania ilikubali kuanzishwa kwa kundi hilo na mwalimu (Nyerere) aliwapa sehemu ya kuendeshea shughuli zao na vifaa,” alisema Kikwete na kuongeza:
“Kwa hiyo, kwa wale walioshiriki katika vita vya ukombozi na askari wa MK (Jeshi la ANC), majina kama Kongwa, Mgagao, Mazimbu na Dakawa hayawezi kuwa mageni na pengine mtakumbuka enzi zile maisha yalivyokuwa.”
Kikwete alisema wakati akiwa Tanzania, Mandela alikuwa akiishi kwa aliyekuwa Kada wa TANU, Marehemu Nsilo Swai na kwamba baada ya kusaidiwa kupata nyaraka za kusafiria kwenda Nigeria, Morocco na Ethiopia, aliacha buti zake nyumbani kwa mzee huyo.
“Familia hii iliendelea kutunza buti hizo wakitaraji kwamba Mandela atarudi, lakini wakati anatoka katika safari yake hakupita tena Tanzania na kwa bahati mbaya alipofika Afrika Kusini alikamatwa na kufungwa,” alisema Kikwete katika hotuba iliyorushwa na vituo vyote vya televisheni vya kimataifa.
Aliongeza: “1995 ikiwa mwaka mmoja tangu Mzee Mandela aingie madarakani, viatu vile vililetwa na mjane wa marehemu Swai, Vicky Nsilo Swai ambaye nimekuja naye leo ili ashirikiane nanyi katika msiba huu ninyi mlio ndugu zake.”
Alisema vita ya ukombozi haikuwa rahisi kwani wakati mwingine Tanzania mbali na kuwasaidia wapigania uhuru hati za kusafiria, ililazimika pia kuwapa majina ya bandia ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...