KIWANDA CHA VILIPUZI KISARAWE KITAPUNGUZA UTEGEMEZI WA BIDHAA KUTOKA NJE - NYONGO


Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema uwepo wa kiwanda cha baruti na vilipuzi cha Ideal Detonators Tanzania Limited wilayani Kisarawe utasaidia kupunguza gharama na utegemezi wa uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.

Nyongo amesema bidhaa hizo ni muhimu katika shughuli mbalimbali za miundombinu, ikiwemo ulipuaji wa miamba na uchimbaji wa madini, hivyo uzalishaji wake nchini utasaidia kurahisisha upatikanaji wake.

Ameyasema hayo Oktoba 6, 2026, baada ya kukagua kiwanda hicho wakati wa ziara yake wilayani Kisarawe, ambapo alisema miaka ya nyuma hakukuwa na sheria zilizowezesha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza vilipuzi nchini.

Hata hivyo, alisema Serikali imefanya maboresho ya sheria na kuweka mazingira yaliyowezesha kuanzishwa kwa viwanda hivyo nchini.

Nyongo aliishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira yaliyowezesha uwekezaji huo, akisisitiza kuwa Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa yenye fursa kubwa za viwanda na uwekezaji.

Alisema mkoa utaendelea kushirikiana na halmashauri kuhakikisha wawekezaji wanapata mazingira rafiki ya uzalishaji, ikiwemo upatikanaji wa huduma muhimu za maji na umeme.

Aidha, Nyongo amekemea uvamizi wa maeneo ya wawekezaji na migogoro ya ardhi, huku akiwataka viongozi, wakiwemo wabunge, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uwekezaji badala ya kuwa vikwazo kwa wawekezaji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, alisema kiwanda hicho kinatarajiwa kutoa ajira kwa vijana, hususan wazawa, pamoja na kuongeza mapato na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Jafo pia alisema uwepo wa kituo cha kupoozea umeme katika eneo hilo utasaidia kuongeza uwezo wa usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali.

Alipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa hatua zinazochukuliwa katika kuendeleza sekta hiyo, akisema uwekezaji huo unaonesha utekelezaji wa dhana ya kuongeza thamani ya madini kwa kuzalisha bidhaa zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji badala ya kuishia kwenye uchimbaji pekee.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, alisema wilaya hiyo inaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili kuharakisha ujenzi na uanzishaji wa viwanda.

Alifafanua kuwa kwa sasa Kisarawe ina viwanda viwili vya baruti na vilipuzi, ambavyo ni Solar Intracom Chemicals (Solar Nitrochemicals Limited), ambacho tayari kimeanza uzalishaji, na Ideal Detonators Tanzania Limited, kinachoendelea na maandalizi ya kuanza uzalishaji.

Magoti alisema Ideal Detonators ni miongoni mwa viwanda vikubwa vya aina hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku uwekezaji wake ukifikia zaidi ya Sh bilioni 15.

“Wilaya hiyo iko tayari kwa mapinduzi makubwa ya viwanda na inatarajia kupokea uwekezaji mwingine katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, zikiwemo nondo, spika na viwanda vya kutotolesha kuku,” alisema Magoti.

Meneja Mkuu wa Ideal Detonators Tanzania Limited, Ramadhan, alisema lengo la kiwanda hicho ni kutoa suluhisho la upatikanaji wa bidhaa za vilipuzi zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji madini na shughuli nyingine zinazohitaji matumizi ya vilipuzi.






Post a Comment

Previous Post Next Post