Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe.
UMOJA wa matawi 189 ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Mwanza, umetoa siku tatu kwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bw. Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dkt. Wilbrod Slaa, kutangaza kujiuzulu ndani ya siku tatu vinginevyo watafanya maandamano yasiyo na kikomo.
Tamko hilo limetolewa jana baada ya umoja huo kufanya kikao chake ambacho kilimalizika kwa kutoa tamko la kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Bw. Zitto Kabwe, Dkt. Kitila Mkumbo na Bw. Samson Mwigamba.
Katibu Mkuu, Dkt. Wilbrod Slaa.
Katika tamko lao, umoja huo ulisema uamuzi uliofikiwa na Kamati hiyo woga wa kidemokrasia, unafiki na uzandiki wa hali ya juu kutokana na chama hicho kukwepa demokrasia kwa kisingizio cha kusaliti na uhaini ndani ya chama hicho.
Akisoma tamko hilo, Bw. Robert Gwanchele, ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa matawi ya CHADEMA, mkoani humo, alisema Bw. Mbowe na Dkt. Slaa wanapaswa kujiuzulu nafasi zao ili kupisha uchunguzi wa mapato na matumizi ya fedha za chama zinazotokana na kodi za wananchi.
ZITTO KABWE.
Bw. Gwanchele ambaye pia ni Mwenyekiti wa Vijana Kanda ya Ziwa Magharibi na Mjumbe Kamati Tendaji, Wilaya ya Ilemela, alisema kamati hiyo imewabagua viongozi ambao wametumia nguvu zao na akili nyingi kukijenga chama.
Alisema sababu za kuandamwa viongozi hao ni kutaka kujua mapato na matumizi ya fedha za chama zinazotokana na ruzuku ya fedha za Serikali, michango ya wanachama na wapenzi ambayo wanaitoa katika mikutano ya wazi.
Sababu nyingine ni kujua mapato ya harambee za M4C katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Dar es Saalam, kutaka kujua taratibu za matumizi ya rasilimali ya chama ambazo ununuzi wake una mashaka makubwa.
Migogoro ndani ya chama.
Akizungumzia migogoro ndani ya CHADEMA, Bw. Gwanchele alisema Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bw. Freeman Mbowe, Katibu wake, Dkt. Wilbrod Slaa, wameshindwa kutatua migogoro ya viongozi na wanachama waliopo mikoani kwa njia za vikao.
"Hali hii ndiyo iliyosababisha migogoro hata katika Mkoa wetu na mwisho wa siku tukapoteza Halmashauri ya Jiji baada ya kufukuzwa kwa baadhi ya madiwani, kuvunjwa uongozi wa Mkoa na wabunge kuwa juu ya chama.
"Wabunge wanatumia nafasi zao kupanga safu za viongozi ambao wanaona watawatumikia wao si chama, hali hiyo ndiyo iliyochangia mifarakano ndani ya chama hapa Mwanza hadi baadhi ya viongozi kuvuliwa uongozi kwa maamuzi yasiyozingatia utafiti, uhalisia wa kweli," alisema.
Bw. Gwanchele alisema umoja huo unataka kujua hatua gani zilizochukuliwa dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema, kumkashfu Bw. Kabwe katika mitandao ya kijamii kuwa ni mnafiki na mzandiki.
Pia umoja huo unataka kujua hatua gani zilizochukuliwa na chama dhidi ya Bw. Henry Kilewo kwa kuweka waraka unaoitwa ripoti ya siri ukimuhusisha Bw. Kabwe lakini chama hicho kiliukana mbele ya vyombo vya habari.
"Jambo la kushangaza, viongozi wetu wamelifumbia macho suala hili hivyo baadhi ya wanachama kama sisi tunaamini zengwe hili la kumchafua Bw. Kabwe lina baraka za viongozi wa juu.
"Tulianzisha umoja huu kwa sababu viongozi wetu wanaotuwakilisha katika vikao vya maamuzi ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa, wamekuwa waoga wa kuwakilisha mawazo yetu ambayo tunawatuma badala yake wengi wao wamekubali kuwa vibaraka," alisema.
Alisema CHADEMA ni chama cha siasa ambacho kinapaswa kuendeshwa kwa misingi ya kufuata taratibu, kanuni na katiba si vinginevyo lakini badala yake umeibuka utamaduni wa viongozi wa juu kujitwalia mamlaka.
Mawaziri wa JK
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza Mawaziri waliotajwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa ni mzigo.
Kama Rais Kikwete atashindwa kuchukua uamuzi mgumu dhidi ya viongozi hao, CHADEMA kitalipeleka bungeni suala hilo ili Bunge lichukue hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Bw. John Mnyika, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya uzinduzi wa Rasimu ya Sera ya Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Alisema kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Bw. Nape Nnauye juu ya Mawaziri mzigo ni vyema likafanyiwa kazi na Rais Kikwete badala ya kupuuzwa.
Alisema Bunge ndilo lenye Mamlaka kisheria ya kuwawajibisha Mawaziri hao hivyo ni vyema wabunge wa vyama vyote wakaona umuhimu wa kuungana hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
"Kama kweli kauli ya Kinana na Nape si ya kinafiki basi Rais Kikwete kama Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na CCM Taifa, awafukuze hawa Mawaziri ambao ni mzigo.
"Viongozi wa CCM na wabunge tuungane ili kama Rais Kikwete atashindwa kuchukua hatua, Bunge lifanye kazi yake kwa kuwa ndio chombo chenye mamlaka kisheria ya kuwawajibisha, Nape na Kinana wasome katiba ili kujua nani ambaye anapaswa kuwawajibisha hawa Mawaziri," alisema.
Aliongeza kuwa, vikao vya Kamati Kuu ya CCM vinaweza kuwalinda Mawaziri hao na kumtaka Rais Kikwete atekeleze ahadi yake ya kukutana na vyama vya upinzani mara tatu kabla ya kura ya maoni.
Akizungumzia Rasimu ya Mabadiliko ya Sera ya Tabia Nchi, Bw. Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema asilimia 70 ya majanga ya asili ambayo yanatokea nchini na duniani yanasababishwa na hewa ukaa ambayo inasababishwa na matumizi ya mafuta.
Al i s ema wa n a n c h i wo t e wanakaribishwa kutoa maoni ambayo yataingizwa katika rasimu hiyo na mwisho wa kutoa maoni ni Desemba 31 mwaka huu ambapo mawazo yao yatasaidia kutengeneza rasimu nzuri.
Kwa upande wake, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dkt. Rodrick Kambangila, alisema ameamua kung'atuka katika nafasi zote za uongozi wa chama hicho na kuwa kada wa CHADEMA.
"Naanimi kupitia vyama vya siasa Serikali inaweza kuondoa urasimu katika Sekta ya Afya na kuwezesha upatikanaji wa huduma bora kwa Watanzania.
"Ipo haja ya kubadilisha mfumo unaotumika katika sekta hii kwa sasa ili kupata sera madhubuti zinazomjali Mtanzania maskini ambaye hawezi kumudu gharama," alisema. MAJIRA
No comments:
Post a Comment