Ambrose Calist |
Arusha. Mtuhumiwa mmoja kati ya tisa waliotiwa mbaroni kuhusiana mlipuko wa bomu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arusha na kusomewa mashtaka 21 yakiwamo ya mauaji na kujaribu kuua.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kamuzora, mtuhumiwa huyo, Victor Ambrose (20), dereva wa Bodaboda na mkazi wa eneo la Kwa Mromboo, Arusha alisomewa mashtaka hayo yakiwamo matatu ya mauaji ya watu watatu waliofariki katika tukio hilo lililotokea Mei 5, mwaka huu.
Wakisoma kwa kupokezana hati ya mashtaka, Mawakili wa Serikali, Zachariah Elisaria na Haruna Matagane walidai Calist pia anatuhumiwa kwa makosa 18 ya kujaribu kuua.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kimyakimya akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa polisi na hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mashtaka yanayomkabili yanapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 27, mwaka huu itakapotajwa tena na mtuhumiwa amerudishwa mahabusu.
Saa moja kabla ya Ambroce kupandishwa kizimbani saa nne asubuhi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas aliitisha mkutano na waandishi wa habari kitendo ambacho kiliwafanya baadhi yao kushindwa kufuatilia vyema tukio hilo.
Waarabu waachiwa huru
Polisi imewaachia huru raia wanne wa kigeni waliokuwa wakishikiliwa kuhusiana na tukio hilo baada ya uchunguzi uliofanywa na Polisi wa Tanzania, Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na Polisi wa Kimataifa (Interpol) na kubaini hawakuhusika.
Kamanda Sabas aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa raia hao walikamatwa baada ya kutiliwa shaka walipoonekana wakitoka kwenye hoteli moja karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi Arusha, muda mfupi baada ya tukio hilo.
Raia watatu wa Falme za Kiarabu(UAE), walioshikiliwa na kuachiwa wamegundulika kuwa ni watumishi wa Serikali.
Kamanda Sabas aliwataja kuwa ni Abdul Azziz Mubarak (30), (Mamlaka ya Mapato), Fouad Saleem Ahmed Al Hareez Al Mahri (29), (Zimamoto) na Daeed Abdulla Saad (28), ambaye ni Askari wa Usalama Barabarani.
No comments:
Post a Comment