.jpeg)
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Mkoa wa Pwani imesema iko tayari kutoa ushirikiano katika kuimarisha Bandari Kavu ya Kwala na kuongeza matumizi ya reli katika usafirishaji wa makasha ya mizigo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, wakati wa mazungumzo yake na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), iliyofanya ziara mkoani humo kwa lengo la kukagua miundombinu ya reli na huduma za usafirishaji wa makasha kwenda Bandari Kavu ya Kwala.
Nyongo amesema kuimarishwa kwa Bandari Kavu ya Kwala pamoja na kuongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo kupitia reli kutasaidia kupunguza msongamano wa magari makubwa na foleni katika Jiji la Dar es Salaam.
Amesema Mkoa wa Pwani kwa sasa unapokea wawekezaji wengi wanaokuja kuwekeza katika sekta ya viwanda, hali inayochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuongeza mahitaji ya huduma bora za usafirishaji.
Amesema kutokana na kasi hiyo ya maendeleo, kuna umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya barabara na reli ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Aidha, amelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kuimarisha uwezo wake wa kusafirisha makasha na shehena nyingine kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Bandari Kavu ya Kwala, ili wafanyabiashara na wasafirishaji waweze kuchukua mizigo yao Kwala na kuisafirisha kwenda maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Amesema matumizi makubwa ya reli katika usafirishaji wa mizigo yatapunguza idadi ya magari makubwa yanayoingia na kutoka Dar es Salaam, hivyo kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji.
Nyongo amesema uanzishwaji na uimarishaji wa Bandari Kavu ya Kwala ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kukuza uchumi na kuboresha huduma za usafirishaji nchini.
“Tunataka watendaji waumize vichwa katika kuhakikisha miundombinu ya reli inatumika kikamilifu na kuleta tija iliyokusudiwa. Changamoto zinapojitokeza, watendaji wanapaswa kuwa wa kwanza kuzishughulikia,” amesema Nyongo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC) Nahodha Mussa Mandia, amesema ziara hiyo imelenga kukagua miundombinu ya bandari kavu iliyopo mkoani Pwani ili kutathmini hali yake, uwezo wa kuhudumia shehena na mchango wake katika kurahisisha shughuli za usafirishaji na biashara.
Amesema ziara hiyo pia inalenga kubaini fursa zilizopo katika bandari Kavu ya Kwala, katika kupunguza msongamano wa shehena na magari katika Bandari ya Dar es Salaam,
Amesema kuondosha mizigo na makasha katika Bandari ya Dar es Salaam kunaongeza ufanisi wa huduma wa katika kuhudumia Meli
Naye, Meneja wa Stesheni ya Ruvu wa TRC, Dawa Onyango, amesema shirika hilo linaendelea kuboresha huduma za reli, ambapo kwa sasa reli hiyo ina uwezo wa kuhudumia makasha 100 ya mizigo kutoka Bandari za Tanga na Dar es Salaam.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
إرسال تعليق