NDEJEMBI: TEKNOLOJIA ITUMIKE KUONGEZA UFANISI WA UKUSANYAJI WA MAPATO


Na Mwandishi Wetu, Arusha

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amesema teknolojia inapaswa kuwa nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi na usawa wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili nchi ziweze kufadhili shughuli na vipaumbele vya maendeleo kupitia rasilimali zake.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo, Oktoba 6, 2026, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi wa Mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA), unaofanyika katika Ukumbi wa Gran Melia, jijini Arusha.

Amesema mfumo mzuri wa kodi unapaswa kuwa wa uhakika, kuwezesha biashara halali, kuhimiza uwekezaji na urasimishaji wa shughuli za kiuchumi, sambamba na kuwezesha sekta binafsi kutumia nafasi yake katika kuchagiza mabadiliko ya kiuchumi kama ilivyokusudiwa chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

“Ukusanyaji wa kodi haupaswi kuzuia shughuli za kiuchumi zenye tija, bali unapaswa kuunga mkono shughuli hizo,” amesema.

Makamu wa Rais amesema ukuaji endelevu wa mapato unapaswa kutokana na ukuaji wa uchumi, urasimishaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza wigo wa walipa kodi, kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari, matumizi bora ya data na teknolojia, pamoja na kuwa na mfumo wa kodi unaokua sambamba na uchumi.

Aidha, amesema ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi unapaswa kutoa matokeo ya vitendo, huku akieleza kuwa mabaraza kama CATA yanapaswa kusaidia katika kupima utendaji, kubadilishana taarifa, kuimarisha usaidizi wa kiutawala, kujifunza kutoka kwenye mifumo inayofanya vizuri na kutafsiri uzoefu wa kimataifa kuwa mageuzi ya ndani yanayoweza kupimika.

Amesema Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano wa kikodi baina ya mataifa na inaendelea kuimarisha ushiriki wake katika mifumo ya kimataifa, ikiwemo kubadilishana taarifa za kodi na usaidizi wa masuala ya kiutawala baina ya nchi.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Julai 2026, Tanzania ilitajwa kimataifa kuwa inatimiza vigezo vya kimataifa katika ulipaji kodi pamoja na viwango vya uwazi na ubadilishanaji wa taarifa pale zinapohitajika.

Amesema hatua hiyo ni faraja ya maendeleo, lakini pia ni ukumbusho kwamba viwango vya kimataifa vinaendelea kubadilika, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha mifumo ya kisheria na uwezo wa kitaasisi.

Makamu wa Rais amesema Rais Samia amekuwa akisisitiza matumizi ya teknolojia, usawa, ushiriki wa walipa kodi na utoaji wa huduma bora katika usimamizi wa mapato.

Amesema matarajio ya Serikali ni kuwa na mifumo ya kisasa itakayopunguza mwingiliano usio wa lazima, kuongeza uwazi, kusaidia utekelezaji unaozingatia hatari na kuwawezesha walipa kodi wanaofuata sheria kutimiza wajibu wao kwa urahisi.

Akizungumzia kaulimbiu ya mkutano huo, “Kutumia Teknolojia kwa Ukusanyaji Bora wa Mapato” (Leveraging Technology for Efficient Revenue Collection), Makamu wa Rais amesema teknolojia inapaswa kuwezesha Serikali kurahisisha ulipaji kodi kwa hiari, kuwatambua wale wasiokidhi wajibu wao wa kodi, kupunguza gharama za kiutawala, kuboresha huduma kwa walipa kodi na kuwezesha biashara halali.

CATA YATAJWA KUWA JUKWAA LA KUJIFUNZA

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA), Dkt. Abu Tariq Jamaluddin, amesema CATA ni jumuiya ya viongozi na wataalamu wa masuala ya kodi wanaojifunza kutoka kwa kila mmoja na kukua pamoja.

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, CATA imeendelea kuimarisha jumuiya hiyo kupitia programu za uongozi, mipango na teknolojia, pamoja na mijadala inayofanyika kwa njia ya mtandao kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu.

Awali, Kiongozi mwenyeji wa mkutano huo ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA Yusuph Mwenda, amemshukuru Rais Samia kwa uongozi wake katika kuimarisha mabadiliko ya kidijitali yanayowezesha ukusanyaji wa kodi kwa urahisi na ufanisi.

Amesema Serikali imewekeza katika mifumo kadhaa ya kisasa, ikiwemo Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS), wenye jumla ya moduli 17.

Amesema miongoni mwa moduli hizo ni mfumo wa utoaji ankara za kielektroniki, ambao sasa unawawezesha walipa kodi kutoa ankara hizo bila kulazimika kutumia mashine halisi.

Mkutano huo unawakutanisha zaidi ya wataalamu na viongozi 400 kutoka nchi 48 za Jumuiya ya Madola, ukiwa na lengo la kubadilishana maarifa na uzoefu katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa kodi kwa kutumia teknolojia za kisasa.






Post a Comment

Previous Post Next Post