Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani
hapa limesema litaendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali katika kulinda
na kutetea haki za watoto. Hayo yalisemwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mary
Lugola ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha mwishoni
mwa wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa mtaani duniani.
Katika maadhimisho hayo
ambayo yalifanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa, Mrakibu huyo
Mwandamizi wa Polisi alisema jeshi la
polisi kupitia dawati la jinsia na watoto mkoani hapa limekuwa karibu sana
kiutendaji na mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya serikali kama vile Mkombozi,
CCR, Action For Children n.k katika kutetea na kulinda haki za watoto wa
mitaani.
Mrakibu huyo Mwandamizi
wa Polisi ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha alisema
mbali na jeshi hilo kujihusisha katika kutetea na kulinda haki za watoto wa
jamii hiyo, pia linasaidia kuinua na kuibua vipaji vya watoto hao kupitia
programu ya MWONGORIKA ya Polisi jamii ambayo inajihusisha na michezo kwa
vijana.
Alisema kupitia Dawati
hilo, jeshi la polisi limeweza kuwahudumia watoto wa mitaani kwa kushirikiana
na mashirika hayo ili kuwawezesha waishi katika mazingira salama na kupata
mahitaji muhimu.
“Kwa mfano
tumeshawahi kuwaunganisha na wazazi wao pamoja na kuwasafirisha kwenda makwao
watoto waliokuwa tayari kurudi ”. Alisema Bi. Lugola.
Alimalizia kwa kusema
kwamba Dawati la Jinsia na watoto huwa linahakikisha linapata taarifa za watoto
walioathirika na pia wale wote wanaowanyanyasa watoto hao wanachukuliwa hatua
za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Nalo shirika la Mkombozi
kupitia risala yao iliyosomwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Shirika hilo Bi.
Doris Cornell alisema kwamba ujumbe wa mwaka huu katika kuadhimisha siku hiyo
ni “Nyumbani Mtaani Nyumbani” ikiwa na maana ya kwamba, mtoto atatoka nyumbani
kwenda mtaani na kisha atarudi nyumbani.
Alisema lengo la siku
hiyo ni kuwapa jukwaa watoto waishio na kufanya kazi mtaani wakiungana na
wengine duniani kote kupaza sauti ili haki zao zisiipuzwe.
Bi. Doris alisema watoto
waishio mitaani na kulala mitaani wanazofursa na haki sawa na watoto wengine
duniani na kwamba wana haki ya kuishi, kulindwa, kuendelea na kushiriki katika
mambo yanayogusa maisha yao kama ilivyoainishwa katika mkataba wa Kimataifa wa
haki za watoto kifungu cha 4.
Risala hiyo ilieleza
sababu za kuwepo kwa watoto hao mitaani ni pamoja na kukosa haki za msingi
(chakula, malazi, mavazi, ulinzi, elimu, upendo, matibabu n.k) kutoka katika
familia zao, kufiwa na mzazi mmoja au wote wawili.
Sababu nyingine ni
vitendo vya unyanyasaji na ukatili waliofanyiwa katika jamii au familia, kipato
duni katika familia/wazazi/walezi, utumikishwaji wa watoto (ajira za watoto),
kubaguliwa na kunyang’anywa mali za wazazi wao.
Siku hiyo ambayo huwa
inaadhimishwa katika nchi 130 duniani, Tanzania na Uingereza ikiwa ni miongoni
mwa nchi hizo, ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa ngazi ya wilaya
pamoja na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Arusha Mkaguzi Msaidizi wa
Polisi Maria Maswa.
No comments:
Post a Comment