. Akagua Ujenzi wa soko la Kilombero na Kwa Mrombo na kuagiza kipaumbele kiwe kwa Wafanyabiashara waliopisha ujenzi na wenye uhitaji wa maeneo ya kufanyia biashara
. Aagiza Jiji kuboresha huduma katika Masoko na LATRA wahakikishe route za magari kufika katika masoko
Ahimiza usafi kuwa ajenda ya kila Mwananchi
. Awatahadharisha wafanyabiashara kuchukua tahadhari za Mvua za Elniño
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amewataka wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo hatarishi, ikiwemo pembezoni mwa barabara, kuhamia katika masoko yanayojengwa na Serikali kwa ajili ya usalama wao na ustawi wa biashara mkoani hapa.
Mhe. Makalla ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Oktoba 2, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa masoko ya Kilombero na Kwa Mrombo jijini Arusha, ambapo amesisitiza wafanyabiashara waliopisha maeneo kwa ajili ya ujenzi kupewa kipaumbele katika masoko hayo pale yatakapokuwa yamekamilika.
Aidha, ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhakikisha masoko hayo yanakamilishwa yakiwa na huduma muhimu, ikiwemo maji, vyoo, umeme, barabara na mazingira bora ya biashara, akiiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuhakikisha kunakuwa na usafiri wa umma (route) unaofika kwenye masoko hayo ili kurahisisha biashara na kuongeza mzunguko wa watu.
Aidha Mhe. Makalla amewataka wananchi kutunza na kufanya usafi wa mazingira kila wakati, huku akilitaka Jiji la Arusha kuweka mapipa ya taka kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu na kuhakikisha taka zinaondolewa kwa wakati.
Mhe. Makalla ametumia ziara hiyo pia kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa mwezi Oktoba ili kunusuru maisha na mali zao pale mvua hizo zitakapokuwa na athari huku Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Dkt. Wilfred Soileli, akimpongeza Mhe. Makalla kwa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo suala ambalo limeongeza kasi katika utekelezaji wa Ilani ya CCM.





Post a Comment