Na Oscar Assenga, Pangani
Jahazi la MV Tarawanda lililokuwa likitoka Wilaya ya Pangani mkoani Tanga likielekea Mkokotoni, Zanzibar, likiwa limebeba tani 20 za mizigo mbalimbali ikiwemo mihogo, ndizi, machungwa na nazi, limezama katika eneo la Nungwi kutokana na hali mbaya ya hewa pamoja na giza.
Jahazi hilo lilikuwa na watu sita wakiwemo nahodha na wafanyakazi wa chombo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Jeshi la KMKM Zanzibar kwa viongozi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) jijini Dar es Salaam, ambao waliwasiliana na Kituo cha Utafutaji na Uokozi Baharini (MRCC) Dar es Salaam, chombo hicho kilipopata ajali kilikutwa na watu wapatao 12.
Kati ya hao, watu saba waliokolewa na boti za uokozi kutoka Mkokotoni, Nungwi na Ushongo na kupelekwa katika Hospitali ya Kivunge, Kaskazini Unguja.
Katika ajali hiyo, watu watatu bado hawajapatikana huku miili ya watu wawili ikiwa imeokotwa katika eneo la Nungwi na kupelekwa Bandari ya Mkokotoni Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kufika Wilaya ya Pangani, Kaimu Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Tanga, Mhandisi Christopher Mlewa, alisema chombo hicho kilitoka Pangani kikielekea Mkokotoni lakini kilipata ajali katika eneo la Nungwi baada ya kupoteza mwelekeo kutokana na upepo mkali pamoja na giza.
Alisema nahodha wa chombo hicho hawakuzingatia utabiri wa hali ya hewa ambao wamekuwa wakikumbushwa mara kwa mara kuufuata kabla ya kuanza safari.
Awali, Afisa Mwandamizi wa Meli kutoka TASAC, Selemani Puzzy, alisema shirika hilo limepokea kwa masikitiko taarifa za ajali hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari ili kupunguza madhara ya ajali kama hizo.
Alisema kwa mujibu wa sheria za Tanzania hakuna chombo cha mizigo kinachoruhusiwa kusafirisha abiria kwenda Unguja, isipokuwa vyombo vinavyotoka Bandari ya Tanga pekee. Alieleza kuwa vyombo vinavyotoka Bandari za Kigombe, Pangani na maeneo ya Mkwaja vina leseni za kusafirisha mizigo na wanyama tu, si abiria.
“Imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya vyombo kuondoka na watu zaidi ya wanaoruhusiwa. Unakuta chombo kina wafanyakazi sita lakini ajali ikitokea ndani wanapatikana watu hadi 12, jambo ambalo si sahihi,” alisema.
Aliongeza kuwa baadhi ya manahodha wamekuwa wakipakia abiria kinyume cha sheria kwa siri, hali inayoweza kusababisha vifo bila hata kujulikana taarifa sahihi za waathirika.
“Ni muhimu kujenga utamaduni wa kusajili watu wote wanaosafiri. Kubeba abiria kwenye vyombo vya mizigo ni kosa na kunaweza kusababisha vifo. Hata mfanyabiashara aliyekuwa akisafirisha mbao alipanda kwenye jahazi hilo, jambo ambalo si sahihi,” alisisitiza.
Puzzy pia alitoa wito kwa wamiliki wa vyombo na wasafiri kufuatilia utabiri wa hali ya hewa kabla ya safari, kuhakikisha vyombo vina vifaa vya uokoaji na kutumia vyombo vilivyoruhusiwa kisheria kwa usafiri wa abiria.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Adv. Agape Fue, alilishukuru Shirika la TASAC kwa kutoa elimu kwa wadau wa usafiri wa majini ili kuwakumbusha umuhimu wa kufuata sheria na kanuni za usalama baharini.
Alisema usalama ni msingi muhimu wa maendeleo ya uchumi na kuwataka wamiliki wa vyombo kusajili vyombo vyao pamoja na kuvitumia kwa shughuli zilizoidhinishwa tu.
Naye mmiliki wa Jahazi la Salamati kutoka Pangani, Mngwali Haji Ussi, alisema miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo ni mtoto wa dada yake.
Alisema kabla ya tukio hilo alimwonya kijana huyo asiichezee bahari kutokana na hatari zake, lakini alimjibu kuwa amepitwa na wakati.
“Serikali inapaswa kuwachunguza na kuwahakiki manahodha wote wanaoendesha vyombo vya baharini ili kuhakikisha wana leseni halali,” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, alisema siku ya ajali alimtafuta mjomba wake kwa simu ili kumueleza kuhusu hali mbaya ya bahari na kumshauri asiende safari, lakini hakupatikana.
“Hapa kwetu mara nyingi tunatazama nyota kabla ya kuanza safari. Kama hakuna nyota baharini huwa hawatoki kwa sababu wanajua bahari si shwari. Mpaka sasa mjomba wangu bado sijamuona,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa Makuli Wilaya ya Pangani, Waziri Hamisi, aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwepo kwa boti ya uokozi katika maeneo hayo ili kusaidia wakati majanga kama hayo yanapotokea.





إرسال تعليق