Kituo cha Afya Kaloleni kupandishwa hadi kuwa hospitali ya wilaya

Waziri wa Afya,Mohamed Mchengerwa akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha,John Kayombo katika Kituo cha Afya Kaloleni.


 Waziri Mchengerwa aagiza Kituo cha Afya Kaloleni kipandishwe hadhi.

Filbert Rweyemamu,Arusha

Waziri wa Afya,Mohamed Mchengerwa ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Arusha kuanza mchakato wa maombi ya kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Kaloleni kuwa hospitali ya wilaya baada ya kukamilisha ujenzi wa jengo jipya lenye ghorofa tano litakalopunguza msongamano wa wagonjwa.

Hatua hiyo imetokana na msongamano mkubwa wa wagonjwa alioukuta leo Jumatatu,Januari 26,2026 katika ziara yake kukagua utendaji kazi wa Kituo hicho kilichopo katikati ya Jiji na kutatua changamoto zinazokikabili.

“Huu msongamano ni mkubwa nataka mgonjwa akija ahudumiwe kwa wakati kisha aendelee na majukumu ya kiuchumi,lakini ninavyoona hapa haiwezekani leteni maombi ya kujenga Vituo vipya kwasababu serikali inayo fedha na haitaki watu wakae muda mrefu kwenye foleni kusubiri huduma za afya,”amesema Mchengerwa

Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha,John Kayombo amesema baada ya Kituo hicho kuweka vifaa vya kisasa vyenye thamani ya Sh.1.2 bilioni idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma za kiuchunguzi wameongezeka na Jiji lipo katika hatua za mwisho za kukamilisha manunuzi ya ujenzi wa jengo la ghorofa tano.

“Mheshimiwa Waziri ujenzi wa jengo jipya la ghorofa tano kwenye eneo hili utakua mkombozi kwa wananchi ambao wana imani na huduma zinazotolewa katika Kituo cha Afya Kaloleni,mchakato umeshaanza na ujenzi utagharamiwa na mapato ya ndani ya halamshauri,”amesema Kayombo

Waziri Mchengerwa baada ya kukagua vifaa tiba vya kisasa na kuridhishwa na uboreshaji wa huduma zinazotolewa ameagiza Kituo hicho kipandishwa hadhi kuwa hospitali ya wilaya hatua itakayoifanya Jiji la Arusha kuwa na hospitali mbili za wilaya.

Amesema uwepo wa vifaa tiba vya kisasa ambavyo havipatikani kwenye baadhi ya hospitali za wilaya na huduma zinazotolewa  unakifanya Kituo hicho kiwe na hadhi ya kuwa hospitali ya wilaya hatua itakayopanua wigo wa utendaji kazi wake na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na haraka.

Kuhusu uhaba wa watumishi 40 katika Kituo hicho ameahidi kulifanyia kazi na kumwagiza Mkurugenzi wa Jiji kuajiri watumishi wa afya kwa ajira za muda hadi ufumbufu wa kudumu utakapopatikana.

Awali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha,Dk Maduhu Nindwa amesema uwepo wa vifaa tiba vya kisasa umeongeza maradufu idadi ya wagonjwa na hospitali imekua ikipata mapato ya Sh.61 milioni kila mwezi sawa na kiasi cha Sh 741 kwa mwaka.

Katika hatua nyingine,Mchengerwa amesema hatavumilia ukosefu wa dawa kwenye taasisi za afya za serikali kwasababu Bohari ya Dawa (MSD) inao uwezo wa kuhudumia hospitali ,Vituo vya afya na Zahanati na kuonya tabia ya baadhi ya madaktari wanaomiliki maduka ya Dawa kuwaelekeza wagonjwa kununua dawa badala ya maduka ya serikali.

Hii tabia ya baadhi ya madaktari wasio waaminifu sitaivumilia,serikali kupitia MSD inao uwezo wa kutoa dawa zinazohitajika kwenye hospitali zote za serikali,ninazo taarifa za Daktari mmoja katika hospitali ya Temeke mwenye duka la dawa jirani na hospitali namwagiza alitoe mara moja kabla sijamtoe yeye,”amesema Mchengerwa



Post a Comment

Previous Post Next Post