SIHA:Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Nkoba Mabula ameeleza kuwa maandalizi ya mapema kukabiliana na Mvua za El Nino yanaweza kupunguza athari kubwa zinazoweza kujitokeza pindi mvua hizo zitakaponyesha ndani ya maeneo ya Hifadhi dhidi ya shughuli za uhifadhi na utalii.
Ameyasema hayo Oktoba 21, 2026 alipotembelea Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro katika malango ya Lemosho na Londorosi kupokea taarifa ya utekelezaji wa mikakati ya Hifadhi dhidi ya kukabiliana na mvua hizo na athari zake.
"Maandalizi tunayoyafanya ndiyo yatakayotusaidia wakati wa Mvua za El Niño, tujitahidi kuboresha miundo mbinu yetu ili tusipoteze watalii wengi wakati wa mvua hizo kuepuka kupoteza mapato" alisema Mabula.
Awali akitoa wasilisho la utekelezaji wa maandalizi dhidi ya kukabiliana na Mvua za El Niño Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza Eng. Selemani Ntemi alieleza kuwa Hifadhi inaendelea na ufunguzi wa mitaro ya maji, uwekaji wa changarawe maeneo korofi, ukaguzi wa vivuko, ujenzi wa minara ya mawasiliano ya radio na uundwaji wa timu za uokoaji.
Aidha Bw. Mabula alifanikiwa kutembelea kituo cha Shira kujionea shughuli za utalii zinazoendelea, maeneo ya uokoaji wa ndege (Helipad) na athari za moto zilizojitokeza huku akihimiza matumizi ya teknolojia ya ndege nyuki kwaajili ya kukabiliana na ujangili, moto na viashiria vyake.




إرسال تعليق