Raushan DesignShroff TemplatesMafiaXDesign

OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAZIDI KUIMARISHA UWEZO WA MAWAKILI WA SERIKALI


Dar es Salaam, 19 Machi 2025 — Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, amesema kuwa Ofisi yake imejizatiti katika kuhakikisha inaendelea kuboresha uwezo na utendaji wa Mawakili wa Serikali nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza umahiri na weledi katika utoaji wa huduma za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalum uliofanyika katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam, Mhe. Johari alibainisha kuwa mafunzo ya kitaalamu kwa Mawakili wa Serikali yatafanyika Arusha kuanzia tarehe 24 hadi 28 Machi 2025. Mafunzo haya yamelenga kuwawezesha mawakili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Mafunzo haya ni sehemu ya mpango wa kuendeleza wataalamu wa kisheria ndani ya Serikali, sambamba na kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria,” alisema Mhe. Johari.

Ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kusisitiza umuhimu wa kuwa na Mawakili wa Serikali wenye ujuzi wa hali ya juu ili waweze kulinda vyema maslahi ya taifa, hasa wakati huu ambapo Tanzania inafungua milango kwa wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu, mafunzo hayo yataendeshwa na wakufunzi waliobobea kutoka ndani na nje ya nchi, huku mada zitakazotolewa zikigusa maeneo muhimu kama vile uandishi na majadiliano ya mikataba ya kimataifa, usuluhishi wa migogoro ya biashara, pamoja na uandishi wa sheria.

“Tunahitaji kuwa na wanasheria wanaoendana na kasi ya ukuaji wa uchumi na uwekezaji. Ni lazima tuwe na maarifa ya kutosha katika maeneo kama masoko ya fedha, masoko ya mitaji, sheria za fedha za kigeni na masuala ya dhamana na hati fungani,” alieleza.

Katika kuimarisha uzalendo na kulinda maslahi ya taifa, Mhe. Johari alisema kuwa mafunzo haya pia yatakuwa jukwaa muhimu kwa Mawakili wa Serikali kujitathmini na kujijengea utayari wa kutoa huduma zenye tija kwa nchi.

Akihitimisha, Mhe. Johari aliwahimiza Mawakili wote wa Serikali ambao bado hawajajisajili kwa ajili ya mafunzo hayo kuhakikisha wanakamilisha usajili wao mapema, huku akizitaka Wizara, Taasisi na Halmashauri kuhakikisha zinawaruhusu mawakili wao kushiriki ipasavyo.

“Natoa wito kwa Mawakili wa Serikali kote nchini kuhakikisha hawakosi kushiriki mafunzo haya muhimu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mhe. Johari alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza miaka minne ya mafanikio makubwa tangu alipoingia madarakani, akieleza kuwa uongozi wake umeleta mabadiliko chanya katika sekta mbalimbali nchini.





Post a Comment

Previous Post Next Post