Pages

June 16, 2013

HUZUNI STARS YACHAPWA 4-2, IVORY COAST YACHUKUA TIKETI YETU KWENDA BRAZIL 2014



Thomas Ulimwengu wa Tanzania, akimtoka Suleiman Bamba wa Ivory Coast
Na Mahmoud Zubeiry. IVORY Coast imefanikiwa kusonga hatua ya pili na ya mwisho katika kuwanai tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia, baada ya kuifunga Tanzania mabao 4-1 jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Kundi C kanda ya Afrika.

Kwa ushindi huo, Ivory Coast imetimiza pointi 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote katika kundi hilo na sasa itasubiri kucheza na mmoja wa washindi wengine wa makundi mengine tisa ili kuwania kwenda Brazil mwakani.

Tanzania inabaki na pointi zake sita, huu ukiwa mchezo wa kwanza kufungwa nyumbani katika kampeni hizi na Morocco bila kuhusisha matokeo yake na Gambo, ina pointi tano.  

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mehdi Abid aliyesaidiwa na Hamza Hammou, Bauabdallah Omar wote kutoka Algeria, hadi mapumziko Ivory Coast tayari walikuwa mbele kwa mabao 3-2.

Stars ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao mfungaji Amri Ramadhani Kiemba dakika ya kwanza tu aliyepokea pasi ya Mbwana Ally Samatta kufuatia mpira wa kurushwa na Erasto Edward Nyoni kusababisha kizazaa langoni mwa Tembo wa Abidjan.

Nyoni alirusha kama amepiga kwa mguu karibu kabisa na kibendera cha kona kufuatia beki Suleiman Bamba kumpitia Thomas Ulimwengu na kutoa nje na mpira ukaokolewa kabla ya kumkuta Samatta aliyempelekea mfungaji.

Ivory Coast wakasawazisha bao hilo dakika ya 15 kupitia kwa Lacina Traore baada ya mabeki wa Stars kuzembea kuokoa na Yaya Toure akafunga la pili kwa mpira wa adhabu dakika ya 23, nje kidogo ya eneo la hatari.

Bao hilo lilitokana na wachezaji wa Stars kupanga ukuta wao vibaya na kumpoteza maboya kipa wao, Juma Kaseja.

Stars ilirudi mchezoni na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 35 mfungaji Ulimwengu aliyeunganisha krosi maridadi ya Shomary Kapombe.

Hata hivyo, Ivory Coast wakapata penalti rahisi baada ya Gervinho kujiangusha wakati anakabiliana na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ Yaya Toure akaenda kumtungua Kaseja dakika ya 43.

Kipindi cha pili Stars ilikianza vizuri na kushambulia mara nyingi langoni mwa Ivory Coast, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen dakika ya 87 kumtoa kiungo Mwinyi Kazimoto na kumuingiza mshambuliaji Vincent Barnabas yaliigharimu Tanzania kwa kufungwa bao la nne na kupotea kabisa mchezoni. Baada ya kutoka Kazimoto, aliyetekeleza majukumu yake vizuri leo, Ivory Coast wakatawala sehemu ya kiungo na kutengeneza bao la nne lililofungwa na Bonny Wilfred dakika ya 88.

Pamoja na kufungwa, Stars ilicheza soka safi ya kuvutia na mabao yote yalitokana na makosa – na si kuzidiwa uwezo. 

Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe/Khamis Mcha dk 85, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Mwinyi Kazimoto/Vincent Barnabas dk 87, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Amri Kiemba.

Ivory Coast; Boubakar Barry, Arthur Boca, Didier Zakora, Solomon Kalou/Sio Giovanni, Gervais Yao, Jean Jarques Gosso Gosso, Alain Aurier, Lacina Traore/Bonny Wilfred, Yaya Toure, Geoffrey Serey na Suleiman Bamba/Nori Koffi Christian. 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...