Pages

June 22, 2013

CUF wakwama kuipindua CHADEMA


 Edson Kamukara, Dodoma
WABUNGE wa Chama cha Wananchi (CUF), jana walikwama kufanya mapinduzi ya kuongoza kambi rasmi ya upinzani, wakidai kuwa chama cha CHADEMA kinachoongoza kambi hiyo wabunge wake hawamo bungeni kwa wiki nzima.

Hoja hiyo iliibuliwa bungeni jana na Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwan (CUF), aliyeomba mwongozo wa Spika wa Bunge jana baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, akisema kwa saa 96 sasa kambi ya upinzani iko wazi, hivyo CUF wanatangaza rasmi kwamba kuna mapinduzi ndani ya Bunge kwa kambi hiyo kuongozwa na CUF.

Kauli ya Barwan ambaye alikuwa amekalia kiti cha kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe (CHADEMA) iliibua vicheko kwa wabunge wote ukumbini huku Spika wa Bunge, Anne Makinda naye akishindwa kujizuia akisema; “Kazi kweli kweli.”

Hata hivyo jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya Spika Makinda, kufafanua kuwa kwa mujibu wa kanuni, kambi ya rasmi ya upinzani ni wabunge wote wa upinzani na kuongeza kuwa hata hivyo vyama hivyo vimekuwa na misimamo tofauti katika kuongoza kambi hiyo kulingana na uwiano wao.

Alisema kwa sasa kambi hiyo inaongozwa na CHADEMA na kwamba licha ya CUF kukidhi kigezo cha kuwa na asilimia 12.5 ya wabunge, hivyo kuwa na sifa za kuunda kambi ya upinzani lakini wanaoiongoza (CHADEMA) hawajatangaza kuicha kazi hiyo.

Barwan jana alikaa sehemu ya Mbowe huku Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) alikalia kiti cha Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, kuonesha kuwa wabunge wa chama hicho wametwaa kambi kutoka kwa CHADEMA.

Wabunge wa CHADEMA wakiongozwa na Mbowe walikuwa jijini Arusha kuhudhuria mazishi na kuwafariji wafuasi wa chama chao waliofariki na kujeruhiwa katika tukio la mlipuko wa bomu lililotokea Jumamosi iliyopita wakati wa kuhitimisha mkutano wa kampeni za udiwani.

Chanzo:Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...