Pages

May 11, 2013

POLISI WATATU MBARONI KWA KUKUTWA NA FUVU LA MWANADAMU

 Morogoro
JESHI la polisi mkoani Morogoro linawashikilia askari polisi watatu na raia mmoja kwa kukutwa na fuvu la kichwa kinachodhaniwa kuwa cha mtu aliyeuawa hivi karibuni.

Askari hao inadaiwa walitaka kumbambikizia kesi mfanyabiashara aliyetambulika kwa jina moja la Mura anayefanya shughuli zake katika mji mdogo wa Dumila ulioko Kilosa mkoani Morogoro ili awape sh milioni 25.

Askari hao na raia huyo walitaka kiasi hicho cha fedha ili wasimfikishe polisi mfanyabiashara huyo.
Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa mtaa wa Mgudeni, Zaituni Kifutu, alisema kukamatwa kwa polisi hao kulitokana na wananchi kubaini mchezo wa kubambika fuvu hilo.

Fuvu hilo lilikutwa chini ya uvungu wa gari namba T370 CCZ mali ya Samson Mura mfanyabiashara wa maduka katika eneo la Dumila.

Kwa mujibu wa Kifutu, askari hao watatu na mwenzao inadaiwa walifika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo na kufanya upekuzi na baadaye walikwenda kwenye gari hilo ambapo walilitupa fuvu hilo chini ya uvungu wa gari.

“Nimefika hapa nikakuta hawa askari niliwatambua kwa jina moja moja la Madodo, Mudi, Nurani na Sharifu Hamisi aliyejitambulisha ni askari kutoka Mvomero.

Alibainisha askari hao wakiwa katika gari la mfanyabiasahara huyo walilizunguka mara kadhaa na ndipo Nurani na Hamisi waliibuka na mfuko huo waliohoji ni wa nani.

Aliongeza kuwa mfuko na swali hilo viliwafanya watu waliokuwa eneo la tukio kuwatilia shaka askari hao huku wakiwalazimisha wafungue mfuko waone kilichomo.

Mwenyekiti huyo alisema kulitokea mzozo mkubwa na walikubaliana waende katika kituo cha polisi Dumila ambako ilibainika askari hao hawakuagizwa kufanya upekuzi nyumbani kwa mfanyabiashara huyo.

“Pale kituoni mkuu wa kituo alikana kumfahamu Hamisi na walipombana zaidi alisema ni mchoma mikaa na askari aliokuwa nao eneo la tukio ni rafiki zake waliomuita waende kufanya dili,” alisema.

Kifutu aliongeza kuwa Hamisi aliweka bayana kuwa askari hao walimueleza kuwa wanakwenda kwa mfanyabishara huyo ili wambambikizie fuvu na hatimaye wamfungulie kesi.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mwigizaji nguli nchini Mohamed Fungafunga (Jengua), Musa Magisu na Charles Lyoba waliitaka serikali kutowapendelea askari hao.

“Huyu Madondo aliwahi kunibambika kesi ya mauji nikafungwa hadi walipokuja wanasheria kunitetea……nimetoka jela siku chache tu zilizopita, huyu askari kazoea mchezo huu,” alisema Salimu.

Akisimulia mkasa huo mfanyabiashara huyo akiwa nyumbani kwake alisema watu wanne walifika nyumbani kwake ambapo watatu kati yao anawafahamu kuwa ni polisi na kumuarifu wanataka kufanya upekuzi nyumbani kwake.
Aliongeza kuwa baada ya maelezo hayo aliwaruhusu watu hao kuendelea na kazi yao pasi na wasiwasi wowote licha ya kutokuwa barua yoyote inayowaonyesha kuagizwa kuifanya kazi husika.

Alisema mara baada ya kumaliza upekuzi huo walitoka nje na yeye aliamua kuelekea katika shughuli zake kwa kutumia gari lake lakini askari hao walimtaka ashuke kwenye gari hilo ili walichunguze.

“Wakati nikiwa chini ghafla Hamisi akainama na kuibuka na fuvu hilo akituhoji ni la nani? Sote tulishtuka sana lakini tulianza kuwatilia shaka kwa kuwa mfuko huo haukuwepo,” alisema.

Alibainisha mfumo huo ulisababisha tafrani na ikakubalika tuende kituo cha polisi lakini wakiwa njiani askari hao walimtaka awape sh milioni 25 ili wasilifikishe jambo hilo mbele za vyombo vya sheria.

Kaimu mkuu wa upelelezi wa Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, Asifiwe Uhimbe, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuwashikilia askari hao na raia waliyekuwa naye.

Alisema wanawashikilia askari hao ili kujua kwa kina zaidi kilichotokea nyumbani kwa mfanyabiashara anayedaiwa kutaka kubambikiwa kesi.

Kamanda Uhimbe aliwataka wananchi kuwa watulivu jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Alisema matukio ya askari kuwabambikia kesi wananchi yanawafanya wakose imani na Jeshi la Polisi ambalo halitokubali sifa hiyo mbaya na litawashughulikia wale wote watakaobainika kuhusika.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...