Na Mwandishi Wetu.

MWENYEKITI wa Makampuni ya Mati Group of Companies Ltd, David Mulokozi, amechangia Sh milioni 100 kupitia kampuni ya Mati Super Brands Ltd pamoja na familia yake binafsi, kusaidia miradi ya maendeleo ya Jimbo Katoliki la Mbulu.

Mchango huo umetolewa katika harambee iliyofanyika ndani ya Dekania ya Babati, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya Almasi ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki la Mbulu, ambapo Mulokozi alikuwa mgeni rasmi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mulokozi alisema mchango wake umetokana na imani yake kwa Mungu, akieleza kuwa kila alichonacho ni zawadi kutoka kwake na kwamba kuchangia maendeleo ya Kanisa na nyumba za ibada ni njia mojawapo ya kumshukuru Mungu.
Alisema kusaidia shughuli za maendeleo ya Kanisa kwake ni sehemu ya imani na nadhiri yake mbele za Mungu, huku akihimiza jamii kuendeleza utamaduni wa kujitolea kwa kuchangia miradi ya maendeleo kulingana na uwezo wa kila mmoja.

Aliongeza kuwa maendeleo ya taasisi za kidini yanahitaji ushirikiano wa waumini, wadau na watu wenye mapenzi mema, akisisitiza kuwa kila mchango unaotolewa kwa moyo wa kujitolea una nafasi muhimu katika kufanikisha malengo yaliyowekwa.

Akisoma taarifa ya harambee hiyo, Dekano wa Dekania ya Babati, Reginald Kimati, alisema jumla ya fedha zilizopatikana pamoja na ahadi zilizotolewa zimevuka Sh milioni 200 zilizolengwa kukusanywa katika dekania hiyo.

Alisema Jimbo Katoliki la Mbulu limeweka lengo la kukusanya Sh bilioni mbili kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa hosteli za malazi, ukumbi, jukwaa la kudumu kwa ajili ya maadhimisho ya kijimbo pamoja na kuchangia ujenzi wa kituo cha kichungaji mjini Babati.
Kimati alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuboresha mazingira ya huduma za kichungaji na kuongeza uwezo wa Kanisa kuhudumia waumini pamoja na wadau mbalimbali watakaoshiriki shughuli za kijimbo.

Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu, Mhashamu Anthony Lagwen, alimpongeza Mulokozi kwa mchango wake na moyo wa kujitolea, akisema hatua hiyo ni mfano mzuri wa ushirikiano katika kuendeleza miradi ya Kanisa.
Alisisitiza kuwa fedha zitakazokusanywa zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha miradi iliyopangwa inatekelezwa na kuleta manufaa kwa Kanisa na waumini wake.

Aidha, aliwahimiza waumini na wadau wengine kuendelea kushiriki katika kuchangia miradi hiyo ili kufanikisha lengo la Sh bilioni mbili na kuhakikisha maandalizi ya maadhimisho hayo yanakamilika kwa wakati.
 Maadhimisho ya Jubilei ya Almasi ya miaka 75 ya Jimbo Katoliki la Mbulu yanatarajiwa kufanyika Machi 2028, yakikumbuka historia ya kuanzishwa kwa jimbo hilo Machi 25, 1953.