RASIMU YA KATIBA MPYA
|
KAMA Watanzania
wataridhia rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
iliyozinduliwa wiki iliyopita na Tume ya Mabadiliko ya Katiba bila
mabadiliko, itapiga marufuku Rais wa Tanzania kujihusisha kwa namna yoyote na
chama chochote cha siasa kikiwemo chama chake, Tanzania Daima Jumapili
limebaini.
Pendekezo hilo limo
katika Ibara ya 69 ya rasimu hiyo inayobainisha madaraka na majukumu ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali
na Amiri Jeshi Mkuu.
Ibara ya 69(4) ya
rasimu hiyo inabainisha kuwa: “Katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa
ibara hii, rais ataepuka kujinasibisha, kwa namna yoyote ile, na chama
chochote cha siasa au kundi lolote kwa namna ambayo inaathiri umoja wa
wananchi.”
Katika ibara
inayotangulia, ya 68(2) Rais wa Jamhuri ya Muungano ametajwa kuwa atakuwa
Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, na kwa mamlaka hayo
kwanza atakuwa alama na taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu
wake, pili atakuwa alama ya umoja na uhuru wa nchi na mamlaka yake na mwisho
atakuwa na dhamana ya kukuza na kuhifadhi umoja wa kitaifa.
Lengo la kuwekwa
marufuku hiyo limebainishwa wazi na ibara yenyewe kuwa ni kulinda umoja wa
wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na umoja wa kitaifa kwa ujumla.
Kama rasimu hiyo
itapitishwa katika kura ya maoni mwakani, rais hataruhusiwa kushiriki katika
mikutano ya kawaida ya hadhara, katika mikutano ya kampeni za uchaguzi au
shughuli nyingine yoyote ya chama chake, isipokuwa vikao vikuu vya maamuzi
vya chama chake.
Wachambuzi wa
masuala ya siasa wanasema kuwa kama kifungu hicho kitakubaliwa kama kilivyo,
litakuwa pigo kubwa kwa chama tawala nchini - Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ambacho kimekuwa kikiwatumia wanachama wake ambao ni viongozi wa serikali,
akiwemo rais kujinufaisha kisiasa.
Kwa muda mrefu tangu
kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, vyama vya upinzani
vimekuwa vikiwalalamikia viongozi wa serikali kutumia nafasi zao serikalini
kufanya kazi za siasa za CCM, hususan nyakati za uchaguzi.
Viongozi wa serikali
ambao wamekuwa wakilalamikiwa ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muunagno wa
Tanzania, mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ambao wamekuwa
wakitumia nafasi zao serikalini kuifanyia kampeni CCM kwa kutumia rasilimali
za umma.
Aidha, kumekuwepo
malalamiko kama hayo dhidi ya marais wastaafu, akiwemo mwasisi na Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama
vingi wa mwaka 1995, alisimama kumfanyia kampeni aliyekuwa mgombea urais wa CCM,
rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Kilicholalamikiwa
zaidi ni kauli yake kwamba; “siwezi kuiachia nchi yangu ikichukuliwa na mbwa”
iliyowakera viongozi wa upinzani kwa kufananishwa na mbwa, hususan aliyekuwa
mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema aliyekuwa
akipewa nafasi kubwa ya kushinda.
Wachambuzi wa
masuala ya siasa wanasema kwa kiasi kikubwa kauli hiyo ya Mwalimu Nyerere
iliathiri na kuteteresha heshima yake mbele ya umma wa Watanzania.
CHANZO TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment